Dar es Salaam, Septemba 8, 2025: Baraza la Habari Tanzania (MCT) limetoa wito kwa vyombo vya habari nchini, vikiwemo vya mtandaoni, kuzingatia maadili ya uandishi wa habari kwa dhati na kuhakikisha taarifa zinazochapishwa au kutangazwa ni sahihi, zenye ushahidi na zisizochochea chuki katika jamii, hususan katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.Katika tamko lake, MCT limesisitiza kuwa kila chombo cha habari kina wajibu wa kuhakikisha taarifa inayoifikia jamii imehakikiwa kwa kina ili kuepusha usambazaji wa taarifa potofu (misinformation), taarifa za uongo (disinformation) na hotuba za chuki (hate speech).
“Maneno yana maana, picha zina maana, na namna tunavyoeleza habari zetu kuna maana kubwa – kwa sababu inaweza kutuunganisha au kutugawa. Ni wajibu wa vyombo vya habari kuwa walinzi wa ukweli,” alisema Katibu Mtendaji wa MCT, Ernest S. Sungura.
Kwa mujibu wa Kanuni za Maadili za mwaka 2020, MCT inasisitiza kuwa kabla ya kuchapisha habari yenye madai au tuhuma, waandishi wa habari wanapaswa kumpa nafasi na haki ya kujibu mhusika au taasisi iliyoathiriwa. Endapo majibu hayapatikani kwa wakati, mhariri anaweza kuendelea kuchapisha ikiwa ameridhika kuwa kuna maslahi ya umma, lakini kwa maelezo yanayoonyesha jitihada za upatikanaji wa upande wa pili.
MCT imeeleza kuwa hivi karibuni kumejitokeza matukio yanayoashiria ukiukwaji wa maadili ya habari, hali inayoweza kudhoofisha imani ya umma kwa vyombo vya habari. Hivyo, baraza limefanya mafunzo katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na Zanzibar kwa wahariri na waandishi ili kuwaongezea uwezo wa kitaaluma na maadili.
“Baraza la Habari Tanzania linaendelea kusimamia maadili, kuhimiza weledi na kulinda heshima ya taaluma ya habari. Tunawahimiza waandishi na watangazaji wote kutanguliza maslahi ya taifa na umoja wa jamii katika kazi zao,” ilisisitiza sehemu ya tamko hilo.
MCT, ambalo lilianzishwa mwaka 1995, limekuwa likisimamia weledi wa vyombo vya habari na linaendelea kukumbusha kuwa kufuata maadili si hiari, bali ni wajibu wa kitaaluma na kinga thabiti dhidi ya hatua za kisheria zinazoweza kuchukuliwa na mamlaka husika.


Toa Maoni Yako:
0 comments: