Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini (RFB), Bw. Joseph Haule, akisisitiza jambo wakati akitoa taarifa ya ukaguzi wa kiufundi na fedha kwa fedha zilizopelekwa na mfuko huo katika halmashauri mbalimbali nchini kwaajili ya ujenzi wa barabara kwa waandishi wa habari (hawapo pichani), mjini Dodoma.
Sehemu ya Wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini (RFB), wakimsikiliza Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini (RFB), Bw. Joseph Haule hayupo pichani), wakati akitoa taarifa ya ukaguzi wa kiufundi na fedha kwa fedha zilizopelekwa na mfuko huo katika halmashauri mbalimbali nchini kwa mwaka wa fedha 2015/16, mjini Dodoma leo.
Meneja wa Mfuko wa Barabara nchini (RFB), Bw, Eliud Nyauhenga akisisitiza jambo mara baada taarifa ya ukaguzi wa kiufundi na fedha kwa fedha zilizopelekwa na mfuko huo katika halmashauri mbalimbali nchini kwa mwaka wa fedha 2015/16 kuwasilisha na Mwenyekiti wa Bodi ya mfuko huo Bw. Joseph Haule , mjini Dodoma leo.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Halmashauri zote nchini zilizobainika kutumia fedha za miradi ya ujenzi wa barabara kinyume cha utaratibu kwa kubadili matumizi na kulipa miradi hewa zimetakiwa kuzirudisha fedha hizo katika Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) ili zikafanye kazi iliyokusudiwa.

Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini (RFB), Bw. Joseph Haule, amesema hayo wakati akitoa taarifa ya ukaguzi wa kiufundi na fedha kwa fedha zilizopelekwa na mfuko huo katika halmashauri mbalimbali nchini kwaajili ya ujenzi wa barabara na kutumika kwa kazi nyingine.

“Haikubaliki yaani zaidi ya shilingi millioni 400, zitumike kinyume cha utaratibu kwa kununua madawati, kompyuta, vifaa vya ofisi, kujenga maabara za shule za sekondari na matumizi hewa kinyume na utaratibu wa matumizi ya fedha za mfuko wa barabara”, amesema Bw, Haule.

Mwenyekiti huyo wa RFB amezitaja halmashauri zinazohusika na matumizi mabaya ya fedha za barabara kuwa ni Jiji la Tanga, Manispaa ya Mtwara, Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Moshi, Songea, Kilolo, Nanyumbu, Masasi na Ushetu.

Nyingine ni halmashauri ya wilaya ya Kyerwa, Karagwe, Ngorongoro, Meru, Kondoa, Kakonko, Kalambo, na Gairo.

Bw, Haule amesisitiza kuwa hatua za kinidhamu na kijinai kwa wote watakaobainika kuhusika na matumizi mabaya ya fedha za mfuko wa barabara zichukuliwe mara moja.

Naye meneja wa mfuko wa barabara Bw, Eliud Nyauhenga amesema wamejipanga kuhakikisha fedha za barabara zinatumika kama ilivyokusudiwa na bodi imeongeza wataalam wa ukaguzi wa miradi inayotumia fedha za mfuko huo hivyo kuzitaka halmashauri kuongeza umakini katika utekelezaji wa miradi ya barabara.

“Nasisitiza umuhimu wa halmashauri zote kushirikiana na maabara za Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), zilizoko mikoani ili kuwezesha kazi za ujenzi wa barabara zinazofanyika kuwa na ubora na viwango” amesema Bw, Nyauhenga.

Bodi ya Mfuko wa barabara ambayo hutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara katika halmashauri nchini imewataka wahandishi wanaosimamia fedha hizo kuongeza ufanisi ili kuwezesha fedha hizo kutekeleza miradi mingi kwa wakati na kwa kuzingatia thamani ya fedha.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: