Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Mhe Ali Hapi ametoa mwezi mmoja kufanyika operesheni kali ya kuondoa kuta, uzio na majengo yaliyojengwa kwenye hifadhi ya barabara za wilayani Kinondoni kinyume cha sheria ya barabara.
Hapi ametoa agizo hilo akielekeza zoezi hilo kuanzia Masaki, Oysterbay, Mikocheni na Msasani ambapo amewataka wahandisi wa manispaa ya Kinondoni na TARURA kukagua barabara zote na kuwapa notisi ya kubomoa wale wote waliojenga kuta, uzio na majengo kwenye hifadhi ya barabara na kuzuia watumiaji wengine wa barabara kupita na hata kupaki kwa dharura katika maeneo hayo kinyume cha sheria ya barabara ya mwaka 2007 na kanuni zake.
Aidha katika ziara hiyo Hapi amebaini baadhi ya majengo ya ghorofa yaliyojengwa na kuongezwa idadi ya ghorofa kinyume cha vibali vya ujenzi vilivyotolewa na manispaa hali inayoweza kuhatarisha usalama wa watu.
"Hatuwezi kuruhusu mtu akajenga kwenye road deserve na kuzuia wananchi wengine watumiao barabara. Wako watu wamejenga kuta, wameweka mageti na majengo ya kudumu katika hifadhi ya barabara kiasi ambacho hata watembea kwa miguu hawawezi kupita. Wengine wameweka mageti na walinzi wenye silaha.Hii haikubaliki."
Mkuu huyo wa wilaya amesema watu wote waliofanya hivyo wabomoe wenyewe vinginevyo watabomolewa na kulipia gharama za ubomoaji zitakazotumika.
"Natoa mwezi mmoja, kwa halmashauri pamoja na TARURA, muanze na maeneo ya Oysterbay, Masaki, Msasani na Mikocheni wanakoishi matajiri, mfanye operesheni kukagua barabara zote mkiwa na ramani na kubomoa maeneo hayo mara moja."
Aliagiza DC Hapi.
Aidha Hapi akielekeza majengo yote marefu yanayojengwa kukaguliwa na wahandisi ili kuona kama masharti yaliyotolewa kwenye vibali vyao yanafuatwa.
Toa Maoni Yako:
0 comments: