Rais Guy Scott wa Zambia akiwa na Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe
Na Nova Kambota, Dar es salaam-Tanzania
Alipochaguliwa Barack Obama kuwa rais wa taifa kubwa zaidi duniani Marekani, waafrika walifurahishwa na hali hiyo huku wakichagiza kuwa hiyo ilikuwa ni silaha dhidi ya ubaguzi kwa waafrika.
Obama ambaye ana asili ya Kenya alipongezwa hata na wahafidhina wa Afrika kwa kueleza kuwa hakuna watu wa asili wa Marekani isipokuwa jamii ya wahindi wekundu pekee, hivyo kulikuwa na kila uhalali wa mwanasiasa mwenye asili ya Afrika kuliongoza taifa hilo.
Sasa ni kama vile kibao kimegeuka, sasa ni jaribio tosha kwa wahafidhina na labda waafrika wote, nazungumzia rais mpya wa Zambia Dr Guy Lindsay Scott ambaye amechukua nafasi baada ya kifo cha rais Michael Satta.
Hili si jaribio dogo hata kidogo, hasa kwa kuzingatia kuwa bado waafrika wengi wanajitofautisha na wazungu kwa vigezo kadha wa kadha lakini uasili, utamaduni na hata rngi zao, na hapa ieleweke kuwa Zambia kiasili ni nchi ya kiafrika ambayo inapaswa kuongozwa na waafrika wenyewe, inashangaza si haba kwa mtu mwenye asili ya Uskochi kuingia Ikulu ya nchi ya Kiafrika akiwakilisha wananchi ambao hafanani nao kinasaba wala kiutamaduni.
Watu wameanza kujipa matumaini hewa kuwa ni rais wa muda, huu pengine ni uvivu wa kufikiri na labda ni kipimo cha kushindwa kutambua uafrika ni nini hasa? Ama rangi au dhana/ideology?
Kwa siasa za Afrika Guy Scott aweza kuwa rais wa kudumu, kujikita kutazama katiba ni kukimbia ukweli namna katiba za nchi zinavyovunjwa barani Afrika ili marais kadha wa kadha waendelee kubaki madarakani, ni muhimu kuzingatia kuwa uzoefu wa siasa za Afrika unaonyesha marais kama Daniel Arap Moi wa Kenya ama Gudluck Jonothan awali walionekana wa mpito lakini hali ikaja kugeuka , wakawa marais waliodumu madarakani, je hili halitatokea kwa Zambia? Tungoje tuone.
Vipi Guy Scott akiwa mwenyekiti wa umoja wa nchi za Afrika (AU), atakapowaongoza marais wenzake wa Afrika kujadili namna ya kupambana na unyonyaji wa mabeberu wa magharibi , tusemeje hapa? Hiki si kipimo kwa vyama vya upinzani barani Afrika kujitafakari namna vinavyojaza wanachama mpaka nafasi za juu za utawala kwa namna Patriotic Front (PF) cha Michael Satta kilivyoiweka Zambia kwenye kizungumkuti?
Kuna mengi ya kungoja hapa, lazima tusubiri tuone namna hali ya mambo itakavyokuwa, dunia inasubiri kuona wahafidhina mithili ya Robert Mugabe watampokea vipi Guy Scott? Watamkubali kama mwafrika mwenzao au watampinga? Wapo wanaoona rais wa kwanza wa Zambia mzee Dr Keneth Kaunda amebarikiwa kuishi muda mrefu kushuhudia nchi yake hiyo aliyoipigania mpaka kupata uhuru mnamo mwaka 1964 ikipitia wakati mgumu kama huu katika kitendawili hiki cha rais Guy Scott!
Toa Maoni Yako:
0 comments: