Na Jumia Travel Tanzania.

Kila ifikapo Septemba 27 ya kila mwaka dunia huadhimisha siku ya utalii duniani. Maadhimisho hayo hufanywa na kila nchi ambapo kunakuwepo na shughuli kadhaa zikiongozwa na malengo na kauli mbiu tofauti zilizoazimiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UNWTO).
Mnamo mwaka 2015, Mkutano Mkuu wa Baraza la Umoja wa Mataifa uliutangaza mwaka 2017 kama Mwaka wa Kimataifa wa Utalii Endelevu kwa Maendeleo. Na hivyo kuifanya kauli mbiu ya mwaka huu kuwa ni ‘Utalii Endelevu kwa Maendeleo.’

Maeneo matano ambayo yanaangaziwa na kufanyiwa kazi mwaka huu ni; Ukuaji wa uchumi endelevu na wa pamoja; Ujumuishwaji wa jamii, ajira na kupunguza umasikini; Ufanisi wa rasilimali, utunzaji wa mazingira na mabadiliko ya hali ya hewa; Amali za kiutamaduni, utofauti na urithi; na Maelewano ya pamoja, amani na usalama.
Katika kuunga mkono maadhimisho haya, Jumia Travel ikiwa ni mdau wa masuala ya utalii Tanzania na Afrika kwa ujumla imekuwa ikifanya jitihada za kukuza ufahamu juu ya maeneo na vivutio mbalimbali vya utalii nchini.

Hivi sasa kuna kampeni inayoendelea kwa jina la ‘Destinations Campaign’ ikiwa inalenga kukuza ufahamu juu ya maeneo tofauti nchini ambayo watanzania hawafahamu kama ni vivutio vya kitalii.

Tanzania imebarikiwa kuwa na maeneo mengi lakini hayapewi kipaumbele wala kutangazwa vilivyo. Na endapo ikiwa yanatangazwa, sio yote yanayopata fursa sawa kama vile Zanzibar, Mlima Kilimanjaro na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo watu wengi nchini na duniani wanayafahamu.
Jumia Travel imeamua kuitumia fursa ya kufanya kazi na maelfu ya hoteli nchini na Afrika kuyaangazia maeneo hayo na sehemu ambazo wageni wanaweza kulala. Kikubwa kinachofanyika ni kuwafahamisha watanzania juu ya shughuli tofauti wanazoweza kuzifanya pindi wakitembelea maeneo hayo. Mbali na hapo wamiliki na mameneja wa hoteli huhojiwa juu ya masuala wanayoona yanaweza kuwavutia wateja kwenye hoteli zao.

Jitihada za kukuza ufahamu na kutangaza maeneo mbalimbali nchini zinafanywa pia na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB). Bodi ya Utalii imekuja na mkakati na mbinu mpya kwa kuyatenga maeneo ya usimamizi wa wanyama tofauti na ya kawaida yaliyozoeleka na watalii wengi.

Kwa mfano, hivi sasa TTB inafanya jitihada kubwa za kukuza maeneo matano yaliyomo kwenye mpango wa usimamizi huo ambayo ni Burunge ipo Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara, Randilen ipo Wilaya ya Monduli mkoa wa Arusha, Ikona ipo katika Wilaya ya Serengeti mkoa wa Mara jirani na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Ipole ipo katika Wilaya ya Sikonge mkoa wa Tabora na Mbomipa ambayo ni muunganiko wa vijiji zaidi ya 21 vya tarafa za Idodi na Pawaga vinavyozunguka Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Kwa kufanya hivyo inatoa fursa kwa watalii kuwa na machaguo ya sehemu za kutembelea tofauti na yaliyozoeleka. Kwa sababu hata kwenye maeneo haya watalii wanaweza kukidhi haja zao kwa kuwaona wanyama na kufanya shughuli nyinginezo za kitalii.

Kwa mujibu wa ripoti ya utalii ya mwaka 2016 iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Kimataifa la Utalii Duniani, Mwaka 2016 umethibitisha kuwa ni mwaka mwingine wa mafanikio katika sekta ya utalii kimataifa licha ya changamoto kadhaa. Idadi ya watalii kimataifa imekuwa kwa mwaka wa saba mfululizo na kufikia bilioni 1.2, idadi ya ukuaji ambayo haijawahi kutokea tangu miaka ya ‘60’ (1960). Ukuaji mkubwa zaidi umeonekana kwenye sehemu za Afrika, Asia na Pasifiki.
Tunakukaribisha katika kuungana nasi na kusherehekea Mwaka wa Kimataifa wa Utalii Endelevu kwa Maendeleo 2017.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: