Na Mwandishi Wetu
Wadau wa sekta ya usafiri wa majini katika mikoa ya Mwanza, Kigoma na Kagera arehe 16 Aprili, 2026 wamejitokeza na kutoa maoni yao kuhusu athari za ongezeko la bei ya mafuta, wakisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua stahiki zitakazolinda maslahi ya wananchi pamoja na uendelevu wa huduma hiyo.
Wakizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), maafisa waratibu wa vikao hivyo, wamesema kuwa vikao hivyo vimeandaliwa kwa lengo la kukusanya maoni ya wadau kabla ya kufikia uamuzi wowote kuhusu marekebisho ya nauli za usafiri wa majini.
Wameongeza kuwa vikao hivyo vimeitishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 29 cha Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania, Sura 415, kinachoitakaTASAC kuwashirikisha wadau mbalimbali ili kupata maoni katika michakato mbalimbali inayohitaji maoni ya wadau.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika mkoani Kagera, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) wa Mkoa wa Kagera, Bw. Isaya Tendega, ameipongeza TASAC kwa kuandaa vikao hivyo ambavyo vimefanyika katika wakati muafaka kufuatia mabadiliko ya bei ya mafuta yaliyoanza kutumika hivi karibuni, hali inayoweza kuongeza gharama za uendeshaji wa vyombo vya usafiri majini na kuathiri maisha ya wananchi.
Baadhi ya wadau walioshiriki mkutano huo walieleza kuwa ni muhimu kwa mamlaka husika kuzingatia uwiano kati ya gharama za uendeshaji na uwezo wa wananchi kumudu nauli ili kuepusha kuwaongezea mzigo wananchi, hususan wale wanaotegemea usafiri wa majini kwa shughuli zao za kila siku.
Aidha, wadau wengine walipendekeza kuwepo kwa mikakati mbadala ya kupunguza gharama za uendeshaji, ikiwemo matumizi ya nishati mbadala na kuboresha ufanisi wa vyombo vya usafiri, badala ya kutegemea zaidi ongezeko la nauli.
TASAC imebainisha kuwa itaendelea kupokea maoni hadi tarehe 26 Aprili, 2026 kabla ya kukamilisha mchakato wa kufanya maamuzi ambao utakuwa shirikishi na wa uwazi, ukizingatia maoni ya wadau wote pamoja na hali halisi ya soko.











Toa Maoni Yako:
0 comments: