
Na Mwandishi Wetu
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt. Dotto Kuhenga, ametoa mhadhara kuhusu nafasi ya vyombo vya habari nchini Tanzania na mchango wake kwa jamii kwa wanafunzi na maprofesa kutoka Chuo Kikuu cha Washington and Lee cha nchini Marekani.
Mhadhara huo uliotolewa kwa wanafunzi wa Programu ya Masomo ya Majira ya Kiangazi (Summer School), ulihusisha majadiliano mbalimbali kuhusu vyombo vya habari, jamii na mafunzo katika mazingira ya kimataifa.
Akizungumza kupitia ukurasa wake wa Facebook, Dkt. Kuhenga alisema kikao hicho kilijaa majadiliano ya kuvutia, maswali mbalimbali pamoja na kubadilishana uzoefu na mitazamo tofauti kuhusu nafasi ya vyombo vya habari katika maendeleo ya jamii.
Alieleza kuwa majadiliano hayo yalitoa fursa ya kujifunza zaidi kupitia maingiliano ya kitaaluma na kuimarisha uelewa kuhusu namna vyombo vya habari vinavyoweza kuathiri jamii katika mazingira ya sasa ya kidijitali.
Aidha, alisema uzoefu huo umekuwa ukikumbusha kuwa ualimu wenye matokeo chanya haujengwi katika kutoa maarifa pekee, bali pia kupitia kusikiliza, kujifunza na kukua kwa pamoja kupitia majadiliano yenye tija.Mhadhara huo umeonekana kuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma na kubadilishana uzoefu wa kimataifa katika sekta ya elimu, mawasiliano na vyombo vya habari.




Toa Maoni Yako:
0 comments: