Katibu Tawala wa Wilaya ya Ikungi, Rashid M. Rashid (kulia) akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Kongamano la Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Mkoa wa Singida walipomtembelea ofisi kwake Agosti 29, 2023 kwa ajili ya kuzungumzia kongamano hilo litakalofanyika Oktoba 7, 2023.
Na Dotto Mwaibale, Singida
SHUJAA wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Mkoa wa Singida wanatarajia kufanya kongamano kubwa la wazi na la kihistoria ambalo pamoja na mambo mengine litajadili suala la uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam, ukatili wa kijinsia na mambo mengine ambapo linawaomba wadau mbalimbali kusaidia kuchangia Sh. Milioni 11.5 kwa ajili ya kufanikisha kongamano hilo.
Kamati ya maandalizi ya kongamano hilo wakiongonzwa na Mwenyeki wa Smaujata Mkoa wa Singida, Dismas Kombe wameeleza nia ya kongamano hilo walipokutana na Katibu Tawala wa Wilaya ya Ikungi, Rashid M. Rashid , Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Haika Masawe, Afisa Ustawi wa Jamii wa wilaya hiyo, Robby Muhochi pamoja na Mkuu wa Polisi wa Wilaya hiyo Mrakibu wa Polisi (OCD), Suzana Kidiku.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Juma Amrani akizungumza lengo la kongamano hilo ambalo litafanyika Oktoba 7, 2023 Stendi ya Mabasi ya zamani mjini hapa na kuwa na watu zaidi ya 1000, alisema ni kutoa elimu juu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia, uchangiaji wa damu salama, elimu kuhusu mkataba wa Bandari ya Dar es Salaam, dira ya maendeleo ya Taifa letu kuanzia mwaka 2025/ 2050.
Amrani alitaja mambo mengine yatakayokuwepo kwenye kongamano hilo kuwa ni elimu salama mashuleni hasa kwa mtoto wa kike na kupunguza alama ziro na kwamba watakuwepo wataalamu mbalimbali wakiwemo Maafisa Ustawi wa Jamii na maendeleo ambao watatoa mada.
Alisema kuwa katika kongamano hilo kutakuwa na viongozi wa Serikali, dini wananchi, wanafunzi na kuwa litanogeshwa na burudani za aina tofauti tofauti kama muziki wa kizazi kipya, asili, mashairi, ngonjera na nyimbo ambazo Smaujata wataziandaa zenye mafundisho ya kupinga ukatili.
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Omari Mwangi alisema wanaamini kupitia kongamano hilo jamii itapata elimu na kupunguza kama sio kumaliza vitendo vya ukatili vilivyokithiri kutokana na kumomonyoka kwa maadili ambapo kwa upande mwingine kunachangiwa na wazazi au walezi.
'' Wazazi wengi wamekuwa wakikwepa majukumu ya malezi ya watoto wao na kuwaacha wafanye mambo yao jambo ambalo limewafanya wajikute wakiingia katika makundi yasiofaa na kuanza kufanya vitendo vilivyo kinyume na maadili,'' alisema Mwangi.
Makamu Mwenyekiti wa Smaujata Mkoa wa Singida, Ambwene Kajula alisema kuwa lengo la kongamano hilo ni kuwapata viongozi ili wapate majibu ya moja moja kutoka na changamoto mbalimbali walizonazo wananchi dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
'' Tuliona kongamano itakuwa njia rahisi ya kuwakutanisha wananchi wengi na viongozi wao wengi kutoka wilaya zote za Mkoa wa Singida ili wajue changamoto zao pia itakuwa ni fursa kwa Smaujata kujitangaza,''.
Alisema pamoja na jitihada kubwa inayofanywa na Smaujata ya kupambana na vitendo vya ukatili bado elimu haijawafikia watu wengi na kupitia kongamano hilo wataweza kuipata kupitia michezo ya kuigiza na kuwa kutakuwa na makala maalumu ya video 'Ducumentary' ambayo itaonesha watu wakitoa shuhuda za ukatili wa kijinsia na hatua zilizochukuliwa dhidi ya watuhumiwa wa vitendo hivyo.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Ikungi, Rashid M. Rashid
na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Haika Masawe waliipongeza Smaujata kwa kuandaa kongamano hilo ambalo ni muhimu katika kutokomeza vitendo vya ukatili si kwa Mkoa wa Singida pekee bali kwa nchi nzima ambapo wameonesha kila nia ya kuchangia ili kulifanikisha na kuwataka waandike barua rasmi ya maombi ili ipelekwe ngazi za juu kwa ajili ya utekelezaji.
Kwa upande wake Mkuu wa Polisi wa wilaya hiyo Mrakibu wa Polisi (OCD), Suzana Kidiku aliwapongeza Smaujata kwa kuandaa kongamano hilo ambalo linakwenda kuwa msaada katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili na uharifu.
Alisema katika wilaya hiyo kumekuwa na wimbi kubwa la watoto ambao wanafanya uharifu mkubwa jambo ambalo linaleta changamoto kubwa ya kuwahifadhi kwani hawawezi kuwaweka mahabusu ya watu wakubwa kulingana na sheria zinazowalinda.
Mkuu huyo wa wilayani humo alisema kukithiri kwa utoro wa watoto mashuleni ndio chanzo kikubwa cha kujiingiza kwenye vitendo vya uharifu huku matukio ya ubakaji na ulawiti yakiongeza kila kukicha.
Aidha, Kidiku alisema ili kuthibiti utoro huo wameanzisha utaratibu kwa watoto vinara wa utoro kusaini kila asabuhi wanapofika fika shuleni na wanapotoka katika daftari maalum litakalokuwa kwa mkuu wa polisi wa kata ilipo shule husika wanazosoma ambapo pia litakuwa likisainiwa na mwalimu wa darasa la mwanafunzi na kuwa utaratibu huo wamehusishwa na wazazi wao.
Katika kuwaunga mkono Smaujata, Kidiku aliahidi kutoa kiasi cha fedha ambazo zitasaidia kununulia maji ya kunywa wakati wa kongamano hilo.
Mwenyekiti wa Smaujata Mkoa wa Singida, Dismas Kombe aliwashukuru viongozi wa wilaya hiyo kwa mapokezi mazuri waliowapa na akawaomba wadau wengine kujitokeza kusaidia ili wapate kiasi hicho cha fedha.
Alisema kwa mtu yeyote, Taasisi, Wafanyabiashara, makundi mengine na madhehebu ya dini watakao kuwa tayari wana weza kuwasiliana na waratibu , Dismas Kombe kwa namba ya simu 0758489886, Mwenyekiti wa Kongamano, Juma Amrani kwa namba 0763850879 na Makamu Mwenyekiti wa Smaujata Mkoa wa Singida, Ambwene Kajula kwa simu namba 0713343687 na Makamu Mwenyekiti wa kongamano hilo, Omary Mwangi kwa namba ya simu 0782651919.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Juma Amrani alimpongeza Mwenyekiti wa Smaujata Wilaya ya Ikungi, Hussein Mseule kwa kuratibu ziara hiyo ambayo imeonesha mafanikio makubwa na mapokezi mazuri ya kamati hiyo.
Kamati hiyo inatarajia kuendelea na ziara hiyo ya kuwaomba wadau kuchangia kongamano hilo katika Wilaya za Mkalama, Iramba, Manyoni na Itigi.
Timu nzima ya Smaujata ambayo ilishiriki kwenye ziara hiyo ni Wajumbe wa kamati ya maandalizi ya kongamano hilo Omari Mwangi Makamu Mwenyekiti, Mwenyekiti Juma Amrani, Katibu, Beatrice Claud na Mweka Hazina Elineema Babu.
Wengine ni Katibu wa Smaujata Mkoa wa Singida, Patrick Msinda, Katibu wa Smaujata Wilaya ya Ikungi, Maxwell Ngwallo, Ester Issaya na Rehema Mangula.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Haika Masawe, (kulia) akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Kongamano la Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Mkoa wa Singida walipomtembelea ofisi kwake Agosti 29, 2023 kwa ajili ya kuzungumzia kongamano hilo litakalofanyika Oktoba 7, 2023.
Wajumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Kongamano la Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Mkoa wa Singida wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ikungi, Mrakibu wa Polisi , Suzana Kidiku baada ya kumtembelea ofisini kwake.
Kikao na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Haika Masawe kikiendelea. Kushoto ni Mtunza fedha wa kamati hiyo, Elineema Babu na kulia ni Mjumbe wa kamati hiyo kutoka Manyoni, Rehema Mangula.
Wajumbe wa kamati hiyo wakiwa katika picha ya pamoja na Katibu Tawala wa Wilaya ya Ikungi, Rashid M. Rashid.]wa sita kutoka kushoto}
Makamu Mwenyekiti wa kamati ya kongamano hilo, Omari Mwangi akizungumza kwenye kikao hicho.
Mwenyekiti wa Smaujata Mkoa wa Singida, Dismas Kombe akichangia jambo wakati akiwatambulisha wajumbe wa kamati ya kongamano hilo.
Wajumbe wakiwa katika picha ya pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Haika Masawe.
Makamu Mwenyekiti wa Smaujata Mkoa wa Singida, Ambwene Kajula akizungumza kwenye kikao hicho.
Kikao na Katibu Tawala Wilaya ya Ikungi kikiendelea.
Mwenyekiti wa kamati ya kongamano hilo, Juma Amrani akitoa taarifa ya kongamano hilo kwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Ikungi } hayupo pichani}
Mwenyekiti wa Smaujata Wilaya ya Ikungi, Hussein Mseule] kushoto } na Katibu wake Maxwell Ngwallo|\} kulia } wakitafakari namna watakavyopata fedha za kongamano hilo.
Afisa Ustawi wa Jamii wa wilaya ya Ikungi, Robby Muhochi (kulia ) akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Kongamano la Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Mkoa wa Singida.
Mwenyekiti wa Smaujata Wilaya ya Ikungi, Hussein Mseule, akizungumza kwenye kikao hicho.
Wajumbe wa kamati hiyo wakiomba dua.
Wajumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Kongamano la Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Mkoa wa Singida wakiwa katika picha ya pamoja na Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Ikungi Robby Muhochi ]wa tatu mbele kutoka kushoto. }baada ya kumtembelea ofisini kwake..
Toa Maoni Yako:
0 comments: