
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Benki ya Exim Tanzania imeendesha zoezi la kitaifa la uchangiaji damu wa hiari kwa kushirikiana na Taasisi ya Taifa ya Mpango wa Damu Salama (NBTS), ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 11 ya ushirikiano wao unaolenga kuimarisha upatikanaji wa damu salama nchini.
Zoezi hilo lililofanyika Juni 10, 2026, limefanyika katika mikoa sita ambayo ni Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Mbeya, Tabora na Mtwara. Lengo lake ni kuhamasisha wananchi kujitokeza kuchangia damu ili kusaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa damu katika hospitali na vituo vya afya nchini.
Kwa zaidi ya miaka kumi, Benki ya Exim Tanzania na NBTS wamekuwa wakishirikiana kuhamasisha utamaduni wa uchangiaji damu wa hiari. Kupitia kampeni hizo, zaidi ya chupa 800 za damu hukusanywa kila mwaka, hatua inayosaidia kuokoa maisha ya kina mama wanaopata changamoto wakati wa kujifungua, waathirika wa ajali, wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji, watoto na wengine wanaohitaji kuongezewa damu kutokana na matatizo mbalimbali ya kiafya.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo katika makao makuu ya Benki ya Exim jijini Dar es Salaam, Meneja Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo, Kauthar D'souza, alisema mpango huo unaonesha dhamira ya taasisi hiyo katika kuunga mkono vipaumbele vya afya vya taifa.
"Benki ya Exim tunaamini jukumu letu haliishii katika utoaji wa huduma za kifedha pekee, bali pia kuwa mshirika wa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla. Kupitia programu yetu ya Exim Cares, tunaendelea kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, ubunifu, uhifadhi wa mazingira na uwezeshaji wa jamii ili kuleta mabadiliko chanya na endelevu," alisema Kauthar.
Aliwahimiza Watanzania wenye sifa za kuchangia damu kujitokeza kushiriki katika kampeni hiyo, akieleza kuwa dakika chache za mtu kutoa damu zinaweza kuokoa maisha ya wengine. "Mchango wako unaweza kuwa sababu ya mama kurudi salama kwa familia yake, mtoto kupata matibabu anayohitaji au mgonjwa kupewa nafasi nyingine ya kuendelea kuishi," aliongeza.
Kwa upande wake, Afisa Uhamasishaji wa Damu Salama Kanda ya Mashariki kutoka NBTS, Evelyn Dielly, aliipongeza Benki ya Exim kwa ushirikiano wake wa muda mrefu katika kuimarisha juhudi za ukusanyaji damu nchini.
"Tunathamini mchango wa Exim Bank katika kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa uchangiaji damu wa hiari na kuboresha upatikanaji wa damu kwa wagonjwa kote nchini. Kila chupa ya damu inayokusanywa husaidia kuokoa maisha na kusaidia vituo vya afya kukabiliana na mahitaji ya dharura ya kitabibu," alisema Evelyn.
Kampeni hiyo ya kila mwaka, ambayo sasa imefikisha miaka 11, inaendelea kuwa mfano wa ushirikiano wenye tija kati ya sekta binafsi na taasisi za umma katika kuimarisha huduma za afya na kukuza utamaduni wa uchangiaji damu wa hiari nchini Tanzania.





Toa Maoni Yako:
0 comments: