Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Maria Mashingo akipiga chapa ng’ombe katika Kijiji cha Igalula Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi mapema leo alipokwenda kuhamasisha zoezi la upigaji na kuwataka wafugaji kuhakikisha mifugo yote inapigwa chapa ifikapo Januari 31 mwaka huu.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Mifugo) Dk. Maria Mashingo akiwaonesha wafugaji sehemu sahihi ambayo ng’ombe anatakiwa kupigwa chapa ili kuepuka kuiraribu ngozi baada ya kushiriki zoezi la upigaji chapa katika Kijiji cha Igalula wilayani Tanganyika mkoani Katavi leo.

Na Kumbuka Ndatta, WMUV

KATIBU Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dk. Maria Mashingo amewataka wafugaji kuhakikisha wamekamilisha zoezi la upigaji chapa mifugo yao kabla ya muda ulioongezwa na Serikali wa hadi Januari 31 mwaka huu kwani baada muda huo kupita haijulikani Serikali itaamua nini kuhusu mifugo itakayokuwa haijapigwa chapa.

Akizungumza wakati akishiriki zoezi la upigaji chapa mifugo katika Kijiji cha Igalula Kata ya Mpanda ndogo Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi, Dk. Mashingo alisema zoezi hilo la upigaji chapa linatekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya utambuzi ,usajili na ufuatiliaji wa mifugo Na. 12 ya Mwaka 2010 .

Dk. Mashingo alisema upigaji chapa umelenga kudhibiti magonjwa ya mifugo,wizi wa mifugo, uimarishaji usalama wa afya na mazao ya mifugo sambamba na kudhibiti usafirishaji na uhamaji wa mifugo kiholela na kuimarisha biashara ya mifugo na mazao yake kitaifa na kimataifa.

"Wafugaji hakikisheni mifugo yenu yote inapigwa chapa kwani baada ya Januari 31 mwaka huu hatujui Serikali itaamua nini kwa mifugo itakayokuwa haijapigwa chapa "alisema.

Dk. Mashingo alisema pamoja nia njema ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuwatetea wafugaji wanaofanyiwa vitendo vya uonevu na mamlaka nyingine za Serikali pia aliwahimiza kutii sheria za nchi kwa kutoingiza mifugo yao kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kwa mujibu wa sheria.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: