Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Francis Michael, akizungumza na watumishi wa Chuo Kikuu Mzumbe katika kikao kilichofanyika leo, Kampasi Kuu Morogoro.

Watumishi wa Chuo Kikuu Mzumbe wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Francis Michael, wakati wa kikao Kampasi kuu Morogoro.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Allen Mushi akitoa neon la Shukrani, katika kikao kilichofanyika leo, Kampasi kuu Morogoro.
Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, akimkaribisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kuzungumza na watumishi wa Chuo Kikuu Mzumbe.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Francis Michael, akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili leo, Chuo Kikuu Mzumbe, Kampasi Kuu Morogoro kwa ziara ya kikazi.
. Katibu Mkuu Dkt. Francis Michael (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe.
Katibu Mkuu akiwa ameambatana na Menejimenti ya Chuo, akitembelea miradi ya ujenzi wa Hosteli za wanafunzi na Kantini zilizokamilika.
---
Watumishi wa Chuo Kikuu Mzumbe, wameaswa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa zaidi ili kuendelea kuzalisha wataalamu wenye weledi wa kutosha katika fani zao ambao watakuwa tegemeo kubwa katika maendeleo ya Taifa kwa kutumia taaluma zao.Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Francis Michael, alipofanya ziara Makao Makuu wa Chuo hicho Morogoro, na kupata fursa ya kuzungumza na Watumishi.

Aidha, amewataka kutumia vema fursa mbalimbali za elimu zinazotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambayo imeendelea kuwekeza fedha nyingi katika Setka ya Elimu ikiwemo kuanzisha miradi ya vipaumbele ya maendeleo kwa vyuo Vikuu kupitia mradi wa Elimu ya Juu Kwa Mageuzi ya Kiuchumi ( HEET), kuongeza wigo wa elimu kwa wakufunzi kwa fani zote, ufadhili wa miradi ya Utafiti wa Kisayansi, kuongeza ufadhili wa wanafunzi hasa wa fani za Sayansi, pamoja na kujenga shule nyingi za msingi na Sekondari.

Amesisitiza wafanyakazi kufanya kazi kwa weledi, kwani Chuo Kikuu ni Kiwanda cha kutengeneza nguvu kazi ya Taifa, na hivyo wanataaluma hawana budi kuhakikisha wanatoa elimu inayokidhi viwango na mahitaji ya nchi na soko, ili Taifa liweze kusonga mbele.

“Serikali itaendelea kufanyia kazi kwa karibu stahili za watumishi kwa mujibu wa Sheria, sambamba na kuendelea kutunga sera, kupitia upya mitaala ya elimu na kuboresha miundombinu, itakayowezesha kufanikisha mipango ya Serikali ya kuinua ubora wa Elimu nchini” alisisitiza.

Kwa upande wao Watumishi waliopata fursa ya kutoa maoni wamempongeza na kumshukuru Katibu Mkuu kwa kufika chuoni hapo kuzungumza nao, kuwasikiliza na kuzichukua changamoto za kisekta kwa lengo la kwenda kuzishughulikia kwa haraka kwa ushirikiano na mamlaka husika. Aidha, wamemuomba Katibu Mkuu kuendeleza utaratibu wa kuzungumza na Watumishi, kwani kwa kufanya hivyo itasaidia kupunguza changamoto zilizopo katika utendaji pamoja na kuboresha sekta ya elimu kwa kuibua mawazo ya pamoja ya kuendeleza hiyo adhimu nchini.

Naye Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, aliahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Katibu Mkuu, sambamba na kuwahimiza Watumishi wenzake kuendelea kutekeleza miongozo inayoletwa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: