Na Mwandishi wa Jeshi la Polisi -Zanzibar

Makachero wa Jeshi la Polisi Zanzibar wamefanikiwa kukamata kiasi kikubwa cha fedha bandia katika masanduku na kubaini aina nne za utapeli unaofanywa na wajanja wachache kwa kuwaibia wananchi wakiwemo viongozi wenye nyadhifa kubwa Serikalini.

Afisa Uhusiano wa Jeshi la Polisi Zanzibar Inspekta Mohammed Mhina, amesema kuwa katika wizi huo, matapeli hao wamekuwa wakitumia mabunda ya fedha bandia kabla ya kuwapigia simu walengwa kuwahadaa wakijifanya watawapatia utajiri mkubwa.

Akizungumzia utapeli huo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mjini magharibi Zanzibar ACP Aziz Juma Mohammed, amesema kuwa Matapeli hao wamekuwa wakiwapigia simu walengwa wenye tamaa ya utajiri huku wakihusisha mambo ya mizimu.

Kamanda Aziz amesema kuwa Matapeli hao pia huwahadaa watu kwa kuwauzia chupa za maji ya viungo huku wakijifanya kuwa ni madawa ya gharama kubwa kwa ajili ya kusaidia kuhifadhia vyakula zinavyosindikwa ama kusafirishwa nje ya nchi kwa kuuzwa.

Amesema ili kufaniwa utapeli wao, wahalifu hao pia huwaambia watu kuwa wana uwezo wa kubadili karatasi chafu na kuwa fedha za Kigeni jambo ambalo amesema limechangia watu wengi kuibiwa fedha zao.

Kamanda huyo wa mkoa wa Mjini Magharibi, amesema kuwa matapeli hao wamewaibia watu wengi na wanaendelea kufanya hivyo kwa wengine na hivyo amewataka wananchi kujihadhari sana na watu kama hao na kwamba wasikubali kupeana ahadi itakayohusu malipo ya fedha pasipo haja ya kufanya hivyo.

Amewataka wale wote waliokwishaibiwa kwa mtindo huo wakiwemo Viongozi wa Serikali pamoja na watoto wao, kujitokeza bila aibu kutoa taarifa katika vituo vya Polisi ili kusaidia kutoa maelezo yatakayosaiidia kuwanasa Matapeli hao na kuwafikisha mbele ya sheria kwa hatua zaidi.

Kamanda Aziz pia amesema kuwa mitandao ya simu pia imekuwa ikitumika kuwaibia watu na kwamba matapeli huigiza sauti za wakubwa katika kuomba fedha kwa baadhi ya wafanyabiashara na kupewa namba ya simu ambayo ataingiziwa fedha pasipokuonana.

Na wakati huo huo Serikali imeombwa kuhakikisha kuwa inaliwezesha usalama katika maeneo ya vivutio vya watalii ili kuiwezesha sekta hiyo kukuza uchumi wa visiwa hivyo.

Akizungumza na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi ACP Aziz Juma Mohammed, Mwenyekiti wa Mtandao wa Kukuza Utalii Visiwani Zanzibar (ZATI) Bw. Abdull Samadi, amesema kuwa kwa vile zaidi ya aslimia 60 ya mapato ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatokana na utalii, ipo haja sekta hii ikapewa kipaumbele katika usalama.

Amesema sekta ya utalii pia imesaidia ajira kwa vijana ambapo karibu vijana 20,000 wameajiriwa na baadhi yao wamejiajiri wenyewe kutokana na utalii aidha katika mahoteli ama kufanya biashara za kuuza bidhaa za utamaduni kwa watalii.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: