Utangulizi:

Marais wa nchi za Rwanda, Uganda na Kenya, walikutana mwanzoni mwa mwezi uliopita, ambapo mojawapo ya maazimio ya mkutano wao, ilikuwa ni kufanya Mombasa kuwa kituo cha kukusanya ushuru, na hivyo Uganda na Rwanda waanze kusafirisha mizigo yao moja kwa moja kutoka Mombasa. (Angalia ambatisho)

Ufafanuzi:

Chama cha Umoja wa Wasafirishaji wa Malori nchini (TATOA), kinaamini hatua hiyo itadhoofisha uchumi wa nchi yetu kwa kiasi kikubwa sana.

Na kama serikali yetu ikipuuzia kujiondoa kwa wateja hawa wawili, Rwanda na Uganda, huenda nchi nyingine zaidi zikazidi kujiondoa kutumia bandari ya Dar es Salaam.

TATOA inaamini maamuzi kama haya ya nchi za wenzetu ya kurahisisha taratibu za ulipaji ushuru pamoja na kuboresha utaratibu wa bandari ni muhimu kwa bandari yetu pia.

Ripoti ya Benki ya Dunia (WB) ilidhihirisha namna ambavyo bandari ya Dar es Salaam, ufanisi ukiboreshwa, inaweza ikawa mkombozi mkubwa wa uchumi wetu.

Faida za bandari hii kwa uchumi ni mtambuka, kwa hiyo TATOA haitapenda kuona mteja yoyote akijitoa kutumia bandari yetu, au kupungua kwa biashara kwa namna yoyote ile, na hivyo itapigania kwa kuishauri serikali katika kuboresha bandari yetu.

TATOA ni mmoja wa wadau muhimu kwenye sekta hii ya bandari, kwani biashara yake ni kusafirisha mizigo inayofika bandari ya Dar es Salaam kuwafikishia walengwa, hasa nchi zisizo na bandari (land locked countries) kama Congo, Zambia, Rwanda, Malawi,Uganda, Zimbabwe na Burundi.

Hivyo kuondoka au kupungua kwa namna yoyote ile kwa matumizi ya bandari yetu, ni hofu ya TATOA itaathiri uchumi kwa kiasi kikubwa.

Ieleweke kwamba, sekta ya usafirishaji wa malori ni muhimu kwa uchumi wetu. Sekta hii inatoa zaidi ya ajira milioni moja (1) za moja kwa moja, na nyingine zaidi ya milioni tatu (3) zisizo za moja kwa moja.

Sekta ya usafiirishaji wa malori pia, ni yapili kwenye uchangiaji wa pato la taifa (GDP).

Sekta hii pia, ni mojawapo ya sekta chache nchini ambazo zinagusa nyanja tofauti za kiuchumi kama, huduma za simu za kutuma pesa, matairi, spea pamoja na mafuta, ambazo zote zinafaidika na sekta hii.

Mabenki pia yamekuwa ni mojawapo ya taasisi zinazofaidika na sekta ya usafirishaji, ukiangalia kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo, huduma inayoongoza kwenye mabenki ni Vehicle Asset Financing.

Zaidi ya hayo, TATOA pia inachangia kwa kiasi kikubwa kwenye mfuko wa barabara, ambao ndio unatumika kuboresha barabara zetu nchini, kupitia matumizi ya mafuta, ambapo malori pekee yanatumia ziadi ya lita milioni mbili na laki tisa kwa siku kati ya lita milioni tatu na nusu.

Mwisho TATOA inaamini, uboreshaji wa reli ni muhimu kwa maendeleo ya sekta ya usafirishaji nchini, kwani miundo mbinu hii miwili, reli na barabara, inafanya kazi kwa pamoja.

Wakati reli inaweza kufikisha mzigo mpaka stesheni, malori yatahitajika kufikisha mzigo sokoni, au mahala pengine mteja atakapohitaji.

Mifano hai ni nchi ya Uingereza na Afrika Kusini, ambazo zina malori mengi pamoja na kuwa zina mfumo mzuri wa reli.

Lakini kwa nchi yetu, ambayo sekta ya reli bado inaboreshwa, tunaamini malori yataendelea kuwa na umuhimu mkubwa.

TATOA inaiomba serikali, kupitia wizara ya uchukuzi kufanyia kazi kero zilizopo katika bandari ya Dar es Salaam lakini pia kufanyia kazi mapendekezo yanayotolewa na wadau wa sekta ya usafirishaji.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: