Na Said Mwishehe, Michuzi TV
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imekabidhi vifaa katika Kliniki ndogo kwa ajili ya kutoa matibabu kwa waraibu wa dawa za kulevya katika Gereza la Segerea Mkoa wa Dar es Salaam huku ikileza tatizo la dawa za kulevya bado kubwa nchini.
Akizungumza leo Novemba 19,2021Kamishna Generali wa Mamlaka hiyo Gerald Kusaya wakati wa kukabidhi vifaa katika Kliniki hiyo ndoa ya kutibu waraibu wa dawa za kulevya wakiwemo wafungwa,mahabusu pamoja na raia amesema kliniki hiyo itatoa huduma za matibabu kila siku kwa waraibu.
"Tunaatambua umuhimu wa kutoa matibabu ya Methadon kwa waraibu wa dawa za kulevya, kliniki hii ndogo ambayo leo tumekuja kukabidhi vifaa na dawa za methadon ni kwa ajili kuwahudumia waraibu.
"Watumiaji dawa za kulevya kwetu Mamlaka tunamuona ni mgonjwa na anastahili kupata matibabu na ndio maana tumeanzisha kliniki katika Gereza la Segerea na kliniki za aina hii kwa Dar es Salaam zitakuwa nne,"amesema Kusaya.
Amefafanua wameanzisha kliniki ndogo nne katika Mkoa wa Dar es Salaam ikiwemo iliyopo Gereza la Segera ni kwa ajili ya kupunguza msongamano Dar es Salaam ambayo ina Kliniki kubwa tatu bado msongamano ni mkubwa sana, lakini katika maeneo kengine nako waraibu ni wengi.
"Waraibu wa dawa za kulevya waliopo nchini hadi leo hii asubuhi wapo 16000 na wote hao wanaendelea kupata dawa ya Methadon kila siku .Watoa huduma wanachoka kutokana na msongamano,hivyo nisisitize kliniki hizi ndogo zitasaidia kupunguza msongamano.
"Tumeanza na Mkoa wa Dar es Salaam na kadri muda utakavyoruhusu na tukawa na rasilimali tutafungua kliniki hizi ndogo katika mikoa mbalimbali,ifahamike tunayo majukumu manne na moja ya majukumu hayo ni kupunguza uingiaji wa dawa, tunadhibiti dawa zinazotoka nje zisingie nchini.
"Jukumu lingine ni kupunguza uhitaji wa dawa na hapa tunatumia njia ya kutoa elimu ili watu waache kutumia dawa.Lakini kupunguza madhara yanayotokana na dawa za kulevya, hivyo mamlaka ikimkuta mtu anatumia bangi kwetu huyo ni mgonjwa, anatakiwa kusaidiwa kuacha,"amesema
Ameongeza Mamlaka wanaendelea na jukumu la kupunguza madhara na njia mojawapo ni kutoa dawa tiba ya Methadon inayomuwezesha mraibu kuacha "Ndio maana leo tumekutana kwa ajili ya kukabidhi vifaa, na Segerea ni eneo ambalo limekaa vizuri, watakaohudumiwa ni wafungwa,mahabusu na raia, wale walioko maene jirani."
Kamishna Jenerali Kusaya amesema wanawahudumia wafungwa na mahabusu ambao wana uraibu ili wawe na afya njema na hatimaye kulitumikia Taifa licha ya kuwa magerezani
Kuhusu tatizo la dawa za kulevya nchini amesema bado kubwa,watu wanaotumia dawa aina ya heroin wapo 500,000 na hapo hawajajumuisha wanaovuta bangi ambao bi wengi."Mamlaka inaomba ushirikiano, na wale wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya waache, anayejihusisha na dawa za kulevya atapatikana tu.
"Anayejihusisha na biashara ajue kuna kifungo cha maisha jela, tutaendelea kuwakamata kokote walioko, usiku na mchana tunafanya kazi, tunaomba taarifa ambazo zitatusaidia kufanikisha mapambano haya, tatizo hili linamgusa kila mtu."
Kuhusu vifaa walivyokabidhi, Kamishna Jenerali Kusaya amesema wamekabidhi Kasiki(Self) kwa ajili ya kuhifadhia dawa, hizo dawa ni mali na global fund wamekuwa wakisaidia kwa sehemu kubwa katika mapambano na ndio wamesaidia vifaa hivyo na mambo mengine.
"Kasiki( self) huwa inatunza pesa lakini hapa inatunza dawa za Methadon kwani zikitumika vibaya inaweza kuwa kama dawa za kulevya,tumekabidhi mashine ya kutoa Kopi,mashine ya kuprinti, kitanda cha kumhudumia mgonjwa,sindano, vikombe,vifaa vya kupima presha,kifaa cha kupima mkojo, kifaa cha kupima kileo,Methadon pamoja na dawa za kupunguza dozi,"amesema.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza Focus Ntakambi amesema amefurahishwa na uwepo wa huduma hiyo karibu kwani baadhi ya mahabusu na wafungwa wamekuwa na uraibu wa dawa za kulevya,hivyo kituo hicho kinakwenda kutatua changamoto ya kukosekana kwa matibabu kwa waraibu.
Wakati huo huo Daktari Mfawidhi wa Hospitali Kuu ya Magereza ambaye pia ni Mratibu wa Mradi wa utoaji huduma ya tiba ya Methadon Dk.Abdilatifu Mkingule amesema wamefarijika kupata kliniki hiyo kwani wameisubiria kwa muda mrefu.
"Katika nchi yetu kuna magereza 129 lakini 10 ndio yanahitaji huduma hiyo,hivyo tunatamani Mamlaka baadae waende magereza mengine na kliniki hii ndio ya kwanza kwa magereza.Tunachangamoto katika kutoa huduma, kuna muongozo wa kitaifa na muongozo wa magereza.
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Gerald Kusaya( kushoto) akikabidhi moja vifaa vitakavyotumika katika Kliniki ndogo ya kutoa tiba ya Methadon kwa Waraibu wa dawa za kulevya kwa Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Dar es Salaam Focus Ntakambi.
Toa Maoni Yako:
0 comments: