Meneja matukio wa Dimba Music Concert, Mwani Nyangassa, akizungumza na waandishi wa Habari jana kutambulisha wanamuziki watakaoshiriki katika tamasha hilo, litakalofanyika Septemba 2 kwenye ukumbi wa Travertine, Hotel Magomeni. Kushoto ni Mhariri wa Dimba Jimmy Chika na kulia ni Meneja Masoko wa Kampuni ya New Habari (2006) LTD Michael Budigila.
Baadhi ya wanamuziki watakaoshiriki Dimba Music Concert, wakiwa na Kamati ya Maandalizi jana mbele ya waandishi wa habari katika Ofisi za New Habari (2006) LTD.
Wanamuziki Juma Kakere, Ally Choki, Hussein Jumbe na Juma Katundu, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kutambulishwa kutumbuiza katika Tamasha hilo Septemba 2.
Mhariri wa Dimba, Jimmy Chika, akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanamuziki na wajumbe wa kamati ya maandalizi ya Dimba Concert.
---
Kampuni ya New Habari (2006) LTD kupitia gazeti lake la DIMBA, imeandaa onesho maalum la muziki wa dansi DIMBA Music Concert litakaofanyika Septemba 2 mwaka huu katika Ukumbi wa Traventine Magomeni jijini Dar es Salaam.
Onesho hilo lina lengo la kuukuza na kupromoto muziki wa dansi, ambao umekuwa ukielekea kupotea kila kukicha.
Katika onesho hilo kutakuwepo na mpambano wa wanamuziki wa dansi, ambapo bendi ya Msondo Ngoma Music (Baba wa Muziki), itachuana na mastaa mbalimbali wa muziki huo kutoka bendi mbalimbali nchini.
Kundi la mastaa ambao tumewapa jina la ‘Timu ya Taifa ya Muziki wa Dansi,’ litakalochuana na Msondo Ngoma, litaundwa na wanamuziki kama Kikumbi Mwanza Mpango' King Kiki', Hassan Rehani Bitchuka 'Stereo', Karama Regesu, Ally Choky, Juma Kakere, Nyoshi El-Saadat ‘Sauti ya Simba’ na Muumini Mwinjuma.
Kwa upande wa vyombo, watakuwepo wapiga vyombo Saadi Ally 'Machine' kwenye dramu, gitaa la solo likitekenywa na Aldofu Mbinga wakati besi litangurumishwa na Hosea Mhogachi.
Aidha, kinanda kitatekenywa Juma Jerry wakati tumba zitakung'utwa Salum Chakuku 'Kuku Tumba', ambapo ala za upepo watakuwepo Ally Yahaya, Hamis Mnyupe Tarumbeta na Shaabani Lendi kwenye Saksafoni.
"Utakua ni usiku wa mastaa wa dansi kuionyesha kazi Msondo Ngoma, kwani miaka ya hivi karibuni imekua ikikosa mbabe katika kila bendi inayoshindanishwa nayo lakini safari hii tumeamua tuwaonyeshe kazi."
Kiingilio katika onesho hilo litakaloanza kuanzia saa 2:00 usiku hadi majogoo, kitakuwa ni shilingi 10,000 kwa wote na 20,000/- kwa VIP.
IMETOLEWA NA MENEJA WA TUKIO ‘DIMBA MUSIC CONCERT’ MWANI NYANGASSA.
Toa Maoni Yako:
0 comments: