Na Said Mwishehe, Globu ya Jamii.
SHIKAMOO Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli.
Pia naomba kutumia nafasi hii kutoa pole nyingi kwako kutokana na msiba wa kuondokewa na dada yako mpendwa Monica Magufuli.
Pole Rais wangu, pole familia ya Rais, ndugu, jamaa na marafiki. Mungu aiweke roho ya mpendwa wetu mahala pema peponi. Amina.
Baada ya utangulizi huo naomba niseme jambo kidogo. Nilishiriki uchaguzi Mkuu mwaka 2015 na kura yangu ya Urais nilikuchagua wewe.
Nikiri sikukosea kwa uamuzi wa kura yangu kukupa wewe uwe Rais wangu. Sijakosea na nashukuru Mungu alinipa utulivu wa kuchagua Rais sahihi kwa ajili ya maisha ya Watanzania wote.
Rais wangu mpendwa nimekuwa nikifuatilia utendaji wako wa kazi, nimekuwa nikifuatilia maagizo yako kwa walio chini yako. Kubwa zaidi nimekuwa nikifuatilia hotuba zako mbalimbali.
Naomba nikiri Rais wangu hotuba yako ambayo umeizungumza wilayani Chato imenigusa mno. Najua umetoa hotuba kadhaa ukiwa Chato lakini naomba nikukumbushe naizungumzia hii hotuba yako ya kuhusu makontena ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Hotuba yako imethibitisha namna ambavyo unaamini katika kusimamia misingi ya utawala wa sheria.
Najua namna ambavyo umewakosha wengi. Umewakosha si kwa sababu wanamchukia au wanampenda sana Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, bali ni kwa kuonesha unavyosimamia sheria.
Ujue Rais wangu huku mtaani ninakoishi kuna mengi yamekuwa yakizungumzwa. Wapo wanaosema unampenda sana Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na kwa sababu unampenda basi hata akikosea huwezi kumchukulia hatua.
Si mimi ninayesema, ila huku mtaani ndio wanavyosema hivyo. Ukweli ni kwamba mtaani kuna maneno maneno mengi yanazungumzwa hasa tukiwa kwenye vijiwe vya kahawa. Basi bwana watu wanazungumza lakini wakifika kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam utasikia wakisema “Huyooo RC wa Dar anapendwa sana. Hawezi kuchukuliwa hatua.”
Basi watasema maneno mengi na wengine wanakumbusha matukio mengi mengi. Kwa kuwa maneno ya kijiweni huwa yanaishia huko huko kijiweni. Anayezungumza sana ndio anaonekana mshindi. Haya ya mtaani yasikupe tabu tuachie sie wa mtaani ndio maisha yetu.
Binafsi nimekuwa na tabia ya kukaa kimya hasa kwenye mambo yanayohusu viongozi wangu, huwa naogopa kusema maana naweza kuambiwa sina adabu.
Nimekuwa muumini wa kuheshimu, kuthamini na kutambua mamlaka zilizopo pamoja na wale ambao umewapa dhamana ya kutusimamia.
Leo naomba nivunje mwiko wa kuzungumza japo kidogo. Iko hivi, Rais wangu hotuba yako kuhusu makontena ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam nimeisikiliza na kuichambua kwa kina.
Naomba nieleweke nimeichambua kwa kiwango cha uwezo wangu wa kufikiri na kuchambua mambo, usinielewe vibaya huenda nachangia ujinga lakini bora niuseme niwe huru.
Baada ya kukusikiliza cha kwanza ambacho kimenijia akilini nilisema kimoyo moyo hakika huyu ndio Rais ambaye Watanzania tunamuhitaji.
Pia nikasema nimeamini Rais wangu anasimama katika sheria katika kuzungumzia jambo lolote, hili la makontena umelizungumza kwa misingi ya kisheria.
Wakati naendelea kutafakari kuhusu hotuba yako pia nikabaini huna rafiki wala adui wa kudumu, kwako unaangalia sheria inataka nini katika kuzungumzia jambo. Hongera Rais Magufuli.
Binafsi nimekuwa nikifuatilia kwa karibu suala la makontena ya Makonda ambayo ndani yake yana samani kwa ajili ya walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Ndivyo tunavyoambiwa.
Kwa bahati mbaya baada ya makontena hayo kutangazwa kuwa yatapigwa mnada Makonda kwa mara kadhaa amezungumza.
Mazungumzo yake kwa sehemu kubwa yalionesha hana shaka, hata kama kuna watu akiwamo Waziri wa Fedha Dk. Philip Mpango wanataka kukwamisha makontena hayo yasitoke atakwambia wewe (Rais).
Sina hakika kama tayari alishakwambia kuhusu kuzuiliwa kwa makontena hayo.
Pia mwishoni mwa wiki iliyopita Makonda akiwa wilayani Ngara mkoani Kagera akiwa kanisani akaamua kuzungumzia tena suala la kuzuiliwa kwa makontena hayo.
Akaenda mbali zaidi kwa kusema kuwa atakayenunua Mungu atamlaani ni kauli ya vitisho ambayo ameitoa kwa Waziri Mpango.
Hata hivyo, Waziri Mpango naye Jumatatu ya wiki hii akaamua kutoa msimamo wake, akasema lazima makontena hayo yalipiwe kodi, kinyume na hapo yapigwe mnada akaenda mbali zaidi kwa kusema hatakuwa tayari kuona sheria za kodi zinachezewa. Hakusita kutoa la moyoni kuwa iwapo atashindwa kusimamia hilo atajipima.
Sijui Dk. Mpango, alikuwa anamaanisha nini lakini nadhani alikuwa tayari kukaa kando iwapo makontena hayo yataruhusiwa kutoka bandarini bila kulipiwa kodi.
Ahsante Rais Magufuli, kwa sababu umesimama katika kweli, kwa hotuba yako ya jana kuhusu makontena hayo maana yake umefunga rasmi mjadala.
Makonda anatakiwa kulipa kodi ili mambo mengine yaendelee.
Nikiri sina chuki na Mkuu wangu wa Mkoa wa Dar es Salaam, pia nikiri sina urafiki naye, bali nikiri ndio Mkuu wangu wa Mkoa na naheshimu na kuthamini nafasi yake, navutiwa na utendaji wake.
Hata hivyo, kabla ya kusikia kauli yako Rais wangu nilikuwa najiongelesha kimoyo moyo kwamba Makonda hakustahili kutumia nguvu nyingi kupambania makontena hayo yatoke bila kulipiwa kodi.
Nikakumbuka ule usemi unaosema hivi: “Mdomo ulimponza kichwa.” Hata hivyo, sikuwa na mahali pakusemea, ila hotuba yako imenipa nguvu na ndio maana napata uthubutu wa kusema.
Najua niko salama maana si dhambi kutoa maoni yangu.
Nilikuwa nawaza iwapo makontena hayo yataruhusiwa yatoke bila kulipiwa kodi. Itakuwaje ikitokea na wakuu wa mikoa wengine wakaanza kuagiza makontena kwa ajili ya wananchi wao na kisha wakataka yasilipiwe kodi?
Kwa mtu wa aina yangu huwa tunawaza na kuacha tu mambo yapite. Hata ukisema nani anakusikia? Hata ukishauri nani anakusikiliza? Je baada ya kupaza sauti yako nani ataifanyia kazi?
Basi nikawa najiuliza maswali mengi bila majibu.
Nikwambie Rais wangu Magufuli, umejibu maswali mengi ambayo nilikuwa najiuliza kimya kimya moyoni. Umethibitisha kumbe unaweza kuyajibu hata yale ambayo tumeamua kukaa kimya.
Wewe ni Rais bora kwa Taifa la Tanzania. Wakati wa kampeni zako za kuwania urais nikiri nilipata bahati ya kuzunguka kwenye kampeni zako katika mikoa karibu yote, sikubahatika kuwa katika Mkoa wa Kigoma, Mbeya na Iringa, lakini mikoa mingine yote nilishiriki.
Kupitia kazi yangu ya uandishi wa habari chombo changu cha habari (Jambo Leo) nilichaguliwa kuwa sehemu ya waandishi wa mgombe urais wa CCM (Ni wewe Rais Magufuli).
Nikwambie tu sijuti kuwa sehemu ya waandishi waliokuwa wanaandika kila unachosema na kukifanya wakati wa kampeni zako.
Matunda ya jua, vumbi, mvua, kutokula mchana, kulala usiku wa manane kwa ajili ya kuhakikisha natimiza majukumu yangu kuhakikisha Watanzania wanakuchagua nilikuwa nafanya kazi sahihi.
Kwa kweli leo umenifurahisha. Si kwa sababu nataka kuona unachukua hatua zaidi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Hapana umenifurahisha kwa sababu umethibitisha kwako sheria ni msumeno na unakata kote kote.
Umetimiza wajibu wako Rais wangu katika kulizungumzia hili la makontena ya Makonda. Nadhani wenye jukumu la kusimamia kodi inapatikana kutoka kwenye makontena hayo wanatekeleza yale ambayo umeyasema. Nadhani wamekusikia.
Najua una mambo mengi ya kufanya na lengo la kuandika maelezo yoote haya marefu ni kutaka uyasome. Najua huenda nimeandika kwa kirefu lakini ujumbe wangu ukawa ni mdogo. Naomba uuchukue Rais wangu na huenda hata ukishindwa kunielewa kwa niliyoeleza basi naomba ushike hata hili la kwamba nakupongeza kwa namna ambavyo umelitolea ufafanuzi suala la makontena ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Pia nitoe ushauri kwa Makonda kwamba najua unao marafiki wengi. Nikwambie marafiki wanaokuzunguka baadhi yao wapo kwa ajili ya kukusifu na wengi wanaogopa kukwambia ukweli maana utachukia.
Makonda kwa kuwa marafiki zako wananufaika kwa kuwa karibu yako wanajua wakikwambia ukweli utawaweka kando. Hivyo, hata ukikosea wenyewe wanakusifu.
Sitaki kutaja orodha ya marafiki zako maana unawajua vizuri kuliko mimi. Wengine kwenye hili la makontena waliamua kusimama kidete kutoa maoni yao. Si kwa sababu hajui ukweli bali walikuwa wanafanya hivyo wakiamini wanakufurahisha. Ukweli baadhi ya marafiki zako wamechangia kukufikisha hapo ambapo umefika.
Hili la ushauri kwa Makonda wala halina maana kwa siku ya leo. Uliyesoma nilichoandika baki na kile ambacho nimemwambia Rais wangu. Ahsante Rais. Hata ukishindwa kusoma hiki ambacho nimekiandika naamini wasaidizi wako watakufikishia tu. Hata kwa kusema kuna mtu anaitwa Said Mwishehe amekupongeza.
Ndugu yangu Gerson Msigwa na Dk. Hassan Abbasi mkipata nafasi ya kusoma nilichoandika basi mfikishieni na Rais wangu. Nikisikia amesoma mwenyewe nitafurahi zaidi. Si unajua tena akina sie wenye maisha ya pangu pakavu tia mchuzi ukisema kuna jambo umelisema jema na Rais amelisikia unakenua meno yote 32 nje. Ahsante Rais Magufuli. Ahsante baba. Ahsante mkuu wa nchi. Tanzania ni yangu. Tanzania ni ya kwetu. Tanzania ni ya kila mtanzania.
Napokea maoni kwa 0713 833822.
Toa Maoni Yako:
0 comments: