Rais wa Taasisi ya Wahandisi Tanzania, Eng. Dk. Malima Bundara akitoa tamko la taasisi yake leo jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani).
---
1. UTANGULIZI (ANGALIZO)
Kabla ya kutoa tamko lake, Taasisi ya Wahandisi Tanzania inatanguliza ufafanuzi ufuatao kwa ajili ya kuongeza uelewa na kuzuia upotoshaji wa habari na/au uchanganyaji wa majukumu ya taasisi mbalimbali katika tasnia ya uhandisi na ukandarasi nchini Tanzania.
Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) ni taasisi ya serikali chini ya Wizara ya Ujenzi iliyoundwa kwa lengo la kusajili na kusimamia kazi za wahandisi nchini Tanzania. Lengo la serikali ni kulinda maslahi ya wananchi na watumiaji wa huduma za kihandisi.
Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) ni taasisi ya serikali chini ya Wizara ya Ujenzi iliyoundwa kwa lengo la kusajili na kusimamia kazi za makandarasi nchini Tanzania. Lengo la serikali ni kulinda maslahi ya wananchi na watumiaji wa huduma za makandarasi.
Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET) ni jumuiya binafsi isiyokuwa ya kibiashara iliyoundwa na wahandisi wenyewe kwa lengo la kuhamasisha, kujenga na kuendeleza taaluma ya uhandisi na stadi za wahandisi nchini Tanzania na kwingineko.
2. KUPOROMOKA KWA JENGO
Tarehe 29 Machi, 2013, jengo lenye ghorofa 16 lililokuwa linajengwa kwenye mtaa wa Indira Gandhi jijini Dar es Salaam liliporomoka na kuua watu 36 na kujeruhi watu wengine kadhaa. Tukio hili siyo la kwanza kutokea jijini Dar es Salaam katika kipindi kisichozidi miaka 10, kwani mwaka 2006 jengo lililokuwa linajengwa Chang’ombe liliporomoka na mwaka 2009 jengo la ghorofa 10 lililokuwa linajengwa eneo la mtendeni jijini vilevile liliporomoka. Katika matukio mawili ya mwanzo serikali iliunda Tume kuchunguza vyanzo vya ajali hizo.
3. TAMKO LA TAASISI
Taasisi ya Wahandisi Tanzania kwa niaba ya Wahandisi wote nchini na kwengineko inatamka kama ifuatavyo:
(a) Kuporomoka kwa jengo lililokuwa linaendelea kujengwa jijini Dar es Salaam kumepokelewa kwa mshangao na huzuni kubwa. Wahandisi wanatoa pole kwa serikali kupitia kwa Mkuu wa Mkoa. Aidha wahandisi wanatoa pole kwa wafiwa na watanzania wote kwa ujumla kutokana na msiba huu mkubwa. Vilevile taasisi inawashukuru wananchi na waandishi wa habari kwa mchango wao katika shughuli za uokoaji kwenye ajali hii.
(b) Taasisi inaipongeza serikali kwa juhudi zake za kupanga na kusimamia uokoaji katika ajali hiyo. Aidha taasisi inaipongeza serikali kwa kuziamini na kuzikabidhi taasisi zake za kitaalamu (yaani ERB na CRB) jukumu la kuunda jopo la kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha kuporomoka kwa jengo hilo. Ni matumaini ya Taasisi ya Wahandisi Tanzania kwamba jopo litakaloundwa litajumuisha wataalamu makini watakaofanya uchunguzi wa weledi na kina na kuzingatia maslahi ya Taifa letu bila kumwonea au kumpendelea mtu au taasisi.
(c) Kwa kuwa Taasisi ya Wahandisi Tanzania ni msemaji wa wahandisi kama wanataaluma ndani na nje ya serikali, Taasisi ya Wahandisi Tanzania inawajibika kusaidiana na serikali katika kupata ufumbuzi wa kudumu na kuondokana na kuporomoka kwa majengo na majanga mengine katika sekta ya ujenzi. Aidha umma wa watanzania unatagemea kupata tamko la wahandisi kuhusu suala hili.
(d) Ingawa kila mtu anataka aelezwe chanzo cha kuporomoka kwa jengo hilo sasa hivi, Taasisi inasema kwamba kufanya hivyo haraka haraka bila kupata taarifa za kutosha ni kuendelea kushughulikia matokeo badala ya kupata kiini kinacholeta matokeo hayo. Kutokana na mtazamo huo, Taasisi imeunda Kamati ya Wataalamu saba kusaidiana na ile Kamati ya Serikali kuchunguza chanzo cha kuporomoka kwa jengo kwa namna tofauti. Badala ya kujikita kwenye uchunguzi wa tukio lenyewe, Kamati ya Taasisi itachunguza sheria na mfumo wa sekta ya ujenzi wa majumba kwa jumla ili kubaini kiini cha matokeo yatakayopatikana katika uchunguzi wa tukio. Kamati ya Taasisi itakusanya na kuchambua taarifa kuhusu;
i) Sheria na taasisi zenye majukumu ya kisheria kwenye ujenzi wa majumba. Orodha ya Taasisi hizi ni ndefu ikiwa ni pamoja na; Halmashauri miji/majiji, OSHA, CRB, AQRB, NCC, TBA, NHC, NEMC, PPRA, Agensi ya Zimamoto na uokoaji na Wizara ya Ardhi.
ii) Viwango na kanuni kwenye sekta ya ujenzi wa majumba hapa nchini.
iii) Taratibu za kazi katika sekta ya ujenzi kuanzia pale mtu anapopata idhini ya kujenga nyumba mpaka nyumba inapokuwa tayari kwa watu kuishi.
iv) Masuala ya usanifu na usimamizi wa ujenzi wa nyumba, wahusika wake na mgawanyo wa kazi.
v) Ripoti za uchunguzi wa matukio kama haya na hatua iliyokwishafikiwa katika utekelezaji wa mapendekezo husika.
vi) KUPOROMOKA KWA JENGO NA UHUSIANO WAKE NA MAMBO YALIYOTAJWA HAPO JUU.
4. MWISHO
(a) Kamati ya Taasisi itaongozwa na Eng. Ladislaus Salema ambaye ni Rais mstaafu wa Taasisi. Kamati imepewa siku 14 kumaliza kazi yake.
(b) Taasisi inawaomba Watanzania wote siyo kuwa na subira, bali pia kushirikiana na Kamati zetu ili kupata kiini na dawa ya maradhi yanayoendelea kujitokeza kwenye sekta yetu ya ujenzi wa majumba.
Mungu ibariki Tanzania
Mungu ibariki Afrika
Imetolewa na
Eng. Dk. Malima M.P. Bundara
Rais wa Taasisi
03 Aprili, 2013
Toa Maoni Yako:
0 comments: