Juzi ya tarehe 29/05/18 mkongwe Juma Kassim Kiroboto a.k.a Sir Nature mwenye talanta na hii tasnia ya muziki wa almaarufu Bongo Flava kupitia kipindi cha XXL cha Clouds alitudondoshea nyimbo mbili kwa mpigo, moja ni Unayumba na nyingine ni Nadhani.

Kwenye wimbo wa Unayumba mie binafsi hajanishawishi sana ila kwenye huu wa Nadhani ndio umenigusa kiasi cha kutaka kuzungumza jambo. Kwenye wimbo wa Nadhani Nature amerudi kama Nature yule wa miaka ya 2000 mwanzoni; Nature wa Sonia, Kigetogeto, hili Game, CCM na CUF, Nini chanzo, Ugali, Sitaki demu, Inaniuma sana, Kisa demu, Mzee wa Busara, Jinsi kijana, Utajiju, Brother man pamoja na nyinginezo nyingi za miaka hiyo.

Nini nataka kusema? Ninachosema ni kwamba Nature amekataa kuwa mfu aliye hai ingali ana uwezo mkubwa wa kupumua. Nature amekataa kuyakubali maneno ya watu fulani fulani washika mpini wenye kusema Nature ameishiwa, kwa sasa hana lolote, mara ooh amepwaya sasa kupitia Nadhani anadhihirisha kuwa bado yuko hai.

Hii habari ya kuzikwa ukiwa hai sio ile ya pumzi kukata katika mwili ni ile dhana ya baadhi ya watu kuamua mstakabali wa ufanisi katika shughuli zako. Unaweza ukawa unauwezo mkubwa wa kutenda jambo ila watajitokeza watu watasema huna lolote na kupitia nguvu ya uongo wao na wengine wataamini kuwa huna lolote, hawa ndio Miungu watu.

Kwenye kiitikio cha wimbo wa Nadhani kinasema;

"Mi nadhani wanaosema nimekwisha wananichimbia kaburi kumbe mimi bado mzima".

Nature anaamini kuwa kuna watu wanataka kumzika akiwa hai pamoja na ukubwa wa kipaji chake, sasa kupitia Nadhani amegoma kufa anataka kwenda nao sambamba.

Kwenye wimbo wa SUMU wa FidQ ameizungumzia dhana ya kuzikwa ukiwa hai mwishoni mwa ubeti wa kwanza, mstari huo unasema hivi;

"Usipostuka Afrika unaweza kuzikwa ukiwa hai".

Hapa Fid Q anatuweka kwenye alama ya tahadhari ya kwamba usipokuwa makini kwa jamii zetu za kiafrika basi utapotezewa muda kama si kukiua kipaji chako. Kuna wasanii wenye vipaji vikubwa lakini leo hii hawasikiki tena sababu wamezikwa wakiwa 'HAI' na vipaji vyao.

Wenye mfumo wasipokuhitaji watatangaza umekufa yaani hauna uwezo tena ingali ukikutana nao kwenye ligi unaondoka na kijiji hiyo ndo nguvu ya mfumo ilivyo ambayo Nature ameistukia.

Tukirudi kwenye wimbo wa Nadhani kaka mkubwa Nature anatambua kwamba wenye nguvu ya kumzika hai mwenye kipaji ni wadau waliojivisha U-mungu mtu katika kuamua nani leo atoke na nani asitoke na kipi apate na kipi asipate sasa anawapa habari ya kwamba;

"Wanaojifanya Miungu watu wameumia". Mstari huu unapatikana mwishoni mwa ubeti wa pili.

Kwa kuonyesha kuwa Miungu watu ndio wanaoamua nini upate na kipi usipate, Joh Makini kwenye wimbo wake wa I see me kuna mistari inasikika kama hivi;

"Muziki una hela mwanzo unapoingia.., hela nyingi zipo mwishoni hutozifikia.., hapo kati kuna kisu, husu na jambia.., wale 'PAPA' (miungu watu) wabakaji mpira hawatotumia (hawatofuata haki)".

Tukirejea kwa mhusika mkuu Sir Nature kwa kuonyesha kuwa yeye ni mwamba na ni sehemu ya historia ya huu muziki mwishoni mwa ubeti wa pili anaendelea kuwapasha habari Miungu watu kuwa yeye ni jemedari na ni kiungo sahihi kwenye kunogesha hii tasnia ya muziki mithili ya kachumbari inavyoongeza chachu ya kula chakula. Kwenye ubeti wa pili anasema;

"We ukipenda niite kachumbari.., jemedari.., mkuu wa habari.., Nature halali natunga silali.., huu mchezo wa hatari.., zibua safari".

Nature anatuaminisha ya kwamba ile milango ambayo Miungu watu walijitahidi kuiziba sasa inazibuka upya na kuianza safari kwa mara nyingine.

Huyu ndiye Juma Nature mwenye talanta ya kipekee kwenye hii familia ya fasihi simulizi akiwa jukwaani sio tu nyimbo zake zinazoweza kuinua umati wa watu la hasha, Ila hata ile sauti yake tu na ule mtindo wake wa kucheza ni ishara tosha ya kukubali kuwa huyu ni NYOTA YA MCHEZO. Rambo amerudi tena.

#DeCheusiDawa
Hans Bukuku
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: