WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii imetahadharisha kuhusu kusambazwa kwa zaidi ya kilo 1,000 za samaki wenye sumu sehemu mbalimbali za nchi na kuwataka wananchi washiriki msako iliouanzisha kuwatafuta.

Taarifa ya wizara hiyo iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam imeeleza kuwa samaki hao ni sehemu ya kilo 124,992 zilizoingizwa nchini kutoka Japan.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tayari Serikali imeanza msako mkali kuwatafuta samaki hao, lakini ikaonyesha wasiwasi kwamba juhudi hizo huenda zisizae matunda kwa kuwa sehemu ya shehena hiyo imeshaingia sokoni.

Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Blandina Nyoni (pichani) alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa samaki hao tayari wameingizwa katika masoko ya Dar es Salaam na Morogoro.

“Wananchi wanaombwa kutoa ushirikiano kwa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Idara za Afya za Mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro na Jeshi la Polisi, ili samaki waliobaki wapatikane,” alisema Nyoni.

Nyoni aliutahadharisha umma kuwa athari za sumu inayohofiwa kuwapo kwenye samaki hao ni ya mionzi ya nyuklia ambayo kimsingi hujitokeza taratibu katika mwili wa binadamu.“Samaki wenye uzito wa tani 1.319 wanafuatiliwa na kumbukumbu zinaonesha kuwa wamesambazwa kupitia soko la Feri, Dar es Salaam, Morogoro Mjini na Kilombero,”alisema

Katika kuhaha ili kuokoa maisha ya Watanzania, Nyoni anasema: “Wizara inaviomba vyombo vya habari, viiarifu na kuielimisha jamii juu ya kuwepo kwa samaki hao wanaochunguzwa kwa kuhisiwa kuwa na madhara.”

Pamoja na juhudi hizo, alifafanua “kazi hii ya ufuatiliaji na uchunguzi, inaendelea usiku na mchana hadi samaki hao watakapopatikana.”

Samaki hao wametoka wapi?

Nyoni alisema samaki hao aina ya “Mackerel” waliingizwa nchini na kampuni ya Alphakrust Ltd ya Dar es Salaam kutoka kampuni ya Kaneyama Corporation ya Chiba, Japan. “Samaki hao walisafirishwa kupitia Bandari ya Yokohama, Japan na kuingia nchini kupitia Bandari ya Dar es Salaam,” alisema Nyoni akidai kuwa taarifa zinaonyesha waliingizwa baada ya kukidhi masharti ya kisheria na taratibu zilizowekwa
“Kwa mujibu wa nyaraka za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mzigo huo ulifika Bandari ya Dar es Salaam tarehe 18 Julai, 2011,” alisema Nyoni na kuongeza:

“Wizara ilipata taarifa siku ya Jumamosi kwamba samaki hao wanahisiwa kuchafuliwa na mionzi ya nyuklia iliyotokea huko Japan, mwezi Machi, 2011.”

Nyoni alisema hadi kufikia juzi asubuhi, kiasi cha samaki wenye uzito wa tani 123.673, kati ya tani 124.992 walioingizwa nchini, walipatikana na kuzuiliwa katika maghala ya kampuni ya Alphakrust Ltd.Kufuatia taarifa hiyo, Nyoni alisema wizara yake  iliiagiza TFDA kuchukua hatua za haraka za kuzuia usambazaji wa samaki hao hadi uchunguzi utakapokamilika.

Alisema samaki hao walisindikwa tangu Desemba mwaka jana na muda wake wa mwisho kutumika ni Juni, 2012.Alisema samaki hao waliruhusiwa kuingizwa nchini kwa kibali cha TFDA namba TFDA11/F/IPER/0896, cha Julai 11 2011.

Wauzaji wanasemaje?
Baadhi ya wauzaji wa samaki wa Soko Kuu la Feri, walisema hatua ya Serikali ya kusitisha usambazaji wa samaki hao, imechelewa kwani tayari sehemu kubwa ya mzigo ilishauzwa.

“Hawa Kamongo ni Samaki adimu sana, Ijumaa tulipopata taarifa kuwa mzigo umeshuka, haraka tulifika kule Jet ambapo ndiyo kuna hilo ghala la Wajapani kwa ajili ya kununua,” alisema Juma Rashid kuongeza:

“Tulifika pale na watu wa vipimo wakaingia na DFP yao  (namba za ushajili za gari), wakafungua kontena wakapima halafu wakatuambia mzigo uko safi. Tukachukua kila mtu kwa kiasi alichotaka, mpaka Jumapili wanakuja kukamata mimi nilishamaliza mzigo wangu wa boksi tano wote.”

Kwa mujibu wa wachuzi hao, boksi moja la samaki hao ambalo lina uzito wa kilo15, linauzwa Sh51,000 kwa bei ya jumla.Juma Amiri (45), alisema shughuli ya kukamata samaki hao ikifanyika Jumapili, alikuwa amebaki na boksi moja tu.Mwenyekiti wa Chama cha Madalali wa Samaki sokoni hapo, Abdala Mjanga, alisema hana taarifa rasmi za suala hilo, lakini alishuhudia kamata kamata hiyo iliyokuwa ikiendeshwa sokoni hapo.

Kauli ya TFDA
Kaimu Mkurugenzi wa TFDA, Hiiti Silo alisema taarifa hiyo ya wizara ni msimamo wa Serikali na idara zake zote ikiwamo TFDA

"...Lakini TFDA tunafanya uchunguzi kwa kasi ili tuimalize kazi hiyo mapema kuokoa maisha ya watu," alisema.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: