Ni siku ya Jumanne ya Februari 26, 2019 majira ya saa mbili na robo nikiwa naendesha gari kurudi nyumbani Madale! Kupitia mitandao ya kijamii naona uzi kwamba ndugu yangu Ruge ametangulia mbele ya haki! Moyo wa binadamu umeumbwa kwa kuogopa taarifa mbaya hasa za kifo tena cha mtu mnayefahamiana.

Nikiwa kwenye mshtuko na mtanziko huo, ghafla kwenye simu yangu unaigia ujumbe wa Mfalme! Ujumbe ambao unathibitisha kifo, safari hii si kupitia taarifa za Gerson Msigwa isipokuwa kupitia kwenye ukurasa wa twitter ya Mheshimiwa Rais, Dk John Magufuli. Kwa kweli umemwelezea Ruge vizuri zaidi!

Ujumbe huo ukanikumbusha thamani ya kila mwanadamu awapo duniani na baada ya kuondoka, utakumbukwa kwa jambo gani? baya ama zuri? Nikakumbuka tena kwamba Ruge hajafa isipokuwa amelala tu! Maana ameacha alama (icon) na benchmark nyingi ambazo kupitia hizo namwona akiendelea kuishi.

Jina Ruge katika tasnia ya burudani pamoja na mambo mengine ya kijamii ni sawa na maji! Usipoyanywa basi utayaoga, kama ikishindikana kuyaoga basi hata chooni utachambia. Ruge ulikuwa zawadi kwa familia na ukoo wa Mutahaba, kwa tasnia ya habari ulikuwa nguzo na katika tasnia ya burudani, ulikuwa funguo!
Tazama zawadi imepotea na nguzo imeanguka, lakini funguo imebaki! Kupitia kwako Ruge umewafungulia vijana wengi dunia kuwa wanachotaka! Bila ufunguo wako pengine leo vijana wengi wangekuwa kama kipofu asiyekuwa na fimbo nyeupe! Changamoto zingekuwa nyingi zaidi, lakini tazama leo umelala usingizi mzito lakini ufunguo umetuachia vijana, kikubwa ni kuutumia vizuri ili isije kutulazimu kubadili kitasa.

Kaka Ruge umeondoka, mdogo wako umeniachia funzo moja kubwa, roho ya kusamehe. Katika maisha yako hukuruhusu chuki na ugomvi vikutawale, hata pale vilipotokea ulihakikisha vinakwisha na maisha mengine yasonge mbele! Ninakumbuka siku Rais anazindua mradi wa bomba la mafuta kutoka Tanga hadi Hoima, Uganda. Pale ulitoa funzo kubwa kama lile alilolitoa Yesu Kristu akiwa amewambwa msalabani pamoja na wale wanyang'anyi wawili!

Rais alitaka Ruge usameheane na Gavana wa Darisalama, bila kinyongo tena kwa sura ya tabasamu ukaonesha kukubali na kuishi kile ulichokiamini. Sitaki kuzungumzia suala la ugomvi uliokuwapo baina yako na Mbunge wa sasa wa Mbeya Mjini, baadaye mkashikana mikono na maisha yakaendelea! Moyo wa aina hiyo unapatikana vifuani mwa wanadamu wachache ambao mmoja wao ni Ruge.

Ninasikitika ninaandika mambo yanayokuhusu wakati hutapata fursa ya kuyasikia, lakini nafarijika kwamba kupitia mafunzo hayo machache kutoka kwako wachache miongoni mwetu tunaweza kujifunza kuwa kama Ruge.

Pumzika kwa amani emanzi eya' Buhaya ninaendelea kuamini kwamba Mwenyezi Mungu amekuchukua baada ya kumaliza kazi ambayo alikutuma uje kuifanya hapa duniani! Amekuita ukafanye kazi nyingine huko mbinguni.

Omukama akuhumuze ne'milembe Amina.

Imeandikwa na Mkinga Mkinga.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: