Na Mashirika ya Kimataifa.
Kamishna wa Tume ya Uchaguzi nchini Kenya Roselyn Akombe ametangaza kujiuzulu, siku saba pekee kuelekea Uchaguzi mpya wa urais uliopangwa kufanyika Octoba 26 mwaka huu.
Akombe ametoa tangazo hilo akiwa jijini New York nchini Marekani, na kusema kuwa hawezi kuendelea kufanya kazi katika Tume hiyo, aliyoielezea kugawanyika.
Aidha, amedokeza kuwa mazingira ya sasa ya kisiasa hayawezi kuruhusu kufanyika kwa Uchaguzi utakaokuwa huru na haki.
“Siwezi kuendelea kufanya kazi, katika mazingira kaa haya, kila dalili zinaonesha wazi kuwa Uchaguzi hauwezi kuwa huru na haki,” alisema Akombe akiwa Marekani.
Bi Akombe aliondoka nchini Kenya siku ya Jumanne, kwenda Dubai kushuhudia uchapishwaji wa karatasi za kupigia kura lakini akaamua kwenda nchini Marekani, ambako pia ni raia wa nchi hiyo.
Kujiuzulu kwa Bi. Akombe, ni pigo kwa Tume hiyo ambayo ilikuwa inamtegemea kuzungumza kwa niaba yake na kuitetea mara kwa mara.
"Tume ijitokeze wazi, iwe na ujasiri na kusema kuwa Uchaguzi huu hauwezi kuwa huru na haki katika mazingira haya," aliongeza Akombe.
Amesema pia alikuwa anapata vitisho kuhusu maisha yake na huenda asirejee nchini Kenya
katika siku za hivi karibuni.
Suba Churchil, kiongozi wa mashirika ya kiraia amesema hali hii inaendelea kuzua wasiwasi kuhusu Uchaguzi huo uliopangwa kufanyika wiki ijayo.
Toa Maoni Yako:
0 comments: