Juu
na chini anaonekana Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na
viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini ya Kikristo Ikulu jijini Dar es
salaam leo ambapo amekuwa na mazungumzo nao ikiwa ni mojawapo ya
jitihada za Rais
Kikwete kutafuta muafaka na kutafuta utatuzi wa hali ya sintofahamu ambayo inanyemelea nchi yetu katika kipindi hiki.
Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika mazungumzo na viongozi
wa madhehebu mbalimbali ya dini ya Kikristo Ikulu jijini Dar es salaam
leo
Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete katika picha ya pamoja na viongozi
wa madhehebu mbalimbali ya dini ya Kikristo Ikulu jijini Dar es salaam
leo. Kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano) Mhe Steven
Wassira.
---
Viongozi wa dini wamewataka waumini kote nchini kulinda amani na
umoja uliopo ili nchi isije ikaingia kwenye mgawanyiko wa kidini na
kuleta machafuko hapa Tanzania.
Wito huo umetolewa na viongozi wa dini leo Ikulu ya Dar-Es-Salaam mara
baada ya kikao cha pamoja baina ya viongozi wa dini na Rais Jakaya
Kikwete.
Viongozi hao wa dini wamefika leo wakiongozwa na Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).
Viongozi wengine wametokea Baraza la Kikristo Tanzania (CCT) Seventh Day Advertist (SDA) na Baraza la Pentekoste Tanzania (PCT).
Mkutano huo umeanza kwa Askofu Ngalalekumtwa kusoma tamko lao la pamoja
kwa Rais Kikwete ambalo ndilo limetoa muongozo wa mazungumzo hayo ya leo
ambayo yamehusu Amani na Usalama wa Taifa na migogoro ya kidini ndani
ya jamii.
Mkutano wa viongozi wa dini ya Kikristo Tanzania ni mojawapo ya jitihada za Rais Kikwete kutafuta muafaka na
kutafuta utatuzi wa hali ya sintofahamu ambayo inanyemelea nchi yetu katika kipindi hiki.
“Nataka tuzungumze ni namna gani tunaweza kutoka kwenye hali hii na
tunakwendaje mbele zaidi na kuhakikisha nchi yetu bado inakua ya amani
na umoja kama ilivyozoeleka”
Rais amesema na kutoa nafasi kwa viongozi wa dini kutoa maoni yao.
Viongozi hao wa dini wamemueleza Rais Kikwete kuwa wanaunga mkono
jitihada zake za kutafuta amani na kwa pamoja wamekubaliana uandaliwe
mkutano wa pamoja baina ya viongozi wa dini zote ambapo masuala ya amani
na umoja wa nchi utajadiliwa kwa kirefu.
Katika kikao cha leo pande zote zimekubaliana kuwa kuna changamoto zilizoko sasa zinahitaji kutatuliwa haraka iwezekanavyo ili kuepusha nchi kutumbukia katika mgogoro mkubwa zaidi,
na pia kukubaliana kuwa pande zote, kwa maana ya serikali na taasisi za
dini, zinawajibu mkubwa wa kuhakikisha amani inadumu.
Kabla ya kikao cha leo , Rais amewahi kukutana na viongozi wa dini ya kiislamu na kikristo mmoja mmoja ambapo alikua
akitafuta maoni na ushauri wa pande zote kabla ya pande zote hazijakaa pamoja na kuwa na msimamo wa pamoja.
Kikao cha leo kimehitimisha jitihada hizo na kinachofuata ni mkutano mmoja ambapo Rais Kikwete atakutana na viongozi wa dini zote kwa pamoja hivi karibuni.
Toa Maoni Yako:
0 comments: