

Onesho la vitendo la uandikishaji likifanywa na wataalam kutoka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Washiriki mbalimbali wakiwa katika mkutano huo mkoani Morogoro.
**********************
Na. Mwandishi Wetu
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza kuanza kwa mzunguko wa 12 wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambao utafanyika mkoani Morogoro na sehemu ya mkoa wa Tanga kwa siku saba kuanzia tarehe 01 had 07 Machi, 2025.
Akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi mkoani Morogoro leo tarehe 17 Februari, 2025, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji Rufaa, Jacobs Mwambegele amesema uboreshaji huo utafanyika kwenye mkoa huo na mkoani Tanga kwenye halmashauri za Wilaya ya Bumbuli, Handeni, Pangani na Mkinga.
“Kwa mujibu wa ratiba, kwa sasa Tume imeanza maandalizi ya mzunguko wa 12 kati ya mizunguko 13 ya uboreshaji wa Daftari. Mzunguko huu wa 12 unahusisha Mkoa huu wa Morogoro na Mkoa wa Tanga katika Halmashauri za Wilaya ya Bumbuli, Handeni, Pangani na Mkinga,” amesema Jaji Mwambegele.
Amesema mikoa 27 tayari imekamilisha zoezi hilo ambayo ni pamoja na Kigoma, Tabora, Katavi, Geita, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Mara, Simiyu, Manyara, Dodoma na Singida.
Ameitaja mikoa mingine kuwa ni Mjini Magharibi, Kusini Unguja, Kaskazini Unguja, Kusini Pemba, Kaskazini Pemba, Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, Iringa, Rukwa, Songwe, Njombe, Ruvuma, Lindi na Mtwara.
“Mikoa miwili ya Pwani na sehemu ya mkoa wa Tanga kwenye Halmashauri ya Jiji la Tanga, Halmashauri za Miji ya Handeni na Korogwe na Halmashauri za Wilaya ya Kilindi, Lushoto na Muheza inatarajia kukamilisha zoezi hilo tarehe 19 Februari, 2025,” amesema.
Wakati huohuo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ndugu. Kailima Ramadhani amesema Tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 302,752 mkoani Morogoro sawa na ongezeko la asilimia 18.7 ya wapiga kura 1,612,952 waliokuwepo kwenye daftari la wapiga kura mwaka 2020.
“Tume inatarajia baada ya uandikishaji Mkoa wa Morogoro utakuwa na wapiga kura 1,915,704. Idadi hii inaweza kuongezeka kwa kuwa inawezekana wapo watanzania ambao walikuwa na sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura wakati wa uboreshaji wa Daftari mwaka 2019/20, lakini kwa sababu moja au nyingine hawakuweza kujiandikisha,” amesema.
Ameongeza kuwa Mkoa wa Morogoro una vituo 2,816 vitakavyotumika kwenye uboreshaji wa daftari ikiwa ni ongezeko la vituo 112 katika vituo 2,704 vilivyotumika kwenye uboreshaji mwaka 2019/20.
Toa Maoni Yako:
0 comments: