VITUO mbalimbali vya kuuzia mafuta nchini, kuanzia jana mpaka leo viligoma kutoa huduma hiyo kutokana na serikali kutangaza kushusha bei ya nishati ya mafuta.


Habari na Matukio wameweza kutembelea vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam na kushuhudia watumiaji wakipata usumbufu mkubwa kutokana na kutokuwapo kwa huduma hiyo. 

Katika kituo cha Kobil kilichopo Ilala, magari mengi yalionekana yakitoka kituoni hapo bila kupata huduma waliyohitaji. Mhudumu wa kike aliyekuwepo katika kituo hicho alikuwa akitoa taarifa kuwa mafuta yamekwisha.Hali kadhalika katika kituo kingine cha Oryx kilichopo eneo la Fire, nacho kilikuwa hakitoi huduma hiyo.

Msimamizi wa kituo hicho, Abdalah Amary, aliiambia Tanzania Daima kuwa wameishiwa mafuta kuanzia juzi jioni na kwamba maelezo zaidi kuhusu kuwepo kwa mafuta katika kituo hicho yatatolewa na makao yake makuu yaliyopo Kurasini.

Mwanchi akiwa amebeba dumu lenye mafuta kwa ajili ya kuweka akiba.

Katika kituo cha Gapco kilichopo Kariakoo, muda wa saa tano asubuhi wauzaji walisema wamebakiza akiba kidogo ya mafuta.

“Ni kweli leo kuna tatizo la mafuta katika vituo vingi. Sisi mafuta tuliyonayo ni kidogo. Baada ya muda mchache kutoka sasa yatakwisha, na makao makuu ya Gapco wamegoma kuuza baada ya mafuta haya kwisha,” alisema mmoja wa wahudumu ambaye hakutaka kutaja jina lake.

Hata hivyo, vituo vya Big Bon, Kariakoo, BP vilivyopo Fire, Kisutu, Jamhuri na Mkwepu, Oil Com vilivyopo katika maeneo ya Posta na Stesheni vilikuwa vikiendelea kutoa huduma hiyo.

Wauzaji wa mafuta katika maeneo mbalimbali walisema wamepunguza bei kama serikali ilivyoagiza, lakini wanauza mafuta hayo kwa hasara, kwa kuwa wanaogopa kutozwa faini.

Wakati huohuo, wafanyabiashara wa mafuta mkoani Rukwa wamegoma kutoa huduma hiyo.

Habari na Matukio ilishuhudia vituo hivyo vikiwa wazi, lakini vikishindwa kutoa huduma hiyo kwa visingizio mbalimbali, ikiwamo kuharibika pampu za kusukuma mafuta, vituo kukosa huduma ya umeme na vituo vingine kuelezwa kutokuwa na mafuta kwa takriban wiki moja sasa.

Vituo vyote vya mjini Sumbawanga, Nkasi na Mpanda kwa siku nzima ya jana havikutoa huduma hiyo, hali ambayo imesababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa bidhaa hiyo.

Kutokana na hali hiyo baadhi ya watu binafsi ‘walanguzi’ wanaodaiwa kuhifadhi mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa wameanza kuuza kwa kulangua, ambapo mafuta ya taa yanauzwa kati ya sh 2,700 hadi sh 3,000, petroli inauzwa sh 5,000 na sh 6,000 wakati dizeli nayo ikiuzwa bei kama hiyo kwa lita.

Uchunguzi zaidi uliofanywa na blog hii umebaini sababu zinazotolewa na watumishi wa vituo hivyo si za kweli, bali wamiliki wa vituo hivyo wamegoma kutoa huduma hiyo kwa kuwa hawaafikiani na bei mpya iliyotangazwa na serikali.

Walisema bei hizo hazina manufaa kwao, hivyo wameamua kuendesha mgomo baridi hadi pale mamlaka inayohusika itakaporekebisha tena bei hizo.
Juzi Mkurugenzi wa EWURA, Haruna Masebu, alitangaza kushuka kwa bei ya nishati ya mafuta, ambapo petroli itapungua kwa sh 202, dizeli sh 173 na mafuta ya taa sh 181.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: