Serikali imesema kuwa watumishi wote wa Serikali Kuu walioajiriwa na kuthibitishwa katika ajira ya masharti ya kudumu na pensheni, kabla ya mwaka 1999 waliunganishwa katika Mfuko wa Pensheni wa PSPF kwa mujibu wa Sheria.
Hayo yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Lucy Mlowe aliyetaka kujua Serikali inawafikiriaje watumishi wa Sekta ya Afya walioajiriwa na Serikali Kuu miaka ya 1980 ambao fedha zao hazikukatwa na mfuko wa hifadhi ya jamii.
Dkt. Kijaji, alisema kuwa Kabla ya Julai 1999 mfumo wa malipo ya mafao ya kustaafu kwa watumishi wa Serikali Kuu haukuwa wa kuchangia hivyo watumishi wote waliokuwa kwenye ajira ya masharti ya kudumu wanastahili malipo ya uzeeni wakiwemo watumishi wa Sekta ya Afya hata bila kuchangia.
“Kwa mujibu wa Ibara ya 5 ya Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa PSPF, watumishi wote wa Serikali Kuu ambao waliajiriwa na kuthibitishwa katika ajira ya masharti ya kudumu na pensheni wanakuwa wanachama wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF kuanzia tarehe ya kuanzishwa kwa mfuko”, alisema Dkt. Kijaji.
Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mafao ya Hitimisho la Kazi Na. 2 ya mwaka 1999 kwa watumishi wa umma ambayo ilianzisha Mfuko wa Pensheni wa PSPF, wastaafu wote ambao ni wanachama wa Mfuko huo na wanaguswa na sheria hii wanalipwa mafao ya kustaafu na mfuko huo kwa kipindi chao chote cha utumishi.
Dkt. Kijaji alibainisha kuwa mafao ya watumishi yanakokotolewa kuanzia tarehe ya kuajiriwa hadi wanapostaafu utumishi wao kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma.
Toa Maoni Yako:
0 comments: