Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Mkali wa kuchekesha na sanaa za majukwaani Afrika Mashariki, Anne Kansiime anatarajiwa kutoa burudani kali hapo August 2, katika ukumbi wa Golden Tulip jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo linaloandaliwa na kituo cha Radio 5 litaambatana na burudani ya muziki kutoka ODAMA Band, pamoja na mchekeshaji Fredi Omondi kutoka Kenya na Pilipili wa Tanzania.
Akizungumzia tukio hilo Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha Radio 5, Robert Francis alisema kuwa wameamua kumualika Kansiime kwa sababu ana kipaji cha hali ya juu katika uchekeshaji na ana mashabiki wengi Tanzania.
“Kansiime ni mchekeshaji ambaye amejizolea umaarufu mkubwa Afrika Mashariki kwa uwezo wake wa kuweka utani kwenye maisha ya kawaida’ alisema Francis.
Kansiime amejipatia umaarufu kupitia mitandao ya kijamiii ambako alianza kwa kuweka vipande vya video akiigiza kama mwanamke wa kiafrika anayekutana na changamoto mbalimbali za maisha.
Mchekeshaji huyo wa kike, ambaye pia huendesha kipindi cha “Don’t Mess With Kansiime” kwenye kituo cha Citizen TV, anatajwa kuwa mwanamke mwenye kipaji cha pekee nchini Uganda na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Burudani hii ya Kansiime, ambayo itakwenda kwa jina la Cheka Kwa Nguvu, itaanza saa moja usiku na tiketi zitauzwa shilingi elfu 90,000 kwa mtu mmoja, na shilingi 700,000 kwa meza ya watu nane.
‘Kama ambavyo mwandishi wa vitabu, Maya Angelou alivyowahi kusema, “Simwamini mtu yeyote asiye cheka” tukio hili linalenga kuonesha umuhimu wa kucheka katika maisha yetu ya kila siku” alihitimisha Francis.
Toa Maoni Yako:
0 comments: