MWENYEKITI Mtendaji wa IPP Dkt. Reginald Mengi (pichani) amefariki dunia usiku wa kumakia leo Mei 2, 2019, akiwa na umri wa miaka 76.
Taarifa zinasema Dkt. Mengi amefariki dunia akiwa Dubai Falme za Kiarabu.
Hata hivyo taarifa hiyo iliyotangazwa na Radio One Sterio ambayo IPP inaimiliki haikutoa ufafanuzi zaidi kuhusu chanzo cha kifo chake.
Dkt. Reginald Abraham Mengi alizaliwa Wilayani Hai, Tarafa ya Machame Mkoani Kilimanjaro ambapo mara nyingi alikaririwa akisema amezaliwa kwenye familia masikini akichangia chumba anacholalal na mifugo mingine kama mbuzi.
Lakini pamoja na kuwa kwenye mazingira kama hayo, Dkt. Mengi hakukata tama na ndoto yake ya kufanikiwa kimaisha ilimpelekea kusoma kwa bidii ambapo alifanikiwa kusomea masuala ya uhasibu nchini Uingereza na baada ya kufanikiwa kumaliza masomo yake alirejea nyumbani mnamo mwaka 1971 na kuajiriwa na Kampuni ya Uhasibu na Ukaguzi wa mahesabu ya Coopers & Lybrand Tanzania (kwa sasa inajulikana kama PriceWaterHouseCoopers) hadi Septemba 1989 na katika kipindi hicho alichaguliwa kuwa mwenyekiti na Kiongozi mwenza.
Mnamo Oktoba 1989 Dtk. Mengi aliondoka Coopers & Lybrand Tanzania na kujielekeza kwenye biashara zake binafsi na kuanzisha IPP Limited, ambayo ikuja kuwa kampuni kubwa kabisa ya kibinafsi nchini Tanzania.
Biashara ambazo Watanzania wa kawaida walizifahamu, ni pamoja na kumiliki vyombo vya habari mashuhuri kabisa hapa nchini ITV/Radio One, Kampuni ya magazeti ya The Guardian Limited, Kampuni ya kuzalisha vinywaji baridi ya Bonite, lakini pia Dkt. Mengi chini ya kampuni yake ya IPP alikuwa akifanya biashara mbalimbali na hivi karibuni alisaini kandarasi ya kuanzisha kiwanda cha kutengeneza magari hapa hapa nchini, lakni pia kiwanda cha kutengeneza madawa ya binadamu na vingine vingi.
Toa Maoni Yako:
0 comments: