Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (R) Semistocles Kaijage akizungumza na waandishi wa habari nje ya mkutano wa Tume na viongozi wa vyama vya siasa.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (R) Semistocles Kaijage (katikati waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja viongozi kutoka vyama vyama vya siasa 19 vilivyoshiriki mkutano huo.Kulia kwake ni Makamu Mwenyekiti Jaji Mkuu Mst. (Znz) Hamid Mahmoud Hamid na kushoto ni Mkurugenzi wa Uchaguzi Kailima Ramadhani na Mjumbe wa Tume Jaji Mst. Mary Longway (wa pili kushoto na viongozi wengine waalikwa katika mkutano huo.

Picha na Hussein Makame-NEC.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imevitaka vyama vya siasa vitumie utaratibu uliopo wa kisheria na kikanuni kuwasilisha malalamiko juu ya mambo yanayojitokeza wakati wa uchaguzi badala ya kuitaka Tume ishughulikie malalamiko ambayo haina mamlaka nayo.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa NEC Jaji, Semistocles Kaijage wakati akifungua mkutano wa Tume na viongozi wa vyama vya siasa uliofanyika jijini Dar es Salaam leo.

Alisema kuwa uzoefu wa chaguzi zilizopita umeonyesha kuwa viongozi wa vyama vya siasa wamekuwa wakifuata vyema taratibu zilizowekwa chini ya Sheria za Uchaguzi katika hatua ya uteuzi wa wagombea katika chaguzi.

Hata hivyo, alibainisha kuwa katika hatua za kampeni hadi kutangaza matokeo, baadhi ya vyama vya siasa na wagombea wao mara kadhaa wameshindwa kufuata taratibu zilizoainishwa katika Sheria za Uchaguzi na Maadili ya Uchaguzi hasa pale ambapo viongozi hao wagombea wanaona haja ya kuchukuliwa hatua dhidi ya uvunjwaji wa Sheria, Kanuni au Maadili ya Uchaguzi na au taratibu za Uchaguzi.

“Tume inachukua fursa hii kuwakumbusha viongozi wa vyama vya siasa kuwa kwenye Maadili ya Uchaguzi, Sheria za Uchaguzi na kwenye Sheria nyingine za Nchi umewekwa utaratibu fasaha wa jinsi na namna ya kushughulikia malalamiko yanayohusu na kugusa ukiukwaji wa Sheria, taratibu na Maadili ya Uchaguzi” alisema Jaji Kaijage.

Alifafanua kuwa miongozo hiyo imetaja na kuainisha adhabu na hatua mbalimbali za kisheria na kikanuni dhidi ya mgombea yeyote, chama chochote, Afisa wa Uchaguzi yeyote na hata kwa mwananchi yeyote anayekiuka Sheria za Nchi au Maadili ya Uchaguzi.

Aliongeza kuwa Sheria na Kanuni za Uchaguzi zimeweka mamlaka na taratibu za kushughulikia malalamiko ya ukiukwaji wa Sheria, taratibu na Maadili ya Uchaguzi.

“Kwa kuzingatia ukweli huu, Tume inaviasa vyama vyote vya siasa na wafuasi wao kutopendelea utaratibu wa kutafuta ufumbuzi wa kiutawala kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika mambo au masuala ambayo Tume haina mamlaka nayo na ambayo utatuzi wake unahitaji kufuata taratibu za Kisheria na Kikanuni.” Alisema.

Alisema utaratibu huo umewekwa bayana kwenye kipengele cha 2.3(e) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015 ambacho pamoja na mambo mengine kinasisitiza malalamiko yeyote yafikishwe kwenye mamlaka inayohusika kwa utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa Sheria.

“Tume ya Uchaguzi inashauri kwa mara nyingine kuwa ni vyema vyama vya siasa, kwa kadri inavyowezekana, vitumie utaratibu uliopo wa Kisheria na Kikanuni kuwasilisha malalamiko yanapojitokeza wakati wa Kampeni, kabla na baada ya kuhesabu kura na baada ya matokeo ya kura kutangazwa.” alisisitiza Jaji Kaijage.

Naye Mkurugenzi wa Uchauzi Kailima Ramadhani alisema kuwa maandalizi ya uchaguzi mdogo katika majimbo matatu na kata sita yamekamilika kwa asilimia kubwa huku vifaa vyote vinavyohitajika kwa ajili ya uchaguzi huo vimeshasafirishwa kwenye halmashauri zote zinazoshiriki uchaguzi huo ikiwemo karatasi za kura.

Alisema wapiga kura 278,137 wanategemewa kupiga kura katika uchaguzi mdogo wa Ubunge majimbo matatu na 324,435 katika uchaguzi mdogo wa Madiwani katika kata sita wakati katika uchaguzi mdogo wa Februari 17, 2018 wa majimbo mawili ya Siha na Kinondoni, wapiga kura 319,482 wanategemewa kupiga kura na 27,120 katika uchaguzi mdogo wa Madiwani katika Kata nne.

Katika mkutano huo ulioshirikisha Tume, viongozi wa vyama vya siasa, mwakilishi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, Mkuu wa Jeshi la Polisi na Serikali, viongozi wa vyama vya siasa waliwasilisha malalamiko yao na kupatiwa majibu kutoka Tume na Jeshi la Polisi.

Mkutano huo wa Tume na viongozi wa vyama vya siasa umejumuisha maandalizi ya uchaguzi mdogo wa ubunge katika majimbo ya Longido, Singida Kaskazini na Songea Mjini na Kata 6 unaotarajia kufanyika Januari 13, 2018 na ule wa majimbo 2 na kata 4 utakaofanyika tarehe 17 Februari mwaka 2017.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: