Mtoa mada katika semina ya wajasiriamali iliyoratibiwa na YESi Tanzania kwa udhamini wa benki ya NBC, Stephen Nyakujanga akisisitiza jambo kwa washiriki.
Na Mwandishi Wetu.
Taasisi isiyo ya kiserikali inayoshughulika na maendeleo ya wajasiamali vijana (YESi Tanzania) kwa kushirikiana na benki ya NBC wameendesha mafunzo ya elimu ya ujasiriamali kwa vijana 205 kutoka sehemu mbalimbali za mkoa wa Dar es Salaam na washiriki kutoka kibaha mkoani Pwani.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo Mwenyekiti Mtendaji wa YESi Tanzania, Denis Maira alisema mafunzo hayo yanalenga kukabiliana na changamoto ya tatizo sugu la ukosefu wa ajira kwa vijana na athari zake kiuchumi, kijamii na kiusalama.
Alisema mafunzo yatawawezesha wajasiriamali vijana kushiriki kikamilifu katika vita dhidi ya umaskini kwa kukuza shughuliza zao za kibiashara, kutengeneza ajira zaidi kwa vijana Watanzania waliohitimu masomo na walio mitaani, na hatimaye kuliletea maendeleo taifa.
Alibainisha kuwa takwimu za hali halisi ya vijana na ushiriki wao katika maendeleo ya Taifa haziridhishi. Vijana wengi, bila kujali viwango vya elimu au ujuzi, wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa ajira na njia nyingine za uhakika za kujipatia kipato na kuendesha maisha yao ya kila siku.
“Kutakuwa na takribani mada nne mahsusi zitakazotolewa na wataalamu waliobobea katika nyanja ya biashara na ujasiriamali.
Vile vile washirika watapata nafasi ya kuwasikiliza wataalamu wa fedha na mikopo kutoka benki ya NBC ambao wamekuwa mstari wa mbele kuona kuwa vijana, hasa vijana wenye mwamko wa ujasiriamali na kujitafutia ajira wanapata nafasi ya kutimiza malengo yao. Kama taasisi ya kifedha, NBC wanatimiza wajibu wao kwa vijana wa Tanzania, ni fursa ambayo nawaomba vijana waitumie.” Alisema Maira.
Toa Maoni Yako:
0 comments: