Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Azza Hilal Hamad (CCM) amekabidhi msaada wa Vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 36.5 kwa ajili ya vituo vya afya na zahanati sita zilizopo katika halmashauri ya wilaya ya Ushetu,Msalala na Kahama Mji wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Mheshimiwa Azza amekabidhi vifaa tiba hivyo leo Jumanne Oktoba 16,2018 kwa Mkuu wa Wilaya ya Kahama,Anamringi Macha wakati wa Kikao cha Baraza la UWT wilaya ya Kahama uliofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Kahama.

Vifaa tiba hivyo ni pamoja na shuka 100,mashine za kupima damu,wingi wa damu,sukari,joto,mapigo ya moyo na vifaa vya kusaidia kujifungua kwa akina mama ambavyo kupatikana kwake kumetokana na jitihada za mbunge huyo kuhakikisha vifo vya mama na mtoto vinapungua mkoani Shinyanga.

Awali akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa tiba hivyo,Mheshimiwa Azza Hilal alisema kupitia Kampeni yake ya ‘Afya Yangu Mtaji Wangu’ na kuwajali akina mama aliamua kutafuta wadau kwa ajili ya kusaidia kumaliza changamoto ya uhaba wa vifaa tiba katika vituo vya afya na zahanati.

“Nawashukuru sana Bahari Pharmacy Ltd na Brett &Beileys kwa kunishika mkono na kuchangia kupatikana kwa vifaa hivi ambavyo leo navikabidhi ili vikatumike kwenye zahanati na vituo vya afya kwani hatutaki kuona vifo vya mama na mtoto”,alieleza Azza.

“Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Jemedari,Dkt. John Pombe Magufuli imedhamiria kuboresha huduma za afya,na tutaendelea kushirikana ili kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya bora ili washikiriki katika shughuli za uchumi”,aliongeza.

Alivitaja vituo vya afya vitakavyonufaika na msaada huo kuwa ni Mwendakulima,Mbika na Lunguya na zanahati ambazo ni Ngogwe,Kisuke na Bulige.

Akipokea vifaa tiba,Mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha alimshukuru mbunge huyo kwa msaada huo na kubainisha kuwa ameunga mkono kwa vitendo ilani ya CCM na juhudi zinazofanywa na Rais Magufuli katika kuboresha sekta ya afya.

“Nikupongeze sana kwani umetumia cheo chako kwa faida ya wote badala ya kujinufaisha wewe mwenyewe,lakini nikushukuru pia kwa kuendelea kujitoa kwa hali na mali katika kukitumikia chama na wananchi,umekuwa kiungo mzuri sana”,alisema Macha.

Kwa Upande wake Mbunge wa Jimbo la Ushetu,Mheshimiwa Elias Kwandikwa ambaye ni Naibu Waziri wa Ujenzi aliahidi kumuunga mkono mheshimiwa Azza kwa kutoa msaada wa vifaa tiba katika vituo vitatu vya afya wilayani Kahama.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: