Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) katika Mkoa wa RUVUMA Bw BENEDICT NGWENYA ambaye pia ni Diwani wa Chama Cha Mapinduzi katika kata ya MPEPAI wilayani MBINGA amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 36 Jela baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa shilingi Milioni 80 Mali ya kampuni ya DAE Limited ya MBINGA.

Mwenyekiti huyo ambaye pia alikuwa katibu wa Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi Captain JOHN KOMBA, amepatikana na hatia katika makosa 12 ya wizi wa kuaminiwa kati ya makosa yote 13 aliyoshitakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa RUVUMA.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama ya Mkoa wa Ruvuma Mheshimiwa BAPTIST MHELELA amesema BENEDICT NGWENYA atatumikia kifungo cha miaka mitatu kwa kila kosa, na adhabu zitakwenda moja baada ya nyingine hali itakayomlazimu kukaa miaka yote 36 jela.

Awali mwanasheria wa serikali mkoani Ruvuma Mwegole Shabani alidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa Ngwenya alitenda makosa hayo kwa nyakati tofauti mwaka 2008 akiwa anafanya kazi kama mhasibu katika kampuni ya DAE LTD ya MBINGA.

Mwigole Shaban ameongeza kuwa mshitakiwa alizichukua fedha hizo kwa lengo la kwenda kugawa kwenya mitambo inayokoboa kahawa mbichi ambapo hata hivyo hakuzifikisha fedha hizo sehemu husika.
Alisema baada ya kutenda kosa hilo aliacha kazi bila kukabidhi ofisi kwa mwajiri wake jambo ambalo lilipelekea mwajiri huyo kumtilia mashaka na kumtaka mkaguzi wa mahesabu wa ndani kufanya ukaguzi wa hesabu za ndani na ndipo alipobaini upotevu wa fedha hizo.

Hata hivyo Hakimu BAPTIST MHELELA amesema rufaa ipo wazi kwa Bw BENEDICT NGWENYA na anaweza kukata Rufaa hiyo ndani ya siku 45.

Mara baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, hali ya huzuni imetawala katika viwanja vya mahakama ya Mkoa Mjini Hapa, hasa kwa vijana wa Chama cha Mapinduzi CCM ambako Bwana NGWENYA alikua mwenyekiti wao lakini ndio hivyo sheria imebaki kuwa msumeno unaokata pande zote.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: