Mikutano na vikao mbalimbali vilivyokuwa vifanyike kwa maandalizi na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Wizara na Taasisi za serikali nchini Zambia vimeahirishwa mpaka hapo baadae ili kutoa nafasi kwa maandalizi ya mazishi ya Rais wa nchi hiyo Dokta Levy Patrick Mwanawasa (pichani).Miongoni mwa shughuli zilizoahirishwa ni vikao vya bunge la Jamhuri vilivyokuwa vinaendelea mjini Lusaka mpaka jana.
Spika wa bunge Mheshimiwa Amusaa Mwanamwambwa amesema wabunge watafahamishwa hapo baadae kurejea kwa shughuli za bunge hilo.
Amesema huu ni wakati wa majonzi makubwa kwa Zambia na kuwasihi wabunge wawe watulivu na waendelee kumuomba Mungu amani iliyopo idumu.
Mwandishi wa Taasisi ya Utangazaji Tanzania aliyekuwa ahudhurie kikao cha maandalizi ya maadhimisho ya siku 16 za Uanaharakati dhidi ya Unyanyasaji wa Kijinsia yanayotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 25 Novemba hadi tarehe 10 mwezi wa 12 alipokwenda kwenye eneo la kikao aliambiwa kikao kimeahirishwa mpaka atakapoarifiwa hapo baadae kutokana na msiba uliolikumba taifa.
Pia televisheni na vyombo vingine vya habari vimekuwa vikitangaza kuanzia jana usiku kuahirishwa kwa mikutano na vikao mbalimbali kutokana na sababu hiyo hiyo.
Vipindi vyote vya burudani kwenye redio na televisheni vimesimamishwa katika kipindi hiki cha siku saba za maombolezo ya kitaifa na badala yake nyimbo za maombolezo na mahubiri ya kuwatia wananchi nguvu na kusisitiza amani na utulivu yanaendelea kurushwa hewani na vyombo hivyo vya habari.
Wakati huo huo wananchi mbalimbali nchini humo wameeleza kutoridhishwa kwao na kuchelewa kutolewa kwa taarifa za mazishi ya Dokta Mwanawasa aliyefariki dunia jana asubuhi nchini Ufaransa alipokuwa kipatiwa matibabu kufuatia stroke aliyoipata alipokuwa akihudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika uliokuwa ukifanyika nchini Misri mwezi wa sita mwaka huu.
Wananchi hao waliokuwa wakihojiwa na redio Phinix wamesema ukimya huu unawaweka katika wasi wasi kwa kuwa hawajui kinachoendelea, na kuongeza kwamba hata hivyo wanaendelea kumuomba Mungu amani na mshikamano miongoni mwa wananchi viendelee.
Taarifa zaidi zinasema baadhi ya wananchi walikwenda shambani kwa Dokta Mwanawasa katika eneo linaloitwa Teka kwa nia ya kuomboleza hapo lakini Meneja wa shamba hilo aliwaomba wakaomboleze majumbani mwao kutokana na kutokuwa na taarifa kutoka kwa familia ya Dokta Mwanawasa kwamba shughuli za msiba huu mkubwa ziendelee shambani hapo.
Dokta Mwanawasa alizaliwa miaka 59 iliyopita alikuwa mtoto wa pili kati ya watoto kumi katika familia yao. Ameacha mke na watoto sita.
Makamu wa Rais wa Zambia na Kaimu Rais wa nchi hiyo kwa sasa Dokta Rupiah Banda jana saa saba mchana alitangaza kifo cha Dokta Mwanawasa kupitia televisheni ya Taifa ya nchi hiyo-ZNBC- na kuwataka wananchi wawe wavumilivu na watulivu na mpaka sasa hakuna taarifa zaidi zilizotolewa kuhusu mazishi ya kiongozi huyo.


Toa Maoni Yako:
0 comments: