Kiongozi mkuu wa waislam mkoa wa Mbeya na Songwe Shekh Mwalimu Ally Mohamed Mwansasu, amewataka waandishi wa habari kote nchini kukemea usaliti unaofanywa na baadhi ya viongoji wa jamii.

Hayo aliyasema jana katika ukumbi wa Tughimbe mjini Mbalizi mkoani hapa, wakati wa uzinduzi wa kitabu kiitwacho Nguvu yangu dhidi yao kilichoandikwa na Mwandishi wa habari Gordon Kalulunga.

Alisema ndani ya kitabu hicho mwandishi kafanya kazi nzuri ya kukemea usaliti, rushwa, kuwakumbusha wabunge wajibu wao, kueleza umuhimu wa kijana wa Afrika kulinda utamaduni wao na kuionyesha serikali na jamii matatizo yaliyopo nchini na namna ambavyo yanaweza kupunguzwa ama kumalizwa likiwemo suala la wizi wa dawa hospitalini.

"Niwashawishi watanzania hasa viongozi kukitafuta kitabu hiki cha kijana wetu Kalulunga kitawasaidia na uongozi bora hupatikana kwa mtu mwenye maadili" alisema Shekh Mwansasu huku akimsihi mwandishi huyo kuchapisha kitabu kingine kikihusu viwanda.

Naye Afisa elimu wa mamlaka ya mji mdogo wa Mbalizi Mwalimu Fredrick Silumbwe alisema wasomi waache kulalamika badala yake wawe wafumbuzi wa matatizo ya jamii.

Alisema mwandishi wa kitabu hicho amekuwa mfano wa wasomi wachache wanaoweza kuthubutu na kwamba makala zilizomo ndani ya kitabu zinafunza ikiwemo andiko lisemalo Magufuli Kajinyonyoa, Mwalimu wa wabunge na mengine.
Gordon Kalulunga (kushoto) na rafiki yake wakishika kitabu kilichozinduliwa.

Kaimu mgeni rasmi katika uzinduzi huo Kissman Mwangomale ambaye pia ni diwani wa kata ya Utengule Usongwe kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji wa Tunduma Hotel Hemedy Steven alisema anawategemea sana waandishi wa habari katika kuionyesha jamii na serikali matatizo yaliyopo ili kuyatafutia ufumbuzi.

"Kijana wetu Kalulunga amefanya kazi kubwa na kinachofurahisha kitabu kimesheheni masuala ya Afya, uchumi na siasa ambacho kwangu na wengine kitakuwa dira ya utendaji wetu na kukua zaidi kifikra" alisema Mwangomale.

Kwa upande wake Mwandishi wa habari Hosea Cheyo ambaye pia ni makamu Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari mkoa wa Mbeya alisema kuandika vitabu ndiko kunampa mtu kutunukiwa udaktari wa falsafa au u-Profesa.

Mwandishi wa kitabu hicho Gordon Kalulunga ambaye ni mwandishi mbobezi wa habari za Afya ya uzazi dawa za kulevya na Viwanda, miundombinu na ubunifu, alitoa rai kwa Rais Dkt. John Magufuli na wabunge wote kukitafuta kitabu hicho na kukisoma maana kitawapa vitu halisi kwasababu akijabeba hadithi bali uhalisia wa maisha ya watanzania.

"Asili ya mtawala yeyote duniani nadhani na hata Mbinguni hapendi kubezwa. Vijana tuseme ukweli wenye ushahidi na wazee watushauri na kutuonyesha njia huku wastaafu akiwemo Rais Benjamin Mkapa na marais walio hai wasisite kukemea pale raia tunapokengeuka na hata kuwakemea na kuwaelekeza waliopo madarakani" alisema Kalulunga.

Alisema kutokana na nchi iendako kuhusu viwanda, ameandaa kitabu kinachoitwa "Pigilieni misumari ujauzito wangu" kinachoonyesha wajawazito na vichanga wanavyofariki nchini na vikwazo vya serikalini vinavyoathiri uanzishwaji wa viwanda vidogo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: