Articles by "ELIMU."
Showing posts with label ELIMU.. Show all posts

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

KAMISHNA wa Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Lyabwene Mtahabwa (Pichani) amesema uwekezaji katika elimu ya awali ni msingi muhimu wa kujenga rasilimali watu bora kwa maendeleo ya Taifa, akibainisha kuwa changamoto kubwa iliyopo nchini ni uelewa mdogo wa jamii kuhusu mahitaji halisi ya mtoto katika umri wa awali.

Akizungumza kuhusu maendeleo ya elimu ya awali nchini, Dkt. Mtahabwa alisema uzoefu wake wa muda mrefu katika taaluma hiyo umeonesha wazi kuwa hatua za mwanzo za maisha ya mtoto, hususan kuanzia miaka sifuri hadi nane, zina mchango mkubwa katika kumjenga mtoto ambaye baadaye anakuwa rasilimali yenye tija kwa Taifa.

“Nimezeekea katika taaluma ya elimu ya awali na nina Shahada ya Tatu katika fani hiyo. Changamoto kubwa ninayoiona hapa Tanzania, hasa kwa watoto wa elimu ya awali, Darasa la Kwanza na la Pili, ni jamii kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu kile ambacho mtoto anatakiwa kupewa ili baadae awe na faida kubwa kwa Taifa,” alisema Dkt. Mtahabwa.

Alifafanua kuwa utu uzima wa mtu ni matokeo ya malezi, mazingira na elimu aliyopitia akiwa mtoto mdogo, akisisitiza kuwa umri wa miaka 0 hadi 8 ni kipindi nyeti kinachohitaji uangalizi, malezi sahihi na uwekezaji wa makusudi.

Dkt. Mtahabwa alieleza kuwa jitihada za Serikali za kujenga rasilimali watu bora haziwezi kufanikiwa endapo jamii haitatambua umuhimu wa kuwekeza ipasavyo katika maendeleo ya watoto wachanga. Alisisitiza kuwa elimu ya awali si suala la hiari, bali ni nguzo muhimu ya maendeleo ya Taifa kwa muda mrefu.

Aidha, aliitaka jamii kushirikiana na Serikali na wadau wa elimu kuhakikisha watoto wanapata mazingira bora ya kujifunza, malezi yenye upendo, lishe bora, afya njema na misingi imara ya maadili tangu wakiwa wadogo.

Alimalizia kwa kusisitiza kuwa dhana ya kujenga rasilimali watu bora inaanza na kujenga rasilimali watoto bora, akihimiza uwekezaji wa dhati katika elimu ya awali kama mkakati wa uhakika wa maendeleo endelevu ya Taifa.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) leo Januari 31, 2026 jijini Dar es Salaam limetangaza matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne uliofanyika Novemba 17, 2025, yakionyesha kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu kwa asilimia 2.61 na kufikia asilimia 94.98, hatua inayodhihirisha maboresho katika sekta ya elimu ya sekondari nchini.

Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo hayo, Katibu Mtendaji wa NECTA, Profesa Said Mohamed, amesema jumla ya watahiniwa 595,810 walisajiliwa kufanya mtihani huo, wakiwemo wasichana 318,910 sawa na asilimia 53.53 na wavulana 276,900 sawa na asilimia 46.47. Kati yao, watahiniwa 526,620 wamefaulu kwa kupata daraja la I, II, III na IV.

Profesa Mohamed amesema ufaulu wa daraja la kwanza hadi la tatu umeongezeka na kufikia jumla ya wanafunzi 255,404 sawa na asilimia 46.1 ya watahiniwa wote waliopata matokeo, hali inayoonesha kuimarika kwa ubora wa ufaulu ukilinganisha na mwaka uliopita.

Ameeleza kuwa jumla ya wanafunzi 569,883 walifanya mtihani huo wakiwa wamesajiliwa katika shule 5,864 nchini kote, huku watahiniwa wa kujitegemea wakiwa 25,927 waliosajiliwa katika vituo 813 vya mitihani.

Hata hivyo, NECTA imesema imefuta matokeo ya wanafunzi 77 kutokana na makosa ya kinidhamu ikiwemo kuandika lugha ya matusi katika skripti za mitihani na udanganyifu. Kati ya wanafunzi hao, 47 walitoka katika vituo vya mitihani na 30 walitoka shuleni.

Kwa mujibu wa NECTA, kati ya watahiniwa 526,620 waliofaulu, wasichana ni 278,108 sawa na asilimia 94.26 ya wasichana wote wenye matokeo, huku wavulana waliofaulu wakiwa 248,512 sawa na asilimia 95.79 ya wavulana wote wenye matokeo, jambo linaloonesha ufaulu wa juu kwa jinsia zote.

NECTA imeendelea kuwasisitiza wadau wa elimu kuimarisha maadili na nidhamu katika mitihani ya taifa, huku ikiwapongeza walimu, wazazi na wanafunzi kwa juhudi zinazoendelea kuchangia kuboresha matokeo ya elimu nchini.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Wakili Patrick Kipangula, amewahimiza wanafunzi wa uandishi wa habari kusoma, kuielewa na kuizingatia Sheria ya Huduma za Habari ili kujijenga kitaaluma na kuepuka migongano ya kisheria wanapoingia kwenye tasnia ya habari.

Wakili Kipangula ametoa wito huo wakati akitoa mhadhara kwa wanafunzi wa Mwaka wa Pili wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma, uliofanyika Januari 30, 2026, chuoni hapo. Mhadhara huo ulilenga kuwaongezea uelewa wanafunzi kuhusu majukumu ya JAB na misingi ya Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229.

Katika wasilisho lake, Wakili Kipangula ameeleza kuwa JAB ina jukumu la kusimamia ithibati ya waandishi wa habari nchini, kulinda taaluma ya uandishi wa habari na kuhakikisha maadili na weledi vinazingatiwa. Amesisitiza kuwa wanafunzi na waandishi chipukizi wanapaswa kuifahamu Sheria ya Huduma za Habari kabla ya kuanza kazi rasmi ili kujiepusha na makosa yanayoweza kuathiri taaluma yao.

Ameeleza pia kuwa ithibati na vitambulisho vya uandishi wa habari ni muhimu kwa wanafunzi wanapokuwa kwenye mafunzo kwa vitendo (field), akisisitiza kuwa uwepo wa nyaraka hizo unatoa uhalali wa kisheria katika utekelezaji wa majukumu ya kihabari, hususan wanapokuwa wakikusanya habari katika maeneo mbalimbali.
Akijibu swali kutoka kwa wanafunzi kuhusu mafunzo katika vyombo vya habari vya vyuo, ikiwemo Mlimani Radio na Televisheni pamoja na SAUT, Wakili Kipangula amesema Sheria inatambua uwepo wa wanafunzi katika vituo hivyo kwa kipindi maalumu cha mafunzo. Amesema baada ya kukamilisha muda wa mafunzo kwa vitendo, wanafunzi wanapaswa kurejea katika ratiba yao ya kawaida ya masomo chuoni.

Mhadhara huo umeelezwa kuwa sehemu ya juhudi za JAB katika kujenga uelewa wa kisheria kwa waandishi wa habari chipukizi, hatua inayolenga kuimarisha weledi, uwajibikaji na heshima ya taaluma ya uandishi wa habari nchini.
Na Mwandishi Wetu, Iringa

MKUU wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James (Pichani), ameonesha kukerwa na kitendo cha Mkuu wa Shule moja mkoani humo aliyerudisha nyumbani wanafunzi waliochelewa kuleta rimu baada ya shule kufunguliwa, akisema hatua hiyo imekosa hekima, busara na haizingatii ustawi wa watoto.

Akizungumza kuhusu hali ya lishe na upatikanaji wa chakula kwa wanafunzi shuleni, RC Kheri James amesema viongozi na watumishi wa umma wana wajibu wa kutumia busara katika kufanya maamuzi, hasa yale yanayohusu moja kwa moja haki na maisha ya watoto. Amesisitiza kuwa maamuzi yanayowagusa wanafunzi yanapaswa kufanywa kwa kuzingatia mazingira halisi ya jamii.

RC Kheri ameongeza kuwa si wazazi na walezi wote wana uwezo sawa wa kiuchumi, hivyo ni muhimu kwa viongozi wa shule kuelewa changamoto zinazowakabili baadhi ya familia kabla ya kuchukua hatua zinazoweza kuwaumiza watoto. “Hatuwezi kudhani kila mzazi ana uwezo sawa. Maisha ya watu yanatofautiana, na hili lazima litambuliwe,” amesema.

Aidha, amewataka viongozi wa elimu kuacha tabia ya kujisahau na badala yake waweke mbele maslahi ya wanafunzi, akisisitiza kuwa elimu ni haki ya msingi kwa kila mtoto na changamoto ndogo za vifaa vya shule hazipaswi kuwa sababu ya kuwanyima watoto haki hiyo.

Amehitimisha kwa kutoa wito kwa walimu wakuu na wasimamizi wa shule zote mkoani Iringa kuhakikisha wanajenga mazingira rafiki ya ujifunzaji, yanayochochea ushiriki wa wanafunzi wote bila ubaguzi, kwa lengo la kufanikisha maendeleo ya elimu na ustawi wa watoto.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo amezindua rasmi Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kisayansi wa Kujenga Umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa watoto wa elimu ya awali na wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la pili, uzinduzi uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Rais Dkt. Samia amesema Mkakati wa KKK ni miongoni mwa ahadi zake za siku 100 alizozitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, akisisitiza kuwa msingi wa elimu bora hujengwa katika hatua za awali za ujifunzaji.
Rais amesema mkakati huo unaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na wizara na taasisi nyingine zinazohusika na maendeleo ya awali ya mtoto, ili kuhakikisha utekelezaji wake unakuwa wa pamoja na wenye tija.

Amesema mtoto anayekosa stadi za msingi za kusoma, kuandika na kuhesabu mapema hukumbwa na changamoto kubwa katika masomo ya juu zaidi, hali inayomfanya kubaki nyuma kielimu. Aidha, Rais amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha watoto wote wanapata umahiri wa KKK kabla ya kufika darasa la tatu ili waweze kujifunza kwa ufanisi katika ngazi zinazofuata.
Katika maelekezo yake, Rais Dkt. Samia ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kushirikiana na TAMISEMI kuhakikisha maandalizi na utekelezaji wa mkakati huo yanafanyika kwa kutumia mbinu shirikishi, bunifu na za kisasa, ikiwemo matumizi ya zana na nyenzo za kufundishia zinazowavutia watoto.

Rais pia amesisitiza kuimarishwa kwa mifumo ya ukaguzi wa elimu, tathmini za mapema na endelevu za ujifunzaji pamoja na ufuatiliaji wa karibu wa utekelezaji wa mkakati huo ili kubaini changamoto kwa wakati na kuchukua hatua stahiki.

Amesema Mkakati wa KKK utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka wa fedha 2026/2027 hadi 2030/2031, sambamba na uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa katika sekta ya elimu ikiwemo ujenzi wa madarasa, kuajiri walimu wapya pamoja na kuimarisha rasilimali watu. Rais amebainisha kuwa Serikali imeajiri walimu 7,000 wa masomo ya Sayansi na Hisabati, ambapo walimu 6,044 tayari wameanza kazi.

Aidha, Rais Dkt. Samia ametambua mchango wa sekta binafsi na wadau wa maendeleo katika kuunga mkono utekelezaji wa mkakati huo, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa pamoja katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya elimu nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema utekelezaji wa Mkakati wa KKK unaenda sambamba na maboresho ya miundombinu ya elimu, sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 (Toleo la 2023), Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na Lengo Namba Nne la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG4) linalohusu elimu bora.

Profesa Mkenda ameongeza kuwa mkakati huo unaweka mkazo katika uwajibikaji, uwazi na kuzingatia matokeo halisi ya ujifunzaji wa watoto badala ya taarifa pekee, ili kuhakikisha watoto wote wanapata stadi stahiki za kusoma, kuandika na kuhesabu mapema.

Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kisayansi wa Kujenga Umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) unalenga kubadilisha kwa kiasi kikubwa matokeo ya ujifunzaji wa awali nchini, sambamba na mchango wa Tanzania katika utekelezaji wa Ajenda ya Afrika 2063.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akicheza pamoja na kikundi cha ngoma za asili cha Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kisutu mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), tarehe 29 Januari, 2026.



 Na Mwandishi Wetu – Dodoma

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imezindua rasmi mfumo mpya wa huduma kwa wateja unaotumia teknolojia ya akili unde (Artificial Intelligence) ujulikanao kwa jina la BWANABOOM, unaolenga kurahisisha na kuharakisha upatikanaji wa huduma kwa wadau wa elimu nchini kwa saa 24 kila siku.

Uzinduzi wa mfumo huo umefanyika leo Januari 28, 2026 katika ofisi za Makao Makuu ya HESLB jijini Dodoma, ukihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na wadau wa sekta ya elimu.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (WyEST), Profesa Daniel Mushi, ambaye ameipongeza HESLB kwa kuendelea kuwa kinara katika matumizi ya teknolojia za kisasa kuboresha huduma kwa wananchi.

“Leo tunaongeza huduma ya akili unde ‘BWANABOOM’ kama njia nyingine muhimu ya kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wadau wa elimu. Hili ni jambo la kujivunia na linapaswa kuigwa na taasisi nyingine nchini,” amesema Prof. Mushi.

Amesema mfumo huo ni hatua muhimu katika safari ya mageuzi ya kidijitali kwenye sekta ya elimu, na kusisitiza umuhimu wa HESLB kuendelea kuuboresha ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani.

Aidha, Prof. Mushi ametoa wito kwa HESLB kuzingatia kwa makini masuala ya usalama wa taarifa binafsi za watumiaji, kupima kiwango cha kuridhika kwa wateja mara kwa mara, pamoja na kuangalia uwezekano wa kuanzisha huduma za lugha ya ishara kidijitali ili kuwahudumia wadau wenye ulemavu wa kusikia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, amesema BWANABOOM ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa taasisi hiyo wa kutumia teknolojia za kisasa ili kuongeza ufanisi, uwazi na urahisi wa upatikanaji wa huduma kwa wanafunzi na wadau wengine wa elimu.

“Tunataka kuhakikisha huduma za HESLB zinawafikia wadau kwa urahisi zaidi, kwa wakati na kwa gharama nafuu kupitia majukwaa ya kidijitali,” amesema Dkt. Kiwia.

Naye Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Bi. Jaqueline Humbaro, amepongeza ubunifu huo na kuahidi kuwa balozi wa mfumo huo miongoni mwa wanafunzi ili wahakikishe wanatumia ipasavyo fursa hiyo mpya.

BWANABOOM unapatikana kupitia tovuti rasmi ya HESLB (www.heslb.go.tz) na pia ndani ya akaunti za wanafunzi kwenye mfumo wa SIPA, na unatarajiwa kupunguza gharama za usafiri, kuokoa muda, na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.

Uzinduzi wa mfumo huo unaonesha dhamira ya dhati ya HESLB katika kutumia teknolojia ya akili unde kama nyenzo ya kuleta mageuzi chanya katika maendeleo ya elimu nchini.
Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Iringa, Dkt. Tumaini Msowoya, amewataka wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Iringa kuwa makini na maisha ya chuoni kwa kujiepusha na ndoa za rejareja, makundi yasiyo na tija pamoja na tabia zinazoweza kuwavuruga kimasomo, huku akisisitiza umuhimu wa uzalendo na nidhamu binafsi.

Akizungumza wakati wa sherehe za kuwapokea wanafunzi wa mwaka wa kwanza, Dkt. Msowoya alisema licha ya wanafunzi kuwa na umri wa zaidi ya miaka 18 kisheria, bado wanapaswa kujiuliza iwapo ndoa au mahusiano ya kuishi pamoja ndiyo yamewaleta chuoni, au ni dhamira ya kutimiza ndoto zao za kielimu.
“Najua mna umri wa zaidi ya miaka 18 hivyo si watoto kwa mujibu wa sheria, lakini jiulizeni: je, ndoa ndiyo imekuleta chuoni? Wazazi wenu wanajua mmeoa au mmeolewa mkiwa hapa?” alihoji Dkt. Msowoya.

Aliongeza kuwa tafiti alizowahi kufanya kuhusu maisha ya wanafunzi wa vyuo vikuu zimebaini kuwa wanafunzi wengi huishi na wenza wao kwa siri bila familia zao kufahamu, jambo alilolitaja kuwa ni hatari na linaloweza kuathiri mwenendo wa masomo na maisha ya baadaye.

Dkt. Msowoya aliwahimiza wanafunzi kuipenda nchi yao, kusoma kwa bidii na kuepuka kujiingiza katika makundi yasiyo na mwelekeo chanya, akisisitiza kuwa wasomi ndio tegemeo la maendeleo ya taifa.

Katika hafla hiyo, Dkt. Msowoya alimwakilisha Dikson Mwipopo, Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Iringa ambaye alikuwa mgeni rasmi. Mwipopo aliwapongeza wanafunzi hao na kuchangia shilingi milioni 2,000,000 kwa ajili ya kuwasaidia katika safari yao ya masomo.

Amesisitiza kuwa nidhamu, maamuzi sahihi na uzalendo ni misingi muhimu kwa mwanafunzi yeyote anayelenga kufanikiwa chuoni na katika maisha kwa ujumla.
Buyu, Zanzibar

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali imedhamiria kufanya mageuzi makubwa katika sekta za elimu, sayansi, utafiti na ubunifu ili kujenga uchumi imara, shindani na endelevu, unaowanufaisha Watanzania kwa upana zaidi.

Rais Samia ameyasema hayo Januari 8, 2026, katika eneo la Buyu, visiwani Zanzibar, mara baada ya kuzindua Jengo la Taaluma na Utawala la Taasisi ya Sayansi za Bahari Zanzibar (UDSM–IMS). Amesisitiza kuwa taasisi hiyo ni mdau muhimu wa Serikali katika kukuza uchumi shirikishi, hususan uchumi wa buluu, unaotegemea rasilimali za bahari.

Amesema uwepo wa IMS utaimarisha uvuvi endelevu, utalii wa baharini, pamoja na ulinzi na matumizi bora ya rasilimali za bahari, hivyo kuchangia moja kwa moja katika kukuza pato la Taifa na ustawi wa wananchi.
Katika hotuba yake, Rais Samia ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa usimamizi mzuri wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), akisema mradi huo umeleta matokeo chanya katika miundombinu na ubora wa elimu ya juu nchini. Aidha, amewahimiza vijana kutumia fursa zilizopo kupata elimu na ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.

Rais pia amewapongeza viongozi na watumishi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa kukamilisha mradi huo kwa wakati na kwa viwango vya juu, huku akiishukuru Benki ya Dunia kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa Mradi wa HEET.

Aidha, amewataka wahadhiri na watafiti kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi ili tafiti na bunifu zitakazofanywa ziweze kuleta matokeo ya moja kwa moja katika maendeleo ya Taifa. Vilevile, amewahimiza wanafunzi kuwa walinzi na mabalozi wa rasilimali za bahari kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amesema ameiomba Serikali kushirikiana na Benki ya Dunia ili kuanzisha Awamu ya Pili ya Mradi wa HEET, itakayowezesha kukamilisha maeneo ya utekelezaji ambayo bado hayajakamilika.

Dkt. Kikwete amesema majengo mapya yaliyozinduliwa ni msingi muhimu wa kuendeleza tafiti za kisasa, kutoa mafunzo bora na kukuza uchumi wa buluu, sambamba na kuchochea maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye, amesema uwekezaji huo utaongeza kwa kiasi kikubwa idadi ya wanafunzi katika Taasisi ya Sayansi za Bahari (IMS). Amesema kwa sasa IMS ina uwezo wa kudahili takribani wanafunzi 172 kwa mwaka, lakini baada ya kukamilika kwa miundombinu hiyo, uwezo utaongezeka hadi wanafunzi 472 kwa mwaka, sawa na ongezeko la wanafunzi 300.

Prof. Anangisye ameongeza kuwa IMS inaingia awamu mpya ya maendeleo kufuatia uzinduzi wa miundombinu ya kisasa katika eneo la Buyu, pamoja na kuimarishwa kwa vituo vya Mizingani na Pangani, hatua itakayoongeza uwezo wa taasisi katika kufundisha, kufanya tafiti na kuendeleza bunifu zitakazochangia maendeleo ya Taifa.
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Rais Mstaafu Wa Awamu ya Nne Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akimpongeza Mhitimu wa Shahada ya Awali ya Sheria ambaye alivunja rekodi iliyodumu miaka 32 kwa kupata Daraja la Kwanza katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (The Law School of Tanzania), rekodi iliyokuwa inashikiliwa na Profesa wa sheria UDSM Prof. Hamudi Majamba.
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Rais Mstaafu Wa Awamu ya Nne Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akimpongeza Bi. Mary Barney Isaac Laseko Mhitimu wa Shahada ya Awali ya Sheria ambaye amevunja rekodi iliyodumu miaka 32 kwa kupata Daraja la Kwanza katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (The Law School of Tanzania), rekodi iliyokuwa inashikiliwa na Profesa wa sheria UDSM Prof. Hamudi Majamba. Pemebni ni wazazi wake Bw. Barney Isaac Laseko na Mama Laseko.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambaye pia ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ameongoza hafla ya Mahafali ya 55 (Duru la Tatu) ya Chuo Kikuu hicho, na kumpongeza mhitimu aliyeng’ara kwa kuvunja rekodi iliyodumu kwa zaidi ya miaka 32 katika historia ya The Law School of Tanzania.

Mhitimu huyo, Bi. Mary Barney Laseko, ambaye ni mhitimu wa Shahada ya Awali ya Sheria (LLB), ameweka historia kwa kupata Daraja la Kwanza katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania—rekodi ambayo mara ya mwisho ilipatikana zaidi ya miongo mitatu iliyopita chini ya Profesa Hamudi Majamba wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Aidha, Mary anajiunga katika orodha ya wanawake wachache waliowahi kufanya hivyo, akifuata nyayo za Dkt. Asha-Rose Migiro, Katibu Mkuu wa CCM, ambaye alikuwa mwanamke wa kwanza kupata daraja hilo kutoka Law School of Tanzania.

Hafla hiyo imefanyika leo katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, ambapo Dkt. Kikwete amewatunuku Shahada na Stashahada wahitimu 2,452. Kati yao, 1,386 (sawa na asilimia 56.6) ni wanawake, ikionyesha mwamko na ushiriki mkubwa wa wanawake katika elimu ya juu.

Katika picha zilizopigwa na mpiga picha mkongwe Issa Michuzi, Dkt. Kikwete anaonekana akimpongeza Bi. Mary kwa mafanikio yake, huku picha nyingine zikimuonyesha akiwa na wazazi wake, Bw. Barney Isaac Laseko na Mama Laseko, waliokuwa wakijivunia mafanikio ya binti yao.

Kwa mujibu wa uongozi wa chuo, mafanikio ya Mary yamepokelewa kama ishara ya ongezeko la ubora, nidhamu na juhudi za wanafunzi wanaosomea sheria nchini.