Msemaji wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Bw. Assah Mwambene akijibu maswali mbalimbali toka kwa waandishi wa habari (hawako pichani) jana mjini Dar es salaam walioshiriki katika Mkutano wa wanahabari juu ya kuchapishwa kwa taarifa zisizo na ukweli na gazeti la Malawi lijulikanalo kama “Malawi News” kuwa wananchi wa Nchi hiyo wanaishi nchini Tanzania kwa hofu. Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Bw. Tiganya Vincent
---
Na Benedict Liwenga - MAELEZO, Dar es salaam

SERIKALI ya Tanzania imekanusha taarifa zilizochapishwa na gazeti la nchini Malawi lijulikanalo kama “Malawi News” kuwa Wamalawi waishio nchini Tanzania wamekuwa wakiogopa kutoka nje kutokana na ubaguzi wanaofanyiwa na Watanzania.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Assah Mwambene amesema kuwa taarifa hizo ni za kupotosha umma na kuleta chuki dhidi ya Tanzania na nchi jirani na hazina ukweli wowote ule.

Bw. Mwambene ameongeza kuwa hakuna raia yeyote wa kutoka Malawi aliyebakwa wala kunyanyaswa kwa namna moja ama nyingine.

“Hakuna mwananchi yoyote kutoka Malawi aliyebakwa , wala hakuna raia yoyote wa Malawi aliyepo hapa nchini anayeogopa kutoka nje kwa sababu ya ubaguzi wowote ” amesisitiza Mkurugenzi huyo.

Amesema kuwa licha Tanzania kuwakamata wahamiaji haramu 1030 kutoka Malawi, Serikali ya Tanzania iliwapa fomu ili kama walikuwa wanahitaji kuishi nchini wahalalishe uwepo wao hapa Tanzania kwa wale wote walionyesha nia ya kuendelea kuwepo hapa nchini .

Aidha wahamiaji wote haramu 1030 kutoka Malawi waliachiwa huru na wanaendelea kukamilisha taratibu za kuhalalisha uwepo nchini.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa mpaka sasa kati wahamiaji haramu 1030 hakuna aliyewekwa ndani ama kushikiliwa na vyombo vya dola kwa kosa la kuwepo kinyume.

Kufuatia taarifa hizo ,Mkurugenzi huyo amelitaka gazeti hilo kusahihisha taarifa hiyo na kuiomba radhi Tanzania kwa upotoshaji huo na kuongeza kuwa kauli hiyo ni sawa na matusi kwa Tanzania.

Aidha amesema kuwa hadi hivi sasa zaidi ya wahamiaji haramu 24,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokarisia ya Kongo (DRC) , Rwanda, Burundi , Uganda na Zambia wamerejeshwa makwao kwa kosa la kuishi Tanzania bila vibali.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: