Timu ya Polisi Mbeya na Tumbaku Morogoro wakimenyana ambapo Tumbaku waliibuka kwa seti 35-17.
Wachezaji wa timu ya Uhamiaji wakiwa katika picha ya pamoja kwenye Uwanja wa Sokoine Mjini Mbeya ambapo Uhamiaji
iliibuka na ushindi wa mabao 27-19.
Mchezaji wa timu ya Netiboli ya Uhamiaji Hadija Msafiri, akifunga
goli katika mchezo wa Ligi ya Taifa uliochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine
Mjini Mbeya dhidi ya Polisi Arusha ambapo Uhamiaji iliibuka na
ushindi wa mabao 27-19.
---
Na Mwandishi Wetu.
TIMU ya mchezo wa Netiboli ya Uhamiaji ya Dar es Salaam, imeanza vizuri michuano ya Ligi ya Taifa ya mchezo huo, baada ya kuichapa Polisi Arusha katika mashindano yalianza kwene Uwanja wa Sokoine Mjini hapa.
Katika Ligi hiyo ambayo inashirikisha timu 12 kutoka katika mikoa mbalimbali ya Tanzania bara, Uhamiaji ilianza mchezo ambapo mpaka mapumziko ya kipindi cha kwanza walikuwa wanaongoza kwa mabao 12-9.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ya kushambuliana mara kwa mara ambapo wachezaji wa Uhamiaji walifika golini kwa wapinzani wao kila mara na kutumia vyema nafasi walizokuwa wanazipata ambapo mpaka mchezo unamalizika waliibuka na ushindi wa mabao 29-19.
Wachezaji wa Uhamiaji waliopeleka kilio kwa wapinzani wao walikuwa Neema Masawe ambaye alifunga mabao 16 pamoja na Khadija Msafiri aliyefunga mabao 11.
Wafungaji wa upande wa Polisi Arusha walikuwa ni Arafa Yahaya ambaye alifunga mabao 15 na Agnes Okasa ambaye alifunga mabao 4.
Mchezo mwingine ulikuwa kati ya Polisi Mbeya dhidi ya Tumbaku ya Morogoro ambapo Tumbakiu ilifanikiwa kushinda kwa mabao 35-17.
Mpaka mapumziko Tumbaku walikuwa wakiongoza kwa mabao 16-6 ambapo wafungaji wake walikuwa Glady Joseph ambaye alifunga mabao 28 na Fanuna Yasin alifunga mabao 6 wakati kwa upande wa Polisi wafungaji wake walikua Magret Mwakifuma aliyefunga mabao 12 na Nyirabu Maximilian aliyefunga mabao 6.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mechi hizo, Mwenyekiti wa Chama Cha Mchezo huo Mkoa wa Mbeya, Marry Mng’ong’o alisema kuwa mashindano hayo yanatarajiwa kufunguliwa rasmi kesho katika Uwanja huo kutokana na ratiba za Ligi Kuu bara kuingiliana ambapo ilianza leo.
Alisema kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi rasmi wa Ligi hiyo anatarajiwa kuwa Abbas Kandoro, ambaye ataambatana na viongozi mbalimbali wa mkoa.
Alisema kuwa awali timu 20 zilitarajiwa kushiriki kwenye mashindano hayo lakini zimejitokeza 12 pekee kutokana na zingine kukumbwa na ukata wa fedha hivyo wakashindwa kusafirisha wachezaji.
Alizitaja timu ambazo zinashiriki kwenye Ligi ya Taifa ambayo itamalizika Septemba 7 mwaka huu kuwa ni pamoja na Filbert Bayi, Polisi Mbeya, Polisi Mwanza, Tumbaku Morogoro, Uhamiaji Dar Es Salaam, Magereza Morogoro, JKT Mbweni, Polisi Arusha, Jeshi Star, CMTU na JKT Ruvu
Alisema kuwa washindi watatu wa kwanza wanatarajiwa kushiriki katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika ambayo yatafanyika mwakani.
“Tunashukuru tumeanza salama japokuwa kuna baadhi ya timu zimeshindwa kuja kushiriki na lakini nyingi zimejitokeza ambapo pia mashindano rasmi yatafunguliwa kesho na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro” alisema.
Toa Maoni Yako:
0 comments: