Na Kajunason Blog team, Dar es Salaam

Tanzania imepata tuzo ya heshima ya ugunduzi wa mfumo bora wa utatuzi wa vikwazo vya kibiashara katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC).

Tanzania imepata tuzo hiyo kupitia Chama Cha Wafanyabiashara wa Viwanda na Kilimo (TCCIA), baada ya kushika nafasi ya pili kati ya tano bora duniani zilizoshiriki ubunifu wa mifumo ya kuondoa vikwazo vya biashara.

Mshindi wa kwanza ni Uingereza na vyama zaidi ya 10,000 kutoka nchi mbalimbali vilishiriki mashindano hayo.

Akizungumza Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa TCCIA, Daniel Machemba, alisema mashindano hayo yaliandaliwa na Shirikisho la Vyama vya Kimataifa vya Wafanyabiashara (ICC) huko Doha, Qatar wiki iliyopita.

Alisema katika mashindano hayo, Tanzania ilishindanisha mfumo wake mpya wa wafanyabiashara kutuma ujumbe mfupi wa simu za mkononi kwa TCCIA muda wowote wanapokumbana na vikwazo.

“Mfumo huo umeweza kuondoa vikwazo vya muda mrefu vya ucheleweshaji wa taarifa, hasa maeneo ya mipakani, ambapo mizigo ilikuwa inacheleweshwa bila sababu za msingi katika mipaka ya nchi wanachama wa Afrika Mashariki.

“Tulichokifanya TCCIA kwa kushirikiana na Trade Mark East Africa ni kuweka mfumo wa urahisi wa kuripoti tukio, mfumo huo maalumu unaowawezesha wanachama wetu hutuma ujumbe wa simu ya mkononi kwa namba 15539 na tatizo hupatiwa ufumbuzi wa haraka,” alisema Machemba.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: