Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Katibu wa Hamasa wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM), Paul Makonda juzi alibanwa na aliyekuwa mshehereshaji wa mdahalo wa Katiba, Said Kubenea akimtuhumu kuhusika na vurugu zilizotokea katika mdahalo huo na kusababisha aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kushambuliwa.
Wakizungumza katika kipindi cha Agenda 2015 kinachorushwa na Televisheni ya Star Tv, Kubenea alisema Jumamosi iliyopita Makonda alikutana na vijana 23 katika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam na kuwalipa Sh50,000 kila mmoja ili wafanye vurugu katika mdahalo huo uliofanyika siku moja baadaye (Jumapili) kwenye ukumbi wa Hoteli ya Blue Pearl.
Katika kipindi hicho, Kubenea na Makonda walitupiana maneno makali huku kila mmoja akimtuhumu mwenzake. Makonda alienda mbali zaidi na kumfananisha Kubenea na mchekeshaji wa mfalme, kutokana na madai aliyokuwa akiyatoa dhidi yake.
Kubenea alieleza jinsi alivyomzuia Makonda kupanda katika jukwaa kuu alilokuwa amekaa Jaji Warioba baada ya kuibuka kwa vurugu huku akimtaka aeleze sababu za kumsogelea Jaji Warioba aliyekuwa akitolewa katika ukumbi huo na mlinzi wake.
“Tunajua kila kitu. Tunajua kuwa ulikutana na vijana hao 23 na baadaye ulikutana na wazee wawili ambao wote walikuonya kuwa unatumika na mambo unayoyafanya si mazuri. Katika hili nina ushahidi wa kutosha.”
Akijibu hilo, Makonda alisema alimkuta Jaji Warioba akiondolewa na mlinzi wa hoteli hiyo pamoja na mlinzi wake binafsi, alichokifanya ni kumtaka akimbilie upande mwingine kwa sababu watu waliokuwa wakitaka kumshambulia yeye (Makonda) walikuwa wakirusha chupa katika eneo ambalo alilokuwapo.
“Sikukutana na vijana na wala sijui hilo unalolizungumza. Unajua Kubenea unazungumza kama mchekeshaji wa mfalme. Mimi nikodishe vijana ili iweje?” alihoji Makonda.
Akizungumza na gazeti hili kuhusu tuhuma za kutumia vijana kufanya vurugu Makonda alisema, “Watanzania wamtazame Kubenea kwa makini. Kama aliniona nikikutana na vijana hao mbona hakuripoti popote mpaka anasubiri kuzungumza katika vyombo vya habari au kuandika katika magazeti.”
“Hao wazee anaowasema (anawataja kwa majina) muulizeni (Kubenea) baada ya kuniona nipo na vijana hao tukipanga kufanya vurugu walinichukulia hatua gani,” alisema.
Toa Maoni Yako:
0 comments: