Na Mwandisi Wetu, Dar es Salaam.

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetoa tamko kuwa ugonjwa wa homa ya dengue umefikia hatua mbaya.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid alisema jana kuwa kuna hali ya hatari na maambukizi ya ugonjwa huo yanaongezeka, hivyo wananchi wanatakiwa kuwa makini.

“Kwa ufupi, mbu sasa ni hatari kuliko ilivyokuwa awali kwa sababu hawa wanaoambukiza homa ya dengue huuma wakati wa mchana, tofauti na wale wanaoambukiza malaria ambao huuma usiku na watu walikwishajua kujikinga kwa chandarua au dawa,” alisema.

Waziri Rashid aliwataka wananchi kuchukua hadhari kwa sababu ugonjwa huo hauna chanjo wala tiba... “Kila mtu anatakiwa kuchukua hatua, maji yasiruhusiwe kutuama kwa muda mrefu kwani humo ndimo mbu huzaliana kwa wingi. Kwa mfano, maji yanayotuama kwenye kofia za mabati, kwenye vifuu na kwenye madimbwi yanatakiwa yaondolewe ili kuzuia mbu hao.”

Alisema ni vyema watu waende hospitali kupima badala ya kuuchukulia kila ugonjwa kuwa ni malaria na akawataka wasipende kutumia dawa kwa matakwa yao kabla ya kuonana na daktari.

Daktari Mtafiti katika Kliniki ya Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST), Belia Klaassen alisema tangu Januari mwaka huu hadi jana, watu waliogundulika kuambukizwa dengue ni 203, kati yao 110 waliugua Aprili pekee.

Alisema tatizo hilo linaongezeka kwa kuwa kuna wagonjwa 20 wapya wanaogundulika kila siku.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: