Na John Kitime

Imani ya uchawi ni utamaduni ambao umekuweko katika jamii zote za binaadamu kwa maelfu ya miaka. Historia na maandiko ya dini mbalimbali yanatukumbusha hilo na kulilaani. Huwa inategemewa kuwa kadri maendeleo na elimu yanavyoongezeka ndio imani hiyo inavyopungua na kupotea, lakini ni wazi safari bado ni ndefu kwani ukipita katika mitaa mingi utaona vibao vikiashiria waganga wanaoweza kutibu magonjwa mbalimbali, na hata kutangaza ‘kusafisha nyota’, ‘kuondoa majini’ na kadhalika.

Tasnia ya muziki kwa kuwa ni sehemu ya jamii, haijakwepa kuguswa na tatizo hilo. Kutokana na mimi mwenyewe kufanya kazi katika bendi mbalimbali niliona na kusikia vituko vingi vilivyohusishwa na imani ya uchawi. 

Mara ya kwanza kuanza kuona vitimbi hivi ‘live’ ni nilipojiunga na bendi moja ambayo ilikuja kuwa maarufu sana wakati wake. Kwa mara ya kwanza nilishuhudia kiongozi wa bendi yangu akiwa na katibu wake wakiwa wanafukiza kwenye radio majani fulani wakati kipindi cha Misakato kikiwa hewani. 

Misakato kilikuwa ni kipindi kilichokuwa hewani kila Jumanne saa tatu na robo asubuhi, katika redio ya RTD, kikiporomosha nyimbo mpya zilizorekodiwa na pia kutoa maelezo kuhusu wanamuziki walioshiriki. Siku hiyo vibao ambavyo tulikuwa tumerekodi vilikuwa vikirushwa hewani kwa mara ya kwanza, ndipo viongozi wangu hawa nikawakuta wakiwa katika shughuli ya kufukiza radio, kwa imani kuwa kwa kufanya hivyo, vibao hivyo vitatikisa wasikilizaji wake. 

Baada ya hapo vituko vingi viliendelea hatimae tulimzoea kiongozi wa bendi yetu kuwa ni mshirikina. Kuna wakati aliletwa mganga ambaye alidaiwa aliwahi kuifanya timu moja maarufu ya soka, ishinde kikombe na kuwa bingwa wa Taifa na alichukuliwa kwa mkataba na bendi na kazi yake ikawa ni kukaa mlangoni akijifanya ni muuza machungwa. 

Yeye alidai kila anapomenya chungwa kwa kuunganisha maganda basi na wateja nao wataingia katika ukumbi kwa kuunganika, huyu alikaa kiasi katika bendi na tukaweza hata kusafiri nae kwenda mikoani. 

Harakati za bendi kutafuta umaarufu kwa uchawi zilipeleka mpaka bendi ikasafiri hadi kwenda Mpanda, ambako viongozi wa bendi walikwenda kwa mganga na kufanya mambo yao yalioyohusisha na hata kumchinja mbuzi ambaye nadhani masharti yalikuwa ni sisi wanamuziki wote tule kipande cha mbuzi yule wa kafala. Sijajua hatima ya nyama ya mbuzi yule maana wanamuziki walifanya mgomo wa kumla yule mbuzi. 

Kiongozi wa bendi katika safari hiyo, alichanjwa shingo yote na akawa na mikrofon ambayo wengine wote tulikatazwa kuitumian na sikuona mtu akiigusa mpaka nilipoacha bendi. 

Ushirikina una matatizo ya kufanya watu wasiaminiane hata kwenye bendi yenyewe, haikuchukua muda mrefu bendi ilipoanza kupoteza umaarufu, Kiongozi wa bendi akaaitisha mkutano na kutuambia kuwa kuanguka kwa bendi kunatokana na mmoja wetu kuiloga bendi, hapo ikatolewa tishio kuwa mtuhumiwa asipojitaja mwenyewe na kuomba msamaha mganga atamfanya awe kichaa. Jambo ambalo liliungwa mkono na wote kuwa kama ni kweli kuna mtu namna hiyo basi apate uchizi. Hakuna aliyekumbwa na tatizo hilo mpaka leo.

Miezi michache baadae, wanamuziki wawili walioamua kuacha bendi walirudisha uniform zao shati zikiwa zimechanywa kwenye kwapa na suruali kuchanywa kwenye maungio ya miguu kwa imani kuwa hizo ndizo sehemu zenye jasho kwa hiyo zingeweza kutumiwa na bendi kiuchawi kuwaharibia maisha.

Katika mizunguko kwenye bendi mbalimbali, nilikuwa katika bendi ambapo siku kukiwa na mpambano wa kupiga bendi zaidi ya moja katika ukumbi mmoja, basi hapo mganga maalumu lazima atafutwe ili kuilinda bendi isimalizwe na wapinzani. Ilikuwa inaaminika kuwa katika mpambano wa bendi, uchawi hutumika kuimaliza bendi ambayo itakuwa haina kinga. Kwa siku hiyo ndani ya spika kuliwekwa tunguli na hirizi mbalimbali tayari kwa mpambano.

Kwa ukweli kabisa hata wanamuziki kutembeleana zamni ilikuwa ni vigumu, kwani ukionekana mwanamuziki wa bendi nyingine katika ukumbi, basi bendi iliyo jukwaani haina raha, anaweza hata akatumwa mtu kufuatilia kila utakachofanya. Na ilikuwa vigumu kuruhusiwa kugusa vyombo vya bendi nyingine kwa wasiwasi wa kuwa unaweza ukaloga kile chombo.

Kulikuwa na hadithi nyingi kuhusu ni kiasi gani bendi ziliweza kufanya ili kupata wateja. Kuna bendi ambayo ilisifika kuwa kila wakimaliza kupiga walipita katika kumbi na kuokota vizibo vya chupa, mifupa, na hata kupata maji toka chooni kwenda kuloga ili wale walioingia wasiingie bendi yoyote kasoro yao. Bendi nyingine zilidaiwa kuwa ziliweka mkataba ambapo zililazimika kutoa kafala ya mtu kila mwaka, hivyo viongozi wa bendi kufiwa na watoto, na hata wanamuziki wageni katika bendi hizo kukutwa na mauti ambayo, kwa chinichini yalidaiwa ni katika kutoa kafala.

Bendi mbili ambazo zilikuwa na upinzani mkubwa katika jiji la Dar es Salaam zilidaiwa hata kutaka kuweka uchawi katika chanzo cha maji Dar es Salaam , na kujikuta wakitaka kuumbuana hadharani kuhusu hilo.

Kama nilivyosema imani ya uchawi huleta kutokuaminiana na hata madhara makubwa ya kutuhumiana mambo ambayo mara nyingi hayana ukweli wowote. Kuna mwanamuziki niliyejaribu kumshawishi aingie katika bendi niliyokuwa nikipigia , alikataa katakata kwa kuwa alidai mmoja wa wanamuziki katika bendi ni mchawi. 

Mwanamuziki mmoja aliwahi kuhadithia jinsi alivyopita uchochoro wa nyumba ya mwanamuziki mwenzake akashangaa kusikia jina lake likitajwa na mwenzie aliyekuwa chumbani kwake na kusema,’ Nyota ya …….izimike kama kaa hili’, akadai alichungulia katika ufa na akakuta mwenzie anatumbukiza kaa la moto kwenye maji. Ugonjwa wa ukimwi ulipoanza kuuwa wanamuziki kwa mara ya kwanza mara nyingi ulihusishwa na uchawi. 

Rafiki yangu mmoja nilipomtembelea wakati akiwa hoi kitandani akanambia,’Nikupe siri? Mi ntakufa lakini nauawa na wanamuziki wenzangu kwenye bendi. Nimepata mganga kanitajia na majina kabisa’. Miezi michache baadae mwanamuziki huyu kabla hajafariki alinambia,’Mjomba sijalogwa wala nini, udude huu, unaniua udude’. Alifariki siku chache baada ya kunambia haya. Mungu amlaze Pema peponi Mjomba.

Kitu ambacho kimenishangaza karibuni tuhuma kuwa kuna wanamuziki wa kizazi kipya wanaendeleza imani hii ya ushirikina. Producer maarufu amejitokeza na kuwakanya wasifanye mambo hayo kwenye studio yake. Na siku chache baada ya hapo tena mwanamuziki mwingine wa muziki huo kawataja ambao aliwaita wabaya wake wanaomloga.!!!!!!! Nikaona loh kumbe shughuli bado inaendelea...  

UZOEFU WANGU NI KUWA WANAMUZIKI WOTE WALIOAMINI NA KUSHIRIKI KATIKA USHIRIKINA ILI KUJIPATIA UMAARUFU WALIISHIA KUWA WANAMUZIKI WA KAWAIDA TU NA HATA KUPOTEA KABISA TOKA KWENYE ULIMWENGU HUO, UKICHUNGUZA UMAARUFU WAO HAUKUTOKANA NA USHIRIKINA LAKINI ULITOKANA NA UBORA WA KAZI ZAO, JAPO KUNA WAKATI HATA WAO WALIONA WAMEKUWA MAARUFU KWA AJILI YA USHIRIKINA. KAMA UNA KIPAJI,UNAFANYA MAZOEZI INAVYOTAKIWA, UNAFUATA TARATIBU ZA UENDELEZAJI NA UTAWALA WA KAZI ZAKO INAVYOTAKIWA HUO NDIO UCHAWI MKUBWA WA KUFANIKISHA KAZI ZAKO...
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: