Mhe Dr Lucy Nkya akizungumza na Waandishi wa habari muda mfupi uliopita ofisini kwake Faraja muda mfupi uliopita.
Jonas akihojiwa na waandishi wa habari kuhusiana na tukuo hilo. Muda mfupi uliopita.
Jonas akihojiwa na waandishi wa habari kuhusiana na tukuo hilo. Muda mfupi uliopita.
Na Mwandishi Wetu, Morogoro.
Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, Lucy Nkya amesema kuwa milio ya risasi iliyosikika ofisini kwake, ilitokana na mtoto wake Jonas Nkya, kuangusha bastola kwa bahati mbaya.
Nkya alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kusikika kwa milio ya risasi ofisini kwake huku kukiwepo kwa taarifa kwamba alivamiwa na mtoto wake huyo akidaiwa kutaka kumuua kwa kumpiga risasi.
Taarifa hizo zilidai kuwa mbunge huyo alikuwa na ugomvi wa kifamilia na mtoto huyo aliyefika katika ofisi za Faraja Trust Fund akiwa na bastola kwa lengo la kumuua.
Mbunge huyo aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, alisema kuwa hawana ugomvi wowote na mtoto wake na iwapo wangekuwa na ugomvi angewatumia wazee na wakubwa wa familia kusuluhisha.
“Jonas amehamia nyumbani kwangu kwa ajili ya kunisaidia kumlea baba yake ambaye ana tatizo la kupooza. Kama tungekuwa na ugomvi, tungegombana nyumbani na siyo ofisini,” alisema Lucy.
Alitoa ufafanuzi kuwa Jonas alifika ofisini kwake kwa lengo la kuchukua gari kubwa ili aende shamba, lakini wakati akitoka ofisini humo, aliinama na ghafla bastola aliyoiweka kiunoni ilidondoka na risasi kuanza kufyatuka.
Dk Nkya pia alikanusha taarifa zilizodai kuwa katika ugomvi huo alikuwa akirushiana risasi na Jonas akisema kuwa, binafsi alishika silaha mara ya mwisho mwaka 1972 alipokuwa katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Mafinga aliposhiriki zoezi la shabaha.
Alisema kuwa tukio hilo limezua taharuki kubwa kwenye familia yake na kwa viongozi wenzake wakiwemo wabunge pia kumfanya ashindwe kufanya kazi zake. Kwa upande wake Jonas Nkya, ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM, alikiri kufika ofisini kwa mama yake akiwa na bastola akieleza kuwa alikwenda kuchukua gari ili aende shamba na kwamba hakuwa na dhamira ya kufanya shambulizi lolote kwa mama yake kwani hawakuwa na ugomvi.
Alisema kuwa risasi zilifyatua baada ya kuanguka kwa bastola hiyo aliyokuwa ameiweka kiunoni na baada ya tukio hilo alikwenda katika Hospitali ya St. Mary kwa ajili kupatiwa matibabu kutokana na mshtuko alioupata baada ya risasi kufyatuka.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa uchunguzi zaidi unafanyika ili kujua kama risasi hizo zilifyatuka kwa bahati mbaya ama kwa nia ovu. “Pamoja na uchunguzi, tunamtafuta Jonas kwa ajili ya kutoa maelezo kuhusu tukio hilo,” alisema .
Toa Maoni Yako:
0 comments: