Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Makamu wa Rais (Sera na Uratibu), Profesa Faustine Kamuzora (kulia), na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Amina Khamisi Shaaban, wakisaini hati za makabidhiano ya sh. trioni moja zilizotolewa na Shirika la Global Fund kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kusaidia mapambano ya Ukimwi, TB na Malaria katika hafla iliyofanyika Ofisi ya Waziri Mkuu jijini Dar es Salaam leo. Wengine waliosimama katikati ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na viongozi wengine kutoka Global Fund.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk. Mpoki Ulisubisya, akizungumza katika hafla hiyo.
Balozi wa Ufaransa Nchini Tanzania, Frederic Clavier, akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mnufaika wa Global Fund, Joan akielezea jinsi alivyo nufaika na shirika hilo.
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu wanaishi na VVU-Ukimwi, Mwinuka Juastine, akizungumza.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Amina Khamisi Shaaban (kulia), akimkabidhi hati ya makabidhiano Mwakilishi wa Global Fund Tanzania, Linden Morrison.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Makamu wa Rais (Sera na Uratibu), Profesa Faustine Kamuzora, akizungumza.
Taswira ya ukumbi wa mkutano katika uzinduzi huo.

Na Dotto Mwaibale

SHIRIKA la Kimataifa la Global Fund limetoa shilingi trioni moja kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya mapambano ya magonjwa ya ukimwi, malaria na kifua kikuu kwa mwaka 2018-2020.

Akizungumza katika hafla ya kutiliana saini makabidhiano ya fedha hizo baina ya mfuko huo na serikali Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema fedha hizo ni muhimu sana kwa nchi yetu.

Alisema fedha hizo zitaelekezwa katika kupambana na magonjwa hayo ambapo kwa ugonjwa wa ukimwi zimetolewa sh.bilioni 769, TB sh. bilioni 67 wakati malaria sh.bilioni 320.

Alisema fedha hizo zitatumika kikamilifu kwa lengo lililokusudiwa na zitasimamiwa na Ofisi ya Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Afya na Mashirika Yasiyo ya kiserikali.

Alisema katika masuala ya ukimwi zitatumika kwa ajili ya vipimo, dawa za kurefusha maisha na kufubaza virusi kwa wagonjwa wa ukimwi na katika ugonjwa wa malaria fedha hizo zitatumika kwa ajili ya vipimo na matibabu pamoja na kununua vyandarua.

"Kwa upande wa wagonjwa wa TB ni asilimia 40 tu ndio waliofika kwenye vituo vya afya na kuthibitika kuwa na maambukizi na wamepatiwa matibabu lakini tunataka hadi ifikapo mwaka 2020 tunataka asilimia 70 ya watanzania watakaogundulika kuwa na maambukizi wajulikane na wapatiwe matibabu" alisema Ummy.

Ummy aliongeza kuwa kati ya wagonjwa 100 wenye maambukizi ya TB wagonjwa 90 waliothibitika kuwa na maambukizi walitibiwa na kupona kabisa.

Katika hatua nyingine Waziri Ummy amewataka Katibu Mkuu wa Wizara yake, Tamisemi na Ofisi ya Rais kuhakikisha wanazisimamia vizuri fedha hizo ili kupata matokeo mazuri waliyo yakusudia.

Mratibu wa Watu Wanaotumia Dawa za Kulevya Tanzania (TANPUD), Happy Assan alisema mradi huo utawasaidia sana na kuhakikisha hawataathirika ukizingatia kuwa fedha hizo zitawafikia walengwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu wanaishi na VVU-Ukimwi, Mwinuka Juastine alisema mradi Global Fund imewasaidia waathirika 900,000 kwa kuwapa dawa za kupunguza makali ya ukimwi ARV na kufubaza virusi vya ugonjwa huo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: