Alhamis, Machi 16, 2017 kumefanyika Mkutano wa wadau wa zao la mkonge kutoka wilaya ya Meatu mkoa wa Simiyu na wilaya ya Kishapu mkoa wa Shinyanga.

Mgeni rasmi katika mkutano huo ulioandaliwa na shirika la OXFAM na asasi isiyo ya kiserikali inayojishughulisha na Maendeleo ya Jamii (Relief to Development Society- REDESO) alikuwa mkuu wa wilaya ya Kishapu mheshimiwa Nyabaganga Talaba.

Awali akizungumza katika mkutano huo,Mratibu Miradi (uchumi) kutoka shirika la OXFAM Haji Kihwele alisema lengo la mkutano huo kuwaweka pamoja wadau hao ili waweze kufahamiana sambamba na kujadili namna ya kulifanya zao hilo kuwa na tija na manufaa zaidi kwa wakulima na kuwasaidia wakulima hao kupata masoko.

"Tumekutana hapa ili tujadili pia namna ya kumuunganisha mkulima wa mkonge anufaike na masoko yenye faida na kupata uwakilishi mzuri katika sekta hii",alisema Kihwele.

Akizungumza katika mkutano huo,mkuu wa wilaya ya Kishapu mheshimiwa Nyabaganga Talaba aliwataka wadau wa zao la mkonge kwenda kuwekeza kwa kujenga viwanda katika wilaya yake kwani ardhi ipo ya kutosha.

"Wadau wa mkonge njooni Kishapu muwekeze,tunayo ardhi ya kutosha,hivi sasa maji kutoka ziwa Victoria yamefika Kishapu,umeme na barabara zinazopitika kipindi chote zipo,tunataka kulifanya zao la mkonge kuwa rasmi badala ya kutumika kwenye mipaka kutenganisha mashamba na milingoti kwa ajili ya kujengea nyumba",alieleza Nyabaganga.

"Kipindi cha majaribio kimekwisha,tunalima pamba lakini pia tumeamua kulima mkonge,tunataka kilimo hiki kiwe rasmi,wananchi wanajitahidi kulima zao la mkonge lakini changamoto kubwa iliyopo ni ukosefu wa soko hivyo ni vyema ofisi za bodi ya mkonge zikawa na ofisi katika maeneo yanayolima,wakulima wanahitaji kunyanyuliwa kwani hata mikopo inayotolewa haitoshi",aliongeza Nyabaganga.

Miongoni mwa wadau walioshiriki katika mkutano huo ni wakulima na wasindikaji wa zao la mkonge,wazalishaji wa bidhaa za mkonge,taasisi za kifedha ikiwemo Vision Fund,bodi ya mkonge (TSB),Chemba ya wafanyabiashara,wakulima na viwanda (TTCIA),Shirika la kuhudumia viwanda vidogo (SIDO),Umoja wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA),Mtandao wa Asasi za Wakulima (Agriculture Non- State Actors Forum -ANSAF) na viongozi mbalimbali kutoka halmashauri ya wilaya ya Kishapu na Meatu.
Mratibu Miradi (uchumi) kutoka shirika la OXFAM Haji Kihwele akizungumza wakati wa mkutano wa wadau wa zao la mkonge uliofanyika katika ukumbi wa Virgimark Hotel mjini Shinyanga leo Alhamis Machi 16, 2017. Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog.
Wadau wa zao la mkonge wakimsikiliza Mratibu Miradi Kiuchumi kutoka OXFAM Haji Kihwele
Washiriki wa mkutano huo wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Kishapu mheshimiwa Nyabaganga Talaba.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu mheshimiwa Nyabaganga Talaba akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa zao la mkonge kutoka wilaya ya Meatu na Kishapu.
Kulia ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu Boniphace Butondo na Afisa Biashara halmashauri ya wilaya ya Kishapu Konisaga Mwafongo.
Washiriki wa mkutano huo wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea ukumbini.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu Boniphace Butondo na mkuu wa wilaya ya Kishapu Nyabaganga Talaba wakiwa ukumbini.
Mratibu wa Miradi (Ardhi) kutoka OXFAM bi Amina Ndiko akiongezea maelezo kutoka kwa akina mama kutoka Kishapu wanaolima mkonge.
Mkulima wa zao la mkonge kutoka Kishapu Fredina Said akimuonesha mkuu wa wilaya ya Shinyanga Nyabaganga Talaba zulia lililotengenezwa kwa mkonge.
Picha ya pamoja washiriki wa mkutano wa wadau wa zao la mkonge kutoka wilaya ya Meatu na Kishapu.
Picha ya pamoja washiriki wa mkutano huo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: