Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Hoja Mahiba akizungumza wakati wa kufungua kikao cha kujadili matokeo yaliyopatikana kutokana na utafiti mdogo uliofanywa na Shirika la Kivulini kuhusu upatikanaji wa haki kwa wahanga wa ukatili dhidi ya wanawake na watoto wilaya ya Shinyanga leo Jumanne Desemba 3,2019 katika ukumbi wa zamani wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Hoja Mahiba alilishukuru shirika la Kivulini kwa kufanya utafiti kwenye halmashauri hiyo huku akibainisha kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia hususani kwa watoto bado ni kubwa katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.Alisema ili kukomesha vitendo hivyo ni jukumu la kila mmoja kushiriki kupiga vitendo vitendo vya ukatili katika jamii.
Afisa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka Shirika la Kivulini,Godfrey Paschal akiwasilisha taarifa matokeo yaliyopatikana kutokana na utafiti mdogo uliofanywa na Shirika la Kivulini kuhusu upatikanaji wa haki kwa wahanga wa ukatili dhidi ya wanawake na watoto wilaya ya Shinyanga. Alisema wamefanya utafiti katika kata tatu za halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ambazo ni Nsalala,Nyida na Itwangi na kwa upande wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu,utafiti umefanyika katika kata za Kishapu,Talaga,Lagana,Uchunga,Ukenyenge na Shagihilu.
Afisa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka Shirika la Kivulini,Godfrey Paschal alisema Kivulini ilifanya utafiti mdogo kwa wanajamii na watoa huduma mbalimbali kujua kwanini wahanga wengi wa ukatili hawatoi taarifa pale wanapofanyiwa ukatili na kuna changamoto gani zinawakumba ambapo baadhi ya matokeo yaliyopatikana ni Wanajamii wengi wanapenda kutoa taarifa za matukio ya ukatili wa kijinsia kwa wenyeviti wa vitongoji wenyeviti wa vijiji na wanamabadiliko kuliko kwa watoa huduma wengine.Pia ujuzi na uwezo wa wenyeviti wa vitongoji na vijiji wa kusuluhisha kesi ni mdogo sana.Godfrey Paschal pia alieleza kuwa kuahirishwa kwa kesi mara kwa mara mahakamani, wakati wananchi wanatumia rasilimali zao nyingi kwenda kwenye kesi mara kwa mara na Polisi kuchukua muda mrefu kufanya uchunguzi/upelelezi kwenye kesi hususani kesi za mimba mpaka mtuhumiwa wa kesi anakimbia imekuwa ni changamoto kubwa.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Hoja Mahiba akiongoza mjadala namna ya kumaliza vitendo vya ukatili wa kijinsia hususani matukio ya mimba na ndoa za utotoni.
Afisa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka Shirika la Kivulini,Godfrey Paschal akichokoza mada wakati wa mjadala namna ya kumaliza vitendo vya ukatili wa kijinsia hususani matukio ya mimba na ndoa za utotoni.
Mratibu wa Mradi wa Kusaidia Utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Kuzuia Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto mkoa wa Shinyanga, unaotekelezwa na Shirika lisilo la kiserikali la Women Fund Tanzania (WFT), Glory Mbia akichangia hoja wakati wa mjadala wa namna ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Makamu Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, ambaye ni diwani wa kata ya Iselamagazi, Isack Sengerema akichangia hoja wakati wa mjadala wa namna ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia ambapo alipendekeza wanafunzi wanaopewa mimba nao washughulikiwe badala ya kuwafunga jela wanaume wanaowapa mimba wanafunzi pekee.
Mwakilishi wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Claude Kanyorota kutoka kitengo cha polisi na Jamii alishauri wenyeviti wa serikali za mitaa wapewe elimu ya kuhamasisha kuelekeza wananchi kupeleka kesi za ubakaji kwenye vyombo vya dola.Aliwasisitiza wananchi kutoa taarifa pindi wanapobaini kuwepo kwa dalili ama vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Diwani wa kata ya Nyida,Seleman Segeleti akichangia hoja wakati wa mjadala wa namna ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Mchungaji Ibrahim Robert kutoka kanisa la CCT Shilabela kata ya Pandagichiza akichangia hoja wakati wa mjadala wa namna ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Diwani wa kata ya Itwangi Sonya Mhela akichangia hoja wakati wa mjadala wa namna ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Mwakilishi wa BAKWATA Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Hemed Rashid akichangia hoja wakati wa mjadala wa namna ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Mzee wa mila kutoka kijiji cha Welezo kata ya Nsalala ,Kapaya Sosoma akiwasisitiza Wasukuma kuacha tabia ya uoga kupeleka kwenye vyombo vya dola kesi zinazohusu matukio ya ukatili wa Kijinsia.
Afisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa Shinyanga Ngwale Tedson akichangia hoja wakati wa mjadala wa namna ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Afisa Ustawi wa Jamii halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Elizabeth Mweyo akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) katika halmashauri hiyo.
Mkaguzi Msaidizi wa Polisi kutoka Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Shinyanga,Victoria Maro akitoa taarifa ya Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Shinyanga juu ya matukio ya ukatili wa kijinsia. Alisema makosa yanayoripotiwa mara kwa mara katika ofisi za dawati ni kubaka,kulawiti,kutelekeza familia na mashambulio.
Afisa Elimu kata ya Nyida,Martin Kingu akiwasilisha taarifa ya matukio ya ukatili wa kijinsia ikiwemo mimba za wanafunzi kwenye kata ya Nyida.
Afisa Elimu kata ya Nsalala,Ilioza Kakusa akiwasilisha taarifa ya matukio ya ukatili wa kijinsia ikiwemo mimba za wanafunzi kwenye kata ya Nsalala.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog.
Imeelezwa kuwa kuahirishwa kwa kesi za ukatili wa kijinsia hususani mimba za utotoni mara kwa mara mahakamani na idadi ndogo ya kesi zilizofika mahakamani na kufanikiwa imewafanya wananchi waone hakuna haja ya kupeleka kesi kwa vyombo vya sheria matokeo yake matukio ya ukatili kuendelea kuwepo katika jamii.
Hayo yamesemwa na Afisa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka Shirika la Kivulini,Godfrey Paschal leo Jumatatu Desemba 3,2019 kwenye kikao cha wadau wakati akiwasilisha taarifa matokeo yaliyopatikana kutokana na utafiti mdogo uliofanywa na Shirika la Kivulini kuhusu upatikanaji wa haki kwa wahanga wa ukatili dhidi ya wanawake na watoto wilaya ya Shinyanga ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia.
Alisema kutokana na utafiti mdogo walioufanya katika wilaya ya Shinyanga na Kishapu wamebaini kuwa changamoto hizo zinazopatikana mahakamani zinawafanya wananchi wakati tamaa wakati wanatumia rasilimali zao nyingi kwenda kwenye kesi mara kwa mara ambazo mwisho wake hauwanufaishi.
Alisema kitendo cha Polisi kuchukua muda mrefu kufanya uchunguzi/upelelezi kwenye kesi hususani kesi za mimba za utotoni mpaka mtuhumiwa wa kesi anakimbia bado ni changamoto.
“Tumebaini pia kuwa Wanawake wengi hawatoi taarifa kwa sababu ya kuogopa kuachwa na mume wake na kuwaacha watoto wake wakiteseka lakini pia kwa taratibu na utamaduni wa wasukuma hawapendi kutoa taarifa/ kumshtaki mume kwa watoa huduma kama Maafisa ustawi, polisi, na mahakama, badala yake wanataka kesi iishie ngazi ya familia tu”,alieleza Paschal.
Paschal alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi kutoa taarifa za matukio ya ukatili wa kijinsia kutokana na kwamba wanajamii wengi wamekuwa wakitoa taarifa tu pale wanaposhindwa kuelewana wao kwa wao hususani kwenye kesi za mimba.
Aidha alisema pamoja na kuwepo ongezeko la kuripotiwa kwa kesi lakini bado kesi nyingi za mimba za utotoni haziripotiwi.
Afisa huyo wa aliwataka wadau kwa kushirikiana na serikali kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kutoa taarifa mapema ndani ya masaa 72 na kuacha kumaliza kesi nyingi na kutengeneza sheria ndogo ndogo zitakazo wasaidia wanajamii watoe taarifa mapema au kuacha ukatili kabisa.
Kwa upande wake mgeni rasmi katika kikao hicho,Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Hoja Mahiba alisema ukatili dhidi ya wanawake na watoto bado lipo katika halmashauri yake hivyo kuwataka wadau na jamii kwa ujumla kushiriki kutokomeza vitendo hivyo.
“Nawapongeza Kivulini kwa kufanya utafiti huu. Naomba kila mmoja ashiriki kwa nafasi yake katika kupiga vita ukatili wa kijinsia.Kila mtu ana familia yake,asimame katika nafasi yake ili jamii iwe salama kwani vitendo vya ukatili vinaathiri maendeleo ya taifa”,alisema Mahiba.
Kikao hicho cha kuwasilisha taarifa matokeo yaliyopatikana kutokana na utafiti mdogo uliofanywa na Shirika la Kivulini kuhusu upatikanaji wa haki kwa wahanga wa ukatili dhidi ya wanawake na watoto wilaya ya Shinyanga umefanyika katika ukumbi wa zamani wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa haki za wanawake na watoto.
Washiriki wa kikao hicho wametumia fursa hiyo kujadili mikakati mbalimbali ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia huku washiriki wakisisitiza zaidi suala la elimu kwa wananchi kuachana na vitendo vya ukatili na kutunga sheria ndogo ili kukomesha ukatili katika jamii.
Toa Maoni Yako:
0 comments: