Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuachia huru Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ambaye alikuwa anakabiliwa na mashitaka ya kutumia lugha chafu dhidi ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinari Pengo.
Askofu Gwajima ameachiwa huru chini ya kifungu cha 225 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA). Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Cyprian Mkeha ameifuta kesi hiyo baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuleta mashahidi kwa takribani miaka miwili.
Kabla ya kufutwa kesi hiyo, Wakili wa Serikali, Joseph Maugo aliieleza mahakama hiyo kuwa leo kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kusikilizwa na kwamba hawana shahidi hivyo wanaomba ahirisho lingine.
Hakimu Mkeha amesema kwa muda wa miezi 14, upande wa mashitaka umeweza kuleta shahidi mmoja pekee hivyo anafuta kesi hiyo.
Awali, katika shauri lililopita aliutaka upande wa mashitaka kuhakikisha wanaleta mashahidi kusikiliza kesi hiyo.
Awali ilidaiwa kuwa, kati ya Machi 16 na 25, mwaka jana maeneo ya Tanganyika Packers Kawe Askofu Gwajima alitumia lugha chafu ya matusi dhidi ya Askofu Pengo.
Inadaiwa alimuita; Ni mpuuzi mmoja mjinga mmoja asiyefaa mmoja anaitwa Askofu Pengo aliropoka sijui amekula nini mimi naitwa Gwajima namwita mpuuzi yule mjinga yule na kuonesha Pengo ni mtoto mpuuzi na mwenye akili ndogo na kwamba maneno hayo yangeweza kuleta uvunjifu wa amani.
Toa Maoni Yako:
0 comments: