Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.

Familia ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mzee Ali Hassan Mwinyi, imepata msiba mkubwa kufuatia kifo cha Abbas Ali Hassan Mwinyi kilichotokea jana alfajiri, Septemba 25, 2025.

Taarifa hiyo imetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kupitia ukurasa wake wa Instagram, ambapo alithibitisha kifo cha kaka yake mpendwa kwa masikitiko makubwa.

“Kwa huzuni na masikitiko makubwa, sisi familia ya Mzee Ali Hassan Mwinyi tunatangaza kifo cha kaka yetu mpendwa, Abbas Ali Hassan Mwinyi, aliyefariki dunia leo asubuhi,” aliandika Dk. Mwinyi.

Marehemu Abbas Mwinyi, ambaye alikuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Fuoni kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi uliopita, pia aliwahi kuwa msemaji wa familia ya Mwinyi wakati wa msiba wa Mzee Ali Hassan Mwinyi, akiwajibika kwa umakini mkubwa kutoa taarifa kwa umma.

Mwili wa marehemu unatarajiwa kusaliwa kesho Ijumaa, Septemba 26, 2025, katika Masjid Jamia Zinjibar, Mazizini mara baada ya Sala ya Ijumaa, na baadaye kuzikwa nyumbani kwao Mangapwani, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Aidha, Dk. Mwinyi alimuombea marehemu msamaha na rehema za Mwenyezi Mungu, akiandika: “Mwenyezi Mungu amsamehe madhambi yake, amzidishie rehema na amjalie makaazi mema peponi. Ameen.”

Msiba huu umetokea kipindi ambacho familia ya Mwinyi inaendelea kuwa mhimili muhimu katika historia ya taifa, hivyo wananchi, viongozi wa kitaifa pamoja na wananchi wa kawaida wameendelea kuonyesha mshikamano kwa kutuma salamu za rambirambi na kuifariji familia hiyo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: