Katibu Mkuu wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi amewaasa Wafanyakazi wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) kufanya kazi kwa weledi ili kupata mafanikio zaidi katika Kampuni hiyo na nchi.
Amesema TSN ni Kampuni ya Serikali inayoaminika hivyo watumishi wanapaswa kufanya kazi kwa weledi ili kuendelea kutoa taarifa zenye ubora zinazozingatia Misingi ya Taaluma ya Uandishi wa Habari.
Amewashukuru wafanyakazi hao kwa kuendelea kutoa ushirikiano kabla na baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kushika tena wadhifa huo hivi karibuni.
“Asanteni kwa ushirikiano mliouonesha kwangu kipindi nina kofia ya Msemaji Mkuu wa Serikali hadi sasa nimeenda kuwa Katibu Mkuu, hamkuchoka na tulifanya kazi usiku na mchana, tuendelee kushirikiana bila kuchoka, ili kukidhi matarajio ya Rais wetu na wananchi kwa ujumla” amesisitiza Dkt. Abbasi.
Akiwa katika ziara hiyo, pia ameitaka Menejimenti ya TSN kujali maslahi ya wafanyakazi wote ili kuleta ufanisi wenye tija.
Naye Kaimu Mhariri Mtendaji wa Kampuni hiyo Bibi. Tuma Abdallah amempongeza Katibu Mkuu huyo kwa kuaminiwa tena katika nafasi hiyo na kuahidi kumpa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake.
Hii ni ziara ya kwanza ya kikazi aliyoifanya Katibu Mkuu, Dkt. Abbasi mara baada ya kuteuliwa tena hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Samia Suluhu Hassan kushika nafasi hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments: