Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa kwenye mazungumzo na Bw. Chang Yaong Hun, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim ya Korea Kusini. Viongozi hao wawili walikutana kwenye ofisi za Benki hiyo Jijini Seoul Korea Kusini wakati wa ziara ya kikazi ya siku tatu ya Waziri Mahiga nchini humo.
Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa na ujumbe wake kwenye mazungumzo na Bw. Chang Yaong Hun, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim ya Korea Kusini. Viongozi hao wawili walikutana kwenye ofisi za Benki hiyo Jijini Seoul Korea Kusini.
Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa kwenye picha ya pamoja na Bw. Jundong Kim, Makamu Mwenyekiti wa Korea Chamber of Commerce and Industries (KCCI). Mwingine pichani ni Balozi wa Tanzania nchini Jamhuri ya Korea Mheshimiwa Matilda Masuka.
Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa na ujumbe wake kwenye mazungumzo na Bw. Jundong Kim, Makamu Mwenyekiti wa Korea Chamber of Commerce and Industries (KCCI).
Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akimkabidhi zawadi ya majani ya chain a kahawa za Tanzania Bw. Choi Jong-won, Makamu Mwenyekiti wa Kampuni ya Dong Myeong ya Korea Kusini.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Augustine Mahiga ameahidi kusimamia uimarishwaji wa uhusiano wa kiuchumi na biashara kati ya Tanzania na Korea Kusini ili wananchi wa pande zote mbili wapate manufaa.

Waziri Mahiga ameyasema hayo alipokuwa anahitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu ambapo siku ya mwisho aliitumia kikamilifu kukutana na taasisi za umma za biashara na viwanda, Benki ya Exim ya Korea pamoja na makampuni binafsi yanayojipanga kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania.

Amesema kuwa miaka 25 ya kwanza ya uhusiano wetu na Jamhuri ya Korea ilijikita kwenye kuweka misingi imara ya uhusiano wa kidiplomasia ambapo nchi zetu zilikuwa zinajiimarisha kama mataifa huru. “Sasa ni wakati wa kushamiri kiuchumi tuone sekta binafsi zinavyoshiriki katika kukuza uchumi, wananchi wa Tanzania waje kwa wingi nchini Korea kujifunza masuala ya teknolojia, uhandisi na hata usanifu na ubunifu. Huu ndio uhusiano wenye tija kwa mataifa yetu”. Mheshimiwa Waziri alisema.

Akizungumza na Bw. Chang Yaong Hun, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim ya Korea, Mheshimiwa Mahiga mbali na kuishukuru taasisi hiyo kwa kuendelea kutoa mikopo na misaada nchini Tanzania, Waziri Mahiga alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ya Mheshimiwa John Pombe Magufuli sasa imejikita kwenye mapambano dhidi ya rushwa na ujenzi wa viwanda ili kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi wetu. Kwasasa Benki hiyo inatekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu ya umeme na maji mikoa mbalimbali ya Tanzania ukiwemo Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mahiga alifafanua kuwa ajenda ya Mheshimiwa Magufuli ya viwanda, haiwezi kukamilika bila kuwa na miundombinu ya msingi kama vile uzalishaji wa umeme wa kutosha na ukuaji wa sekta ya uchukuzi na mawasiliano ambapo Korea Kusini ni wabobezi kwenye masuala hayo.

Alitumia fursa hiyo kumkaribisha Bw. Chang na timu yake kwenda Tanzania kufanya tathmini ya miradi tunayoshirikiana nao, lakini pia miradi mipya kwenye sekta ya uchukuzi kama ujenzi wa Standard Railway Gauge “SRG” kutoka Isaka hadi Kigali, n.k. ambayo ni miradi ya kipaumbele kwa sasa kwa taifa letu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Chang alisifu utendaji kazi wa Rais John Pombe Magufuli, na Serikali ya awamu ya tano ya Tanzania na kusema kuwa utendaji kazi wa aina hii ni wa kupigiwa mfano barani Afrika, na umekuja wakati muafaka tunapoingia kwenye hatua nyingine ya uhusiano wa kiuchumi baina ya nchi zetu mbili. Aidha aliongeza kuwa, wakati umefika sasa wa kufanya kazi, nay eye yuko tayari kufanya kazi na Tanzania kwani Serikali yake, imetoa kipaumbele kwa nchi hii.

Korea Exim Bank ni taasisi ya Serikali inayosimamia mikopo na misaada ya Jamhuri ya Korea inayotoa kwa nchi nyingine. Katika kipindi cha miaka minne (tangu 2016 hadi 2020), Korea Kusini kupitia taasisi hiyo, imeongeza mikopo ya maendeleo kwa bara la Afrika kwa asilimia 20. Uamuzi wa Serikali iliyokuwa madarakani mwaka 2016 wa kuichagua Tanzania kupokea kiasi kikubwa cha msaada huo kuliko nchi nyingine ya Afrika, umeendelezwa na Serikali iliyopo sasa madarakani ya Mheshimiwa Moon Jae-in, Rais wa Jamhuri ya Korea.

Ujumbe wa Mheshimiwa Augustine Mahiga pia ulikutana na kufanya mazungumzo na Bw. Judong Kim, Makamu Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara na Viwanda ya Korea (Korea Chamber of Commerce and Industries KCCI), ambapo Waziri Mahiga aliwasisitiza kuja Dar es salaam kuangalia fursa zilizopo ili kuwashawishi wanachama wao kutafuta bidhaa na masoko nchini Tanzania.

Akielezea umuhimu wa KCCI kuzuru Tanzania na kujifunza soko la biashara, Bw. Edwin Rutageruka Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE aliyeongozana na ujumbe wa Mheshimiwa Waziri Mahiga, alisema njia nzuri ya kupata picha halisi ni kupitia Maonesho ya Biashara ya Saba Saba. Hivyo alitumia fursa hiyo kualika ujumbe wa KCCI kushiriki kwenye maonesho ya 42 yanayotarajiwa kuanza tarehe 28 Juni – 10 Julai, 2018.

Kabla ya kuhitimisha ziara yake, Mheshimiwa Mahiga pia alikutana na kufanya mazungumzo na watendaji wakuu wa makampuni ya DOHWA, ambao wamejikita kwenye ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya reli n.k. Makampuni mengine ni KORAIL, STX Engine, KTMI & STX Offshore pamoja na GS E&C, ambao wote wameonesha nia ya kuwekeza au kufanya biashara nchini Tanzania. Ujumbe mkuu kwa taasisi na makampuni hayo ulikua ni kupanua fursa za ushirikiano wa biaashara na uwekezaji, ubadilishanaji wa ujuzi na ujengaji uwezo wa wafanyakazi ambao ndio nguvu kazi ya taifa letu.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: