Na Mwandishi Wetu.

Manispaa ya Kinondoni imepongezwa kwa hatua nzuri waliyoifikia katika kutekeleza miradi ya DMDP kwa viwango vilivyokusudiwa, ikiwa ni pamoja na kulipa fidia maeneo yaliyopitiwa na mradi.

Pongezi hizo zimetolewa leo na Naibu Waziri wa Nchi ofisi ya Rais anayeshughulikia Afya, Miundombinu, na uwekezaji Mh. Josephat Kandege alipofanya ziara Wilayani hapo kujionea hali halisi ya utekelezaji pamoja na hatua iliyofikiwa miradi hiyo.

Amesema miradi hii ikikamilika italeta taswira nzuri ya Kinondoni na pia utekelezaji wake unakwenda sambamba na ulipaji wa fidia kwa wale ambao wamepitiwa na mradi na tathmini imekwisha fanyika.
 "Mimi niseme nimefarijika, nimefurahia jinsi ambavyo miradi inakwenda na kubwa zaidi ninalowaomba nikatika kuhakikisha kwamba wale ambao wanatakiwa walipwe fidia walipwe kwa wakati " Amesema Naibu Waziri.

Naye Mratibu wa Miradi ya DMDP Manispaa ya Kinondoni Ndg Mkerewe Tungaraza katika taarifa yake ya mradi kwa Naibu Waziri amesema Kinondoni inatekeleza mradi huu kwa kipindi cha miaka mitano (2016-2020), na kazi zinazotekelezwa zimegawanyika katika awamu mbili.

Amezifafanua awamu hizo mbili na kazi zitakazofanyika kuwa ni uboreshaji wa miundombinu pamoja na uboreshaji wa maeneo ya makazi ya wananchi kwa awamu zote.
Katika hatua nyingine Naibu waziri huyo ameitaka mamlaka ya barabara vijijini (TARURA) kuwa na utaratibu wa kufanya ukarabati wa barabara mara zinapoonyesha kuharibika ili kuepusha uharibifu mkubwa unaoweza kutokea.

Naibu Waziri ametembelea miradi ya barabara za Makumbusho, viwandani Msasani Soko la Samaki pamoja na jengo la ofisi ya DMDP ambalo limekamilika kwa asilimia 97.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: