Na Albano Midelo
Wakati wengi walidhani ajali ilizika ndoto zake milele, Deogratius Chami ameandika historia mpya Tanzania kwa kuwa mtu wa kwanza mwenye ulemavu wa kutumia kiti mwendo kufika kilele cha Mlima Kilimanjaro (Uhuru Peak, mita 5,895).
Chami, mzaliwa wa Moshi ambaye hivi sasa ni Mkurugenzi wa Kilimanjaro Disability Royour Tour and Safaris, alifikia mafanikio ya kupanda mlima Kilimanjaro baada ya safari ya siku saba mwaka 2014, na kurudia tena mwaka 2023 kwa siku sita pekee.
Mrajisi wa Ushirika Mkoa wa Ruvuma Venance Msafiri akizungumza siku ya maadhimisho ya siku ya ushirika Duniani ambayo yalifanyika wilayani Nyasa mkoani Ruvuma,amesema ushirika umechangia mafanikio ya mwenye ulemavu huyo baada ya kumpatia mkopo wa maendeleo wa shilingi milioni nane mwaka 2023, hivyo kufanikiwa kuanzisha kampuni hiyo ya utalii..
Amesema Kupitia kampuni hiyo Chami sio tu anautangaza utalii,bali pia anautangaza ushirika na kwamba wanatarajia kumualika mkoani Ruvuma ili aweze kuja kutembelea vivutio vya Mkoa wa Ruvuma hususani wilaya ya Nyasa ambayo ni kitovu cha utalii katika Mkoa.
Akiwa na miaka 13 darasa la sita shule ya msingi Kilimanjaro,Chami alipata ajali mbaya ilimlaza kwa karibu miaka miwili katika Hospitali ya KCMC Moshi. Ndoto zake za kuwa mwanajeshi na mchezaji wa mpira zilionekana kufutika.
Hata hivyo, ushauri wa mwalimu wake wa shule ya msingi ulimgeuza kutoka nafasi ya 129 darasani hadi kuwa miongoni mwa wanafunzi bora, hatua iliyomfikisha hadi Shahada ya Maendeleo ya Jamii na Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi mwaka 2013.
Kwa mujibu wa WHO (2023), watu bilioni 1.3 duniani wanaishi na ulemavu, sawa na asilimia 16 ya idadi ya watu wote. Chami amethibitisha kuwa ulemavu si mwisho wa mafanikio bali mwanzo wa njia mpya ya ushindi.
Picha mbalimbali za Deogratias Chami mtanzania wa kwanza mwenye ulemavu kupanda mlima kilimanjaro hadi kileleni kwa kutumia kiti mwendo ,Chami amepanda mlima kilimanjaro mara mbili mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2014 ambapo alitumia siku saba kufikia kileleni na mara ya pili mwaka 2023 akiwa na kampuni yake ya utalii alifanikiwa kupanda mlima kilimanjaro kwa kutumia siku sita hadi kileleni.





Toa Maoni Yako:
0 comments: